STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 18.09.2017
SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China imepongezwa kwa jitihada
zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendelea kuwajengea uwezo wafanyakazi
wa sekta ya umma kwa kuwapatia mafunzo ambayo huwasadia katika kufanya kazi zao
kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Gavu aliyasema hayo
leo Ikulu mjini Zanzibar katika mazungumzo kati yake na Hung Yutong ambaye ni Makamo wa Rais wa
Taasisi ya ‘China National Research Institute of Food Fermentation Industries’
kutoka nchini humo.
Katika mazungumzo
hayo, Waziri Gavu alieleza kuwa Serikali ya China ina historia kubwa ya
kuisaidia Zanzibar katika kuwajengea uwezo watendaji wake katika sekta mbali
mbali za maendeleo na kwa hatua ya mara hii ya wakufunzi kutoka nchini humo kuja
kuwapa mafunzo watendaji wanaotoa huduma za upishi na ukarimu kwa viongozi wa
wakuu wa nchi pamoja na walimu kutoka Taaasisi ya Utalii iliyopo Maruhubi ni
jambo la kupongezwa.
Aliongeza kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana juhudi hizo za Serikali ya
Jamhuri ya Watu wa China ambazo zimekuwa
zikitoa mchango mkubwa kwa watendaji wa serikali kupata kujifunza mambo mbali
mbali ambapo baadae elimu yao wanayoipata huifanyia kazi na kuweza kuisaidia
Serikali pamoja na kujiongezea ujuzi na maarifa wao wenyewe.
Waziri Gavu alitoa
shukurani na pongezi kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uongozi
wa Taasisi hiyo ya China kwa kuwaleta wataalamu wake hapa nchini kwa lengo la
kuja kutoa mafunzo hatua ambayo alisema itawawezesha watendaji walio wengi
kupata fursa hiyo muhimu.
Akitoa shukurani maalum,
Waziri Gavu alieleza kuwa hatua ya mafunzo hayo inatokana na juhudi za Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein za
kuimarisha uhusiano na ushirkikiano na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China
katika kuhakikisha nchi hiyo inatoa mafunzo hayo kwa watendaji hao wa Serikali.
Alieleza kuwa ni
matarajio yake na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jumla kuwa walengwa wa
mafunzo hayo watayatumia vyema ili waweze kuongeza ujuzi katika shughuli zao za
kazi sambamba na kuitumia vyema fursa hiyo waliyopewa na Rais ya kushiriki
mafunzo hayo.
Aidha, Waziri Gavu
alieleza matumaini yake kuwa mafunzo hayo hayatakuwa ya mwisho na badala yake
yatakuwa ni mafunzo endelevu kwa wafanyakazi hao na wengineo.
Aliongeza kuwa kwa
vile wakufunzi hao kutoka Chuo hicho kinachuhusiana na masuala la upishi na
ukarimu wana uzoefu na utaalamu mkubwa katika kada hizo, hivyo watendaji hao wa
Serikali watapata kujivunza na kujijengea uwezo mkubwa katika kazi zao.
Nae Makamo wa Rais wa
Taasisi ya ‘China National Research Institute of Food Fermentation Industries’
kutoka nchini China Hung Yutong alieleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
China inathamini uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati yake na Zanzibar.
Makamo huo wa Rais wa
Chuo hicho cha ‘China National Research Institu of Food and Fermentation
Industries’ alimueleza Waziri Gavu uzoefu walionao wataalamu wa chuo hicho
katika masuala yanoyohusiana na mapishi pamoja na ukarimu.
Alieleza kuwa mafunzo
hayo ni mashirikiano ya pamoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambayo yatatolewa na wakufunzi kutoka chuo
hicho huku akieleza uzoefu wa chuo chake kutokana na China kuwa na mahitajio
mengi ya kada hiyo.
Kiongozi huyo ambaye
amefuatana na Mkurugenzi wa Chuo hicho Bi
Luo Yanqin alieleza kuwa ana matarajio makubwa kuwa wataalamu watakaotoa
mafunzo hayo watatumia uzoefu walionao na kuweza kuwasaidia watendaji hao
kuelewa mambo kadhaa ya kitaifa na kimataifa yanayohusiana na kada hizo za
masuala ya upishi, uhudumu na mambo mengineyo ya ukarimu kwa wageni.
Alisisitiza kuwa suala
la masomo katika kada hizo yana umuhimu mkubwa kwa watendaji hao wa Serikali
hasa ikizingatiwa kuwa wakati uliopo mambo mengi yanaenda kwa njia za sayansi
na teknolojia.
Aliongeza kuwa mafunzo
hayo yatawasaidia watendaji hao katika kuendeleza shughuli zao za kazi pamoja
na maeneo yao ya kijamii na hata katika kutekeleza azma ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii.
Pamoja na hayo, Huang
Yutong alieleza kuwa mafunzo hayo yatawasidia watendaji hao kupata kujifunza
upishi wa vyakula mbali mbali vya kitaifa na kimataifa vikiwemo vyakula vya
kichina huku akisisitiza haja ya kuendeleza mashirikiano zaidi ili utaalamu
utakaopatikana uzidi kuleta tija kwa wafanyakazi na Taifa kwa jumla.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment