-
|
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
Tovuti: www.chragg.go.tz
|
Septemba 12, 2017
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
THBUB
yampongeza Rais kwa tamko kuhusu kutotekeleza adhabu ya kifo
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
(THBUB) imepokea tamko la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
John Pombe Magufuli alilolitoa Septemba 11, 2017 kuhusu kutotekeleza adhabu ya
kifo wakati wa uongozi wake, kuwa ni tamko lenye kuzingatia haki ya msingi ya
kuishi.
Tume inapenda kuungana na wadau wengine
kumpongeza Mhe. Rais kwa tamko hilo ambalo limekuja muda mfupi kabla ya Siku ya
Kimataifa ya kuhamasisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kufuta adhabu ya
kifo, ambayo huadhimishwa Oktoba 3 ya kila mwaka.
Uamuzi wa Mhe. Rais unaendana na Mkataba
wa Kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa yanayozitaka nchi wanachama kufuta
au kusimamisha utekelezaji wa adhabu ya kifo (abolition/moratorium on the death
penalty).
Tume inatambua kwamba adhabu ya kifo
haijatekelezwa hapa nchini katika kipindi cha takriban miaka 20 iliyopita na
hivyo kudhihirisha kwamba Tanzania ni nchi isiyotekeleza adhabu ya kifo kwa
hiari yake yenyewe pamoja na uwepo wa adhabu hiyo katika sheria za nchi.
Kwa kuzingatia kauli ya Mhe. Rais pamoja
na mahitaji ya sheria za kimataifa za haki za binadamu, Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora inapenda kuchukua nafasi hii, kuishauri Serikali
iridhie Itifaki ya pili ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa;
Itifaki ambayo inazitaka nchi wanachama kufuta adhabu ya kifo.
Imetolewa
na:
(SIGNED)
Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Septemba 12, 2017
No comments:
Post a Comment