Habari za Punde

Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Wafanya Uchaguzi Katika Ngazi za Wilaya za Kichama.

Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdalla Juma Mabodi akifungua mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya  Kaskazini “A”  kichama katika uchaguzi wa Wilaya  uliofanyika leo katika ukumbi wa CCM MKoa wa kaskazini Unguja Mahonda
Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM Taifa, Dk. Hussein Mwinyi akifungua mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Mjini uliofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni Unguja.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Amani wakifuatilia kwa makini harakati mbali mbali zinazofanyika katika uchaguzi huo huko katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini huko Amani Unguja.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Mjini wakifuatilia kwa makini harakati mbali mbali zinazofanyika katika uchaguzi huo katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni Unguja.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Mjini wakifuatilia kwa makini harakati mbali mbali zinazofanyika katika uchaguzi huo katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni Unguja.
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Kati akipiga kura katika uchaguzi uliofanyika leo huko katika ukumbi wa Skuli ya Dunga.

Na Is-haka Omar, Zanzibar.

CHAMA Chama cha Mapinduzi  (CCM)  leo kimefanya uchaguzi  wa ngazi ya Wilaya katika Mikoa ya Zanzibar ili kupata viongozi watakaoongoza nafasi mbali mbali ndani ya ngazi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.

Katika uchaguzi huo  mamia ya wanachama wa chama hicho wamejitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura kutekeleza haki yao ya kidemokrasia kwa mujibu wa Katiba ya CCM.

Akifungua Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Kaskazini  “A” kichama  Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Mahonda, amewasihi wajumbe wa mkutano huo kutumia vyema fursa hiyo kwa kuwachagua viongozi makini na wachapa kazi.

Alisema katika uchaguzi wa ndani wa CCM unakuwa ni wa wanachama wote hivyo baada ya uchaguzi walioshinda na wale ambao kura zao hazikutosha wanatakiwa kushirikiana katika harakati mbali mbali za kuleta maendeleo ndani ya chama.

Dk. Mabodi alieleza kuwa viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huo ndio jeshi la kisiasa litakaloweza kufanikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu wa dola wa mwaka 2020.

Alisema katika kujenga dhana ya CCM mpya na Tanzania mpya chama hicho kimedhamiria kuondosha vitendo vyote vya rushwa, ufisadi, makundi , safu na usaliti ili kuimarisha misingi ya demokrasia na uhuru kwa kila mwanachama ndani ya CCM.

“ CCM Zanzibar haitoweza kuruhusu vitendo vya rushwa, makundi na usaliti vitokee katika uchaguzi unaoendelea na mara baada ya uchaguzi kwani lengo letu ni kukisafisha chama kiwe na viongozi waadilifu watakaosimamia maslahi ya wananchi kwa uzalendo.”alisisitiza Dk. Mabodi.

Pamoja na hayo aliwataka viongozi watakaochaguliwa kubuni miradi endelevu ya kiuchumi na kichama itakayoimarisha siasa katika masuala ya Itikadi kwa kupata wanachama ambao ni makada wenye uzalendo na imani ya kuitumikia CCM katika mazingira yoyote.

Naye Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM Taifa,  Dk.Hussein Mwinyi akifungua mkutano  Mkuu wa CCM Wilaya ya Mjini, alisema ukomavu wa kisiasa ulioonekana katika chaguzi za ngazi za matawi hadi majimbo uliokamilika bila kutokea vurugu ama dalili za rushwa ndio matarajio yanayotegemewa kuonekana katika uchaguzi wa ngazi zilizobaki.

Alisema kwa sasa CCM imeamua kujisahihisha kwa kutorudia makosa yaliyokuwa yakitokea katika chaguzi za ndani ya chama zilizopita hivyo viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huo wafuate Katiba na kanuni  za chama cha mapinduzi.

Dk. Mwinyi alisema baada ya uchaguzi huo wanachama wa chama hicho wanatakiwa kuendeleza mshikamano wa kuhakikisha wanajiandikisha kwa wingi katika daftari la wapiga kura pamoja na kuongeza wanachama wapya ili kujiimarisha kisiasa katika uchaguzi mkuu wa dola ujao.

Katika uchaguzi huo nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti wa Wilaya , Katibu wa Siasa na Uenezi, nafasi ya mkutano Mkuu wa Mkoa , nafasi ya Mkutano Mkuu wa taifa pamoja na nafasi ya Halmashauri kuu ya CCM Wilaya,

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.