Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akisalimiana na Balozi wa Saudi Arabia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Mohammed Mansour Al Malik,alipofika Ikulu Mjini Unguja leo,16/10/2017.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Balozi wa Saudi Arabia katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Mohammed Mansour Al Malik, alipofika Ikulu Mjini Unguja leo,[Picha na Ikulu.]
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 16.10.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewakaribisha wawekezaji wa sekta ya utalii
kutoka nchini Saud Arabia kuja kuekeza Zanzibar kutokana na fursa zilizopo hapa
nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo Ikulu mjini Zanzibar katika mazungumzo kati yake na Balozi wa Saud Arabia
nchini Tanzania Mohammed Mansour Al Malik.
Katika mazungumzo hayo, Dk.
Shein alimueleza Balozi huyo kuwa kutokana na Saud Arabia kuwa na wawekezaji
wakubwa waliowekeza katika sekta ya utalii nchini humo na hata nje ya nchi yao
kuna haja ya kuja Zanzibar kuangalia fursa za kuekeza.
Dk. Shein alimueleza
Balozi huyo kuwa katika visiwa vya Zanzibar kuna vivutio kadhaa vya kitalii
ambavyo vimeweza kuwavutia watalii kutoka nchi mbali mbali duniani hivyo, ni
vyema kwa wawekezaji wa Saud Arabia kuja kuekeza Zanzibar.
Aliongeza kuwa ujio wa
watalii hapa Zanzibar umekuwa ukiongezeka kila mwaka hivyo iwapo kutajitokeza
wawekezaji ambao watawekeza katika sekta ya utalii kutoka nchini Saud Arabia,
sekta hiyo itazidi kuimarika kutokana na nchi hiyo kuwa na wawekezaji wakubwa
na wenye Kampuni kubwa za kitalii.
Aidha, Dk. Shein alimueleza
Balozi huyo mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyowekwa katika
kuhakikisha ujio wa watalii hapa Zanzibar unaongezeka ikiwa ni pamoja na
kuimarisha miundombinu ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la uwanja wa ndege wa
Kimataifa wa Abeid Amani Karume pamoja na Bandari ya Mpigaduri.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Serikali ya Saud Arabia kwa
kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za
maendeleo ikiwemo sekta ya afya, elimu, miundombinu ya barabara na nyenginezo.
Dk. Shein alisema kuwa
Serikali ya Saud Arabia imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kutoa nafasi za
masomo kwa vijana wa Zanzibar kwenda kusoma katika vyuo vya nchi hiyo hatua
ambayo imeweza kuimarisha sekta ya elimu hapa nchini.
Pia, Dk. Shein
aliipongeza nchi hiyo katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha
sekta ya miundombinu hasa ya barabara kwa kusaidia ujenzi wa barabara huko
kisiwani Pemba ikiwemo barabara ya Wete hadi Gando na Wete hadi Konde kupitia
Mfuko wa Maendeleo wa nchi hiyo (Saud Fund).
Pamoja na hayo, Dk.
Shein aliipongeza nchi hiyo kutokana na azma yake ya kusaidia ujenzi wa
barabara ya Chake hadi Wete, ukarabati wa Hospitali Kuu ya MnaziMmoja pamoja na
kukiimarisha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Dk. Shein
alimuhakikishia Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na
watu wake itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Saud Arabia
huku akisisitiza haja kwa nchi hiyo kufungua Ubalozi Mdogo hapa Zanzibar.
Nae Balozi wa Saudia Arabia nchini Tanzania, Mohammed Al
Malik alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Saud Arabia itaendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo huku
akimuahidi kuwa juhudi za makusudi atazichukua katika kuhakikisha wawekezaji wa
sekta ya utalii wanakuja kuekeza Zanzibar.
Balozi Mohammed Mansour
Al Malik alimueleza Dk. Shein kuwa ameyaona mazingira ya Zanzibar na kueleza
kuwa ni mazingira ya pekee ambayo yana kila sifa ya kuwa kivutio cha watalii
kutoka kila pembe ya duniani ikiwemo Saud Arabia.
Balozi huyo alimueleza
Dk. Shein kuwa juhudi za makusudi atazichukua katika kuhakikisha anakuwa balozi
wa kuitangaza Zanzibar kwa watu wa Saud Arabia pamoja na wawekezaji na
wafanyabiashara wa nchi hiyo. Aliongeza kuwa nchi yake ina wawekezaji wengi
ambao wamewekeza nchi kadha duniani katika sekta ya utalii, hivyo atatumia
fursa hiyo kuwashawishi kuja kuekeza na Zanzibar.
Aidha, Balozi Mohammed
Mansour Al Malik alimueleza Dk. Shein kuwa Serikali ya Saud Arabia chini ya
Mfuko wa Maendeleo wa nchi hiyo (Saud Fund), utaendelea kuiunga mkono Zanzibar
katika kuendeleza miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara, afya,
elimu pamoja na kuongeza idadi ya nafasi za masomo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment