Na. Shadrack Sagati
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema
kuwa katika uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika Novemba 26, 2017 katika
kata 43 utagharimu kiasi cha Sh bilioni 2.5.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Kailima Ramadhani,
alisema msingi wa bajeti ya uchaguzi unategemea idadi ya vituo vya kupigia kura
na idadi ya wapiga kura walioandikishwa katika kata husika. Amesema idadi ya Wapiga
Kura ndio inatoa bajeti ya mahitaji ya vifaa vya kuendeshea uchaguzi kama
karatasi za kura pamoja na idadi ya vituo ambavyo vinakuwa na watumishi wasiopungua
wanne. Kailima alitoa mfano kwamba Kata yenye vituo 41 ina bajeti kubwa kuliko Kata
yenye vituo vikubwa.
Alisema katika kituo cha kupigia kura kina watendaji
wanne ambao ni Msimamizi na Msimamizi Msaidizi, karani mwongozaji na mlinzi wa
kituo “lakini pia kuna watu wa ziada kama Wasimamizi Wasaidizi wako ngazi ya
kata na jimbo ambao wanahusika kusimamia zoezi la Uchaguzi katika maeneo
husika.
Alifafanua kuwa gharama nyingine za
uchaguzi ziko kwenye usafirishaji wa vifaa kutoka Tume kwenda kwenye
Halmashauri husika na kutoka Halmashauri kwenda kwenye kata ambako uchaguzi
unafanyika. Gharama hizo pia zanahusu
utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura kupitia machapisho mbalimbali ya Elimu ya Mpiga
Kura, Maelekezo mbalimbali kwa Watendaji wa Uchaguzi n.k.
Elimu hiyo pia hutolewa kupitia Vyombo vya
Habari pamoja na machapisho mbalimbali yatakayotumika kwa ajili ya kutoa elimu
ya mpiga kura.
“Kwenye uchaguzi huu mdogo bajeti yetu ni Sh
bilioni 2.5. Sio kwamba kila kata itatumia gharama sawa za fedha hizi, bali
kuna kata itatumia milioni 20 kutokana na idadi ya vituo vya kupigia kura kuwa
vichache na kata yenye vituo vingi kwenye uchaguzi huu itatumia Sh milioni 150,”
alisema Kailima.
Tume pia imeviasa Vyama vya Siasa
vinavyohusika kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani kutekeleza maadili ya uchaguzi ya
2015 waliyokubaliana kuyafuata na ameonya kuwa chama au mgombea atakayekika
maadili hayo atachukuliwa hatua kama ilivyoanishwa kwenye maadili hayo ya
uchaguzi.
Mkurugenzi huyo amesema Vyama vya Siasa vinatakiwa
kuhakikisha vinawaelemisha wafuasi,Wapenzi na Wananchama wao juu ya kutekeleza
maadili hayo katika kipindi chote cha kampeni. Alisisitiza kuwa iwapo wafuasi
wa vyama vya siasa watakikua maadili hayo, chama husika pamoja na mgombea wake
watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Alitaja baadhi ya vitendo vya kuvunja
maadili ya uchaguzi ni kuchana mabango ya wagombea, kutoa lugha chafu wakati wa
mikutano ya kampeni pamoja na kupitisha muda wa kufanya mikutano ya kampeni.
Alisisitiza kamati za maadili za kata na
jimbo kuchukua hatua kali kwa chama au mgombea ambaye atakikuka maadili hayo. Alisema
kamati hizo zinatakiwa kuchukua hatua ndani ya saa 48 mara chama au mgombea
anapovunja maadili.
Alizitaja baadhi ya adhabu zitazowakabili
wagombea au chama ambacho kitavunja maadili ya uchaguzi kuwa ni kuomba radhi
wananchi hadharani, kutotumia vyombo vya habari kwa muda fulani wakati wa
kampeni, onyo la maandishi, kusimamishwa kufanya kampeni, mgombea kutangaza
mbele ya vyombo vya habari kuwa yeye ni bingwa wa kukikuka maadili ya uchaguzi au
kutozwa faini Sh 100,000,
“Ni hatari kwa chama cha siasa kukiuka
maadili, hivyo navisihi vyama vya siasa kuheshimu na kuzingatia maadili hayo,”
alisema Kailima. “Pia niwaombe vyama vya
siasa vizingatie maadili kwenye mikutano yao, viende kuwaambia wananchi
watawafanyia nini katika kata zao na sio vinginevyo,”alisema Kailima.
Kailima pia alisema chama cha siasa ambacho
kinataka kufanya mabadiliko ya ratiba ya mikutano ya kampeni, lazima
kimfahamishe msimamizi wa uchaguzi wa kata na ombi hilo lazima lijadiliwe na
vyama vyote vinavyoshiriki kwenye uchaguzi.
Kuhusu vitambulisho mbadala vitakavyotumika
wakati kupigia kura kwa wale ambao wamepoteza kadi ya mpiga kura ambavyo ni vitambulisho
vya taifa, leseni ya udereva na hati ya kusafirisha; Kailima amesema
vitambulisho hivyo vitatumika tu kwa watu ambao wameandikishwa katika Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura katika kituo
husika mwaka 2015, lakini pia bado wana sifa za kupiga kura.
“Masharti ya kutumia vitambulisho hivyo
mbadala ni ya kisheria chini ya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kifungu
62 (a). Masharti yake ni lazima mtu awe bado na sifa ya kuwa mpiga kura, mfano
mtu akishahukumiwa na kufungwa kwa kosa la kukwepa kodi, au amechukua uraia wa
nchi nyingine au amewekwa kizuizini kwa mujibu wa sheria na katiba, mtu wa
namna hiyo haruhusiwi kupiga kura hata kama ana kadi ya mpiga kura au vitambulisho
hivyo vingine vitatu,”amefafanua Kailima.
Akizungumza Mikutano ya Kampeni Kailima alitoa
wito kwa vyama vya siasa kutambua kwamba Tume ya Taifa ya uchaguzi imeruhusu
mikutano ya kampeni na sio mikutano ya vyama vya siasa. Amesema mtu
anayeruhusiwa kwenye mikutano ya kampeni ni mgombea mwenyewe, chama chake au
mtu yeyote ambaye anaona anaweza kumfanyia kampeni ndani ya katiba
iliyopitishwa.
No comments:
Post a Comment