Habari za Punde

Zanzibar Yaadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani leo.

Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee , Vijana ,Wanawake na Watoto Maudline Castico Akiwa katika Picha ya pamoja na madaktari wanaotoa huduma  kwa Mtoto Njiti wakati wa maadhimisho ya watoto njiti Zanzibar.  
Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee , Vijana ,Wanawake na Watoto Maudline Castico akizungumza na wafanyakazi na wazee wa watoto njiti walioshiriki maadhimisho ya watoto Njiti katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee , Vijana ,Wanawake na Watoto Maudline Castico akizinduwa Kitabu cha huduma muhimu kwa Watoto Wachanga wakati wa Maadhimisho ya watoto Njiti yaliyofanyika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni (kushoto) Naibu Waziri wa Afya Harusi Saidi Suleiman na wapili (kulia) Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Ali Abdalla.
Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman akitoa maelezo ya  Watoto Njiti Zanzibar na juhudi zinazofanywa kupunguza tatizo hilo wakati wa maadhimisho ya watoto Njiti Duniani yaliyofanyika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Wazazi wa Watoto Njiti Halima Hassan na Hidaya Mohamed wakiwa wamebeba watoto wao wakifuatilia maadhimisho  ya watoto njiti duniani yaliyofanyika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Waziri wa Kazi,Uwezeshaji,Wazee,Vijana,Wanawake na Watoto Mh,Maudline Cyrus Castico akibeba Watoto Njiti katika Maadhimisho ya mtoto  Njiti Duniani yaliyofanyika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Na Kijakazi Abdalla - Maelezo Zanzibar.  17/11/2017.
WAZIRI wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Mh. Maudline Cyrus Castico amesema kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa kabla ya kufika wakati (watoto njiti) Zanzibar imeongezeka kutoka 206  mwaka 2016 hadi kufikia 335 kwa mwaka 2017.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya mtoto njiti Duniani huko ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni, Waziri Castico alisema kuwa idadi hiyo ni ya kutisha hivyo jamii inapaswa kufanya juhudi kupunguza tatizo hilo .

Alisema ongezeko hilo la watoto njiti limekuwa likisababisha vifo vingi vya watoto wachanga hasa ndani ya siku saba za awali baada ya kuzaliwa.

Aliipongeza Wizara ya Afya kwa  kuchukuwa juhudi kubwa za kuboresha huduma za afya kwa mama na watoto ambapo hivi sasa huduma hizo  zinapatikana kila pahala mijini na vijijini.

Alizitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na kuongeza wataalamu na vifaa muhimu za kuhudumia mama wajawazito  na wakati wa kujifunguwa pamoja na kusisitiza umuhimu wa kunyonyesha ziwa la mama pekee kwa muda wa miezi sita.

Hata hivyo alisema kuwa katika kuhakikisha huduma hizo zinaboreshwa kwa watoto njiti, Wizara imefanikiwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa wafanyakazi wanaoshughulikia watoto hao na kwa wazazi.

Alisema jumla ya wafanyakazi 300 wamepatiwa huduma za watoto njiti Unguja na Pemba ili kuhakikisha watoto hao wanakuwa katika mazingira ya afya bora.

Mapema Naibu Waziri wa Afya Harusi Said  Suleiman amesema kuwa sababu kubwa zinazopelekea kuzaliwa  watoto njiti ni pamoja na  msongo wa mawazo wakati wa ujauzito, kujifungua katika umri mdogo chini ya miaka 20 na umri mkubwa zaidi ya miaka 40.

Aliwataka kinababa kuongeza mapenzi  kwa wake zao wakati wa ujauzito na kuacha kuwatelekeza ili kumpa nafasi kujifungua akiwa salama na mtoto mwenye afya nzuri.

“Kuna baadhi ya kinababa wanapogundua  wake zao  wanaujauzito  huona ndio fursa ya kutafuta mke mwengine na kumuongezea mke mkubwa matatizo zaidi,’’ alisema Naibu Waziri wa Afya.

Alisema kizazi cha mtoto njiti ni kizazi hai ambacho kinazaliwa kabla ya kutimia umri wa kuzaliwa hivyo ni muhimu kwa wazazi wote wawili kushirikiana katika malezi kuhakikisha kinakuwa vizuri.

Nao wazazi wenye watoto  Njiti wamewashukuru wafanyakazi wa Wizara ya Afya kwa huduma wanazozipata wakati wanapofika vituoni jambo ambalo linawapa faraja ya kuendelea kuwalea watoto wao katika misingi mizuri. 

Hata hivyo wamesema wapo baadhi ya watu wanaona kuzaa mtoto akiwana hali kama hiyo  ni mitihani jambo ambalo  linawatia huzuni  sana  hivyo  wameitaka  jamii kuondokana na dhana hiyo.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO   ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.