Habari za Punde

Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Sururu Aipongeza Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja Kusogeza Huduma Ndani ya Jamii.


















Kamishna wa wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar, Johari Masoud Sururu, amewapongeza watendaji wa Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwa kusogeza huduma za Uhamiaji karibu na Jamii inayowazunguka. Alitoa pongezi hizo leo alipotembelea Vituo Maalum “Detached Points” vilivyopo ndani ya maeneo ya Kendwa na Nungwi, Shehia za Nungwi - Banda Kuu, Mnarani na Kiungani, Wilaya ya Kaskazini “A” na Fukwe za Kiwengwa, Pongwe na Pwani mchangani, Shehia za Kiwengwa, Moga na Pongwe kwa Wilaya ya Kaskazini “B” alipofanya ziara ya kikazi katika Wilayani hizo tarehe 05 – 06 Disemba, 2017.

Mkoa wa Kaskazini Unguja ni kitovu cha shughuli za Biashara na Uwekezaji katika sekta ya Utalii, hali inayosababisha kuwavuta wageni wengi kutoka Mataifa mbali mbali Duniani kutembelea maeneo hayo kwa madhumuni tofauti. “katika Mkoa huu Idara yetu ina kazi kubwa ya kuhudumia wageni wanaoingia na kuishi ndani ya Mkoa huu, kwani ni Mkoa ambao huwavuta wageni wanaokuja kutembea na kupumzika kwenye fukwe nadhifu, kuna wanaokuja kwa kuwekeza na wale wanaokuja kufanyakazi na biashara mbali mbali za 

Utalii, hali ambayo huibua  changamoto nyingi za Kiuhamiaji” alisema Kamishna Sururu.
Kutokana na muingiliano huo wa wageni wa makundi tofauti, Idara ya Uhamiaji yenye dhamana ya kuhakikisha wageni wote wanaoingia na kuishi nchini wanafanya hivyo kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Uhamiaji, ina mchango mkubwa katika kuimarisha Ulinzi, Uchumi na Utamaduni wa watu wa Zanzibar. Kuanzishwa kwa Vituo maalum kwenye maeneo hayo ni mapinduzi makubwa katika Udhibiti na Usimamizi wa wageni wanaoingia na kuishi Zanzibar kinyume cha Sheria.

“Kwa kweli Nimefarijika sana kuona jinsi mlivyojipanga kuweza kuyafikia maeneo yote yenye changamoto za uwepo wa baadhi ya wageni wanaojipenyeza na kuishi nchini bila ya Kufuata Sheria za Uhamiaji. Uwepo wa Vituo hivi naamini ni muarobaini wa kuondoa kabisa tatizo la Uhamiaji haramu” Alisema Kamishna Sururu na kuongeza

“Hatuzuwii wageni kuja kutembea, hatuzuwii wageni kufanyakazi ama kuwekeza nchini kwetu bali tunataka wageni wote waingie na kuishi nchini kwa kuheshimu Sheria za Nchi yetu, kwa kufanya hivyo tutaweza kufikia ile adhma njema ya serikali kufungua milango ya Biashara na Uwekezaji katika sekta ya Utalii kwa manufaa makubwa bila ya kuathiri Jamii na Tamaduni zetu”.

Aidha, Kamishna Sururu aliwahakikishia Masheha wa maeneo hayo kuwa Idara ya Uhamiaji itaendelea kushirikiana nao kwa vitendo hususan katika kupiga vita Uhalifu wa aina zote ukiwemo Udhalilishaji, Uuzaji na Usafirishaji wa Madawa ya Kulevya unaofanywa na baadhi ya wageni hapa Zanzibar.

Kufuatia kauli hiyo, Sheha wa Shehia ya Nungwi - Banda Kuu, Bw. Mohamed Khamis Haji alisema “Nashukuru sana kwa ujio wako na hasa msimamo ulioutoa juu ya kuwachukulia hatua stahiki wageni wanaojihusisha na vitendo vya Uhalifu hapa Nungwi. Hichi ni kilio chetu cha siku nyingi. Nasi tunaahidi tutaendelea kutoa ushirikiano unaostahiki kwa Askari wa Uhamiaji ili Shehia zetu ziendelee kupokea wageni wenye manufaa kwa Jamii zetu na si vinginevyo”.

Kwa upande wake, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji, Muhsin A. Abdullah alifafanua, lengo kubwa la kuanzisha kwa vituo hivyo maalum vilivyopo maeneo ya Nungwi na Kiwengwa Wilaya ya Kaskazini “A” na“B” ni mkakati mmojawapo katika kuimarisha Doria na Misako ili kuwabaini wahamiaji wasiofata sheria.

“Mkoa huu tumekuwa tukilalamikiwa sana kwamba wageni wengi huzagaa na kufanyakazi kiholela hususan kutoka Mataifa ya Afrika Mashariki, kumepelekea tusogee karibu tuweze kushirikiana na watendaji wenzetu wakiwemo Masheha na Wananchi, hatua ambayo imeanza kuzaa matunda. Tumeongeza wigo wa kuelimishana, kujenga mashirikiano na kupeana taarifa mbali mbali ambazo husaidia sana utekelezaji wa majukumu yetu” alisema Mrakibu Mwandamizi Muhsin.

Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Kiwengwa Bw. Maulid Masoud Ame katika ziara hiyo aliapata fursa ya kuchangia ambapo alisema “Idara ya Uhamiaji inatusaidia sana katika suala zima la kuwatambua nani Raia wa Tanzania na nani mgeni. Maana katika maeneo yetu tuna changamoto kubwa sana ya kuwepo kwa vitendo vya ukiukwaji wa maadili na udhalilishaji vinavyofanywa na watu mbali mbali wakiwemo wageni. Hivyo kwa ushirikiano mkubwa tunaopata kutoka kwa Askari wa Uhamiaji unatusaidia sana kufikia maamuzi. 

Tumekuwa tukipokea malalamiko hayo kwa mfano yakihusisha jamii za Kimasai wanaofanyakazi katika mahoteli mbalimbali hapa Kiwengwa, ambao baadhi yao ni wamasai kutoka Kenya, ambapo sisi tunaona hao wote ni Watanzania wenzetu. Askari wa Uhamiaji kwa utaalamu na weledi walionao hutusaidia katika kuwatambua” alisisitiza Sheha Ame.

Akihitimisha ziara yake kwenye Wilaya mbili hizo, Kamishna Sururu, alitembelea Bandari ya Mkokotoni kujionea changamoto mbali mbali zikiwemo, vipenyo vinavyotumiwa na wahamiaji wasiotaka kufuata Sheria na uwepo wa baadhi ya Manahodha wa vyombo vya usafiri wanaotumia Bandari hiyo, kutoshusha Abiria kwenye eneo lililotengwa.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwasisitiza Askari wa Uhamiaji Wilayani humo, kusimamia vyema majukumu yao kwa mujibu ya Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. “Nawasihi na kuwataka muelewe kuwa sisi tumepewa dhamana na Serikali kuwatumikia wananchi, hivyo nidhamu na heshima ya kazi ndio msingi wa mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yetu”.  Alimalizia Kamishna Sururu.

Imetolewa na:

KITENGO CHA UHUSIANO, AFISI KUU YA UHAMIAJI ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.