Habari za Punde

Mkutano wa nane wa Baraza la tisa la Wawakilishi Zanzibar kuanza Jumatano Tarehe 6 mwezi huu

Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Raya Issa Msellem akizungumza na Waandishi wa habari katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani kuhusu kukamilika kwa maandalizi ya Mkutano wa Nane wa Baraza la Tisa la Wawakilishi linaloanza Tarehe 6/12/2017.

Na Maryam Kidiko  - Maelezo Zanzibar.

Jumla ya maswali 113 yameratibiwa kwa ajili ya kujibiwa na miswada minne ya sheria itawasilishwa kwa mara ya pili katika  mkutano  wa nane wa Baraza la Tisa la Wawakilishi unaotarajiwa kuanza Jumatano tarehe 6 mwezi huu.

Hayo aliyasema Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Raya Issa Msellem katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani wakati akizungumza na Waandishi wa habari.

Alisema kuwa miswada ya sheria iliyowasilishwa na kusomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Septemba - Oktoba mwaka huu itasomwa tena  kwa na kujadiliwa katika mkutano wa  huo.

Katibu wa Baraza aliitaja miswada hiyo kuwa  ni Mswada ya sheria ya kuanzisha Wakala wa usajili wa matukio ya Kijamii Zanzibar na Mswada wa sheria ya kuanzisha wakala wa maendeleo ya viwanda vidogo vidogo, na vya kati pamoja na kuwezesha ushajihishaji na uendelezaji wa viwanda hivyo na mambo mengine yanayohusu na hayo.

Miswada mengine ni mswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbali mbali na kuweka masharti bora ndani yake na Mswada wa sheria ya kufuta sheria ya uchaguzi nama 11 ya mwaka 1984 na kutunga sheria nyengine ya mwaka 2017 pamoja na masuala mengine yanayohusiana nayo.

Vile vile alisema kuwa katika mkutano huo pia kutakuwa na ripoti ya utekelezaji wa kazi za Tume ya maadili ya viongozi wa umma pamoja na kuwasilishwa hoja binafsi ya mjumbe kuhusu kuweka miundo mbinu bora kwa watu wenye ulemavu katika majengo, Barabara, Makaazi, Maeneo ya kupumzikia na maeneo mengine.

Aidha Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar alisema kutakuwa na maombi ya Wananchi wa Kisakasaka Zanzibar kuhusu namna wanavyoweza kufaidika kutokana na machinjiyo ya Wanyama yaliyopo katika maeneo yao.
                                                                

                          IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.