Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein, Amesisitiza Haja ya Kuithamini, Kuiendeleza Lugha ya Kiswahili.

RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja ya kuithamini, kuiendeleza, kuipenda na kuitumia lugha ya kiswahili na kuizungumza bila ya kuichanganya na lugha ya kiengereza.

Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Baraza la zamani la Wawakilishi, Kikwajuni mjini Unguja katika ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili lililowashirikisha wataalamu wa kiswahili kutoka sehemu mbali mbali duniani.

Katika hotuba hiyo, Dk. Shein alieleza haja ya kuitunza lugha hiyo na kuendeleza na pale panapokuwepo wageni basi waandaliwe mazingira ya kuweza kupata machapisho ya lugha zao lakini lugha ya kiswahi ndiyo itumike huku akieleza kuwa tangu miaka ya awali ya iliyokuwa Tanganyika sasa Tanzania Bara na Zanzibar baada ya kujikomboa, Serikali zote mbili zilitambua umuhimu wa kukienzi na kukitunza Kiswahili.

“Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume alituasa kwa kusema ‘Tukuza kilicho chako, mpaka usahau cha mwenzako’ kwa hivyo tuna wajibu mkubwa wa kuitunza lugha yetu ya Kiswahili”,alisema Dk. Shein.

Alisema kuwa upande wa Tanzania Bara, Hayati Mwalimu Nyerere wakati akihutubia Bunge mwaka 1962, alitumia lugha ya Kiswahili kabla ya lugha hiyo haijatangazwa kuwa lugha rasmi na lugha ya Taifa mwaka 1967 ambapo pia, katika mwaka huo, lilianzishwa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA.

Kwa upande wa Zanzibar, Dk. Shein alieleza kuwa muasisi wa Mapinduzi Matukufu na Rais wa Zanzibar , Marehemu Mzee Abeid Amani Karume katika mwezi wa Machi, 1964 alitangaza kuwa lugha ya Kiswahili ndio lugha rasmi na lugha ya Taifa. Kufuatia hatua hizo za kutoa matamko ya kisera, Dk. Shein anaeleza kuwa Serikali zote mbili zilianza kuunda taasisi za kukikuza na kukiendeleza Kiswahili.

Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza jinsi waaandishi mashuhuri walivyochangia kukiendeleza Kiswahili ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar, Dk. Mohammed Seif Khatib pamoja na mabingwa wengine bila ya Marehemu Siti bint Saad ambaye alichagia kutokana na tungo zake.

Aliongeza kuwa hivi sasa Kiswahili ni lugha inayotumiwa na watu takriban milioni mia moja na hamsini duniani  ambayo ni lugha ya Kiafrika inayoongoza kwa kuwa na watumiaji wengi pamoja na kuwepo zaidi ya vyuo vikuu mia moja duniani vinavyofundisha lugha hiyo na vituo vya redio zaidi ya idadi kama hiyo.

Dk. Shein alieleza kuwa mwitikio mkubwa wa washiriki wa kongamano hilo la Kiswahili la Kimataifa hapa Zanzibar ni kielelezo cha watu kuelewa umhimu wa Kiswahili na ni ishara nzuri ya kuimarika na kukubalika kwake.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza makosa ya kadhaa ya matumizi ya maneno mbali mbali katika Kiswahili yanayofanywa na watu kwa kujua au kutokujua na usahihi unaotakiwa kwa mujibu wa lugha ya Kiswahili fasaha.

Hivyo, kupitia hadhara hiyo, Dk. Shein alitoa rai kwamba kubainisha makosa ya matumizi yasiyo sahihi katika lugha kusisubiri wakati wa makongamano na kuitaka BAKIZA, BAKITA pamoja na wataalamu wote wa lugha hiyo kutekeleza jukumu lao.

Alieleza kuwa Kiswahili kina utajiri mkubwa wa msamiati la lahaja, hivyo, si lazima watu watohoe maneno kutoka lugha nyengine na yatumiwe kwenye Kiswahili rasmi.“Kwanza mzingatie lahaja za lugha ya Kiswahili na baadae lugha za Kibantu, si kila mtu aje na maneno yake katika mnasaba huu”,alisema Dk. Shein.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kufikiria kuanzisha kituo maalum ambapo kazi mbali mbali za waandishi wa Kiswahili wa ndani na nje ya Zanzibar na Tanzania zitawekwa pamoja na picha za wataalamu wao huku akilishauri BAKIZA kwa kushirikiana na SUZA kuimarisha vipindi vya lugha ya Kiswhahili kupitia redio na televisheni ili kuongeza ubora wake.

Mapema akitoa salamu za vyama vya Kiswahili duniani, Dk. Mahiri Mwita alieleza jinsi lugha ya Kiswahili inavyozidi kuimarika kutokana na mashirikiano ya vyama hivyo ambapo Profesa Alwiya Omar Saleh anaefundisha lugha ya Kiswahili katika chuo kikuu cha Indiana Marekani alieleza jinsi ya lugha hiyo inavyozidin kukua duniani.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika ufunguzi wa Kongamano hilo la siku mbili akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.