Habari za Punde

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Aifagilia Kampuni ya Premium Agro Chem Ltd Kwa Kazi Nzuri ya Kusambaza Mbolea.

Na Dotto Mwaibale
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Chritina Mndeme, ameipongeza kampuni ya Premium Agro Chem Limited, kutokana na kazi nzuri iliyofanya ya kuharakisha upatikanaji wa mbolea za kupandia aina ya Urea kwa wakulima wa mkoa wake na wilaya zake kwa ujumla.
Mkuu huyo wa mkoa alisema mazingira ya mkoa huo na mahitaji yaliwafanya viongozi kuwa katika changamoto kubwa, lakini kampuni hiyo imefanyakazi kubwa ya kuwafikishia wakulima hao mbolea.  
Alisema mahitaji ya mkoa wake kwa sasa ni zaidi ya tani 52,700, lakini wamepokea kiasi cha tani 15,200, na kutaka juhudi zaidi zifanyike kwani mbolea ya kupandia inahitajika kwa wakulima hao kabla ya Januari 15 mwaka huu.

"Ninawashukuru sana wadau wa mbolea na kilimo kwenye mkoa wetu, lakini kipekee naomba niwashukuru sana Kampuni ya Premium Agro Chem Ltd, kutokana na kazi nnzuri ya kutusambazia kupitia mawakala wao na hata matawi yao hapa Songea na Mbinga, ninawashukuru na kuwapongeza sana kwa kazi nzuri, wameonyesha uzalendo mkubwa," alisema RC Mndeme.

Mkuu huyo wa mkoa aliwaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri ndani ya mkoa wake, kufuatilia suala la upatikanaji wa mbolea kwa wakulima kwenye maeneo yao na kazi hiyo inatakiwa kufanyika masaa 24 bila kuchoka.

Kwa upande wake Meneja Biashara na Masoko wa kampuni hiyo ya Premium Agro Chem Ltd, Brijesh Barot, alisema kwamba wamesambaza zaidi ya tani 8,200 kwa mkoa wa Ruvuma na bado wanaendelea kusambaza kupitia kwa mawakala wengi zaidi.

"Tunaendelea kusambaza mbolea kwa mikoa yote, Njombe, Ruvuma, Mbeya, Iringa, Rukwa, Songwe na Katavi, kupitia kwa mawakala pamoja na kuwatumia maafisa wetu walio katika vituo vya matawi yetu huko kwa ajili ya kuharakisha upatikanaji wa mbolea kwa wakulima vijijini," alisema Barot.

Alisema kampuni yao inafanyakazi kazi hizo kizalendo na ndio maana wamekubali kuuza kwa bei elekezi mbolea ambayo wao walikuwa wameinunua muda mrefu kabla ya kutolewa kwa maagizo ya kununua kwa mfumo maalum wa serikali, na hili linafanywa kwa kumuunga mkono Rais Dkt Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.