Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Sheina, akizungumza wakati wa ziara yake alipotembelea Jengo la ZBC Redio Rahaleo Zanzibar kuangalia ujenzi wa Studio. za kutangazia. kushoto Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee, Waziri wa Habari Utalii Utamaduni na Michezo Mhe Rashid Ali Juma na kulia Mkurugenzi Mkuu wa Shrika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Aiman Duwe.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein leo amezitembelea studio za ZBC Redio zilizopo Rahaleo na
kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha studio hizo
pamoja na jengo lake vyote vinaimarishwa kama ilivyofanywa kwa ZBC Televisheni.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo katika ziara yake aliyoifanya ya kuzitembelea studio za ZBC Redio
zilizopo Rahaleo mjini Zanzibar huku akisisitiza azma ya Serikali ya
kuhakikisha studio zote za ZBC zinakuwa za kisasa na zinakwenda na wakati
uliopo.
Katika ziara yake
hiyo, viongozi wa mbali mbali walishiriki akiwemo Waziri wa Habari, Utalii,
Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma ambaye kwa upande wake alieleza kufarajika
kwake na ziara hiyo ya Dk. Shein pamoja na kueleza hatua za ukarabati
zilizofikiwa ambapo pia, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mahmoud pamoja
na Mshauri wa Waziri wa Wizara hiyo Abdalla Mwinyi Khamis na Katibu Mkuu Omar
Hassan walishiriki.
Rais Dk. Shein
alizitembelea studio zote nne za ZBC Redio zikiwemo zile zilizofanyiwa
ukarabati mkubwa pamoja na zile zinazohitajia ukarabati huku akipata fursa ya
kukitembelea chumba cha habari na kupata maelezo kutoka kwa uongozi wa ZBC
Redio na muhariri Mkuu wa chumba cha Habari Bi Lulu Mzee pamoja na kuzitembelea
sehemu nyengine muhimu za ZBC Redio.
Katika ziara yake hiyo
Dk. Shein alizitembelea studio nne
pamoja na studio kubwa na ile ya VIP ambazo hizo bado hazijafanyiwa matengenezo
na kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa ZBC Aiman Duwe pamoja na Mkuu
wa Utangazaji Suzan Kunambi ambao
walieleza hatua kubwa iliyofikiwa katika ukarabati huo mkubwa.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alieleza hatua za haraka ambazo zitachukuliwa na Serikali katika kuhakikisha changamoto ya
usafiri inapatiwa ufumbuzi ili shughuli zote za uendeshaji katika kituo hicho na
upatikanaji habari unafanyika kwa ufanisi mzuri zaidi.
Dk. Shein alisisitiza
agizo lake la kuwepo kwa watangazaji maalum kwa kutangazia mambo maalum
zikiwemo taarifa maalum za Serikali, za kiuchumi, kijamii, za kisiasa pamoja na
matukio muhimu ya nchi kama ilivyokwa vyombo vya habari ya Kimataifa kama vile
BBC.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alieleza haja ya kuwa na taarifa za habari ambazo zinafanana kati ya ZBC
Redio na ZBC Televisheni hasa kwa kuzingatia kuwa Shirika hilo ni moja na
watendaji wake ni wale wale hatua ambayo itapendeza na itatoa habari vyema kwa
wananchi.
Nao uongozi wa ZBC
ulitoa pongezi na shukurani zake kwa Rais Dk. Shein kwa ziara yake hiyo ya
kuwatembelea na kuona hatua waliyofikia katika baadhi ya matengenezo
yaliyofanywa kwenye studio hizo za ZBC
Redio.
Pamoja na hayo uongozi
huo wa ZBC Redio ulieleza changamoto waliyonayo ya usafiri katika kufanya
shughuli zao za kila siku huku fundi mitambo wa ZBC Redio Lazaro Joseph
akieleza haja ya kuwepo mashine za kisasa za kuhifadhia kumbukumbu za vipindi
mbali mbali studioni hapo “Saver”.
Aidha, fundi huyo
mitambo alieleza hatua zilizoanza kuchukuliwa hivi sasa katika kuviweka vipindi
mbali mbali vya redio, hotuba pamoja na nyimbo kwenye mashine za kuhifadhia
kumbukumbu “ Saver” ili ziweze kudumu kwa muda mrefu pamoja na kuwa salama.
Katika maelezo yao
walieleza kufarajika na hali iliyopo hivi sasa katika studio hizo
ikilinganishwa na hapo kabla wakati Rais Dk. Shein alipozitembelea studio hizo
mnamo tarehe 19 mwezi Septemba mwaka 2016 ambapo hazikuwa katika hali ya
kuridhisha.
Uongozi huo pia,
ulieleza kuwa tayari agizo la Rais Dk. Shein la kuwepo kwa watangazaji maalum wa
kutangaza habari maalum wamelifanyia kazi ambapo kwa upande wa ZBC Redio ni
Fatma Said Ali na Salum Othman ambapo kwa upande wa ZBC Televisheni ni
Mwanajuma Kassim na Ussi Mussa.
Aidha, uongozi huo
ulieleza kuwa tayari wameshaanzisha utaratibu wa kubadilishana kwa watangazaji,
waandishi na watendaji wengine kati ya ZBC Redio na ZBC Televisheni ili waweze
kufanya kazi kwa mashirikiano na ukaribu zaidi katika kuiendesha taasisi hiyo
ambayo imeamua kufanya mabadiliko makubwa.
Kwa upande wa
“Transmitter”, tayari nne zimeshanunuliwa na zimeshafungwa na zikiwa tayari
zinatumika ambapo ushahidi wa hayo yote ni kutokana na hivi sasa Mikoa yote ya
Zanzibar na Pwani ya Afrika Mashariki pamoja na ulimwenguni kote wanapata
matangazo ya ZBC Redio kwa uhakika kupitia 90.5,97.7,94.7.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment