Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Afanya Ziara ya Kutembelea Eneo la Ujenzi wa Matenki ya Kuhifadhia Mafuta Mangapwani Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shei, akimsikiliza Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi Zanzibar Ahmeid Rashid, akitowa maelezo ya eneo linalotarajiwa kujengwa Matenki ya Kuhifadhia Mafuta na Gesi Asilia katika eneo la Mangapwani Wilaya ya Kaskazini B Unguja alipotembelea eneo hilo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amefanya ziara ya kutembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya Mradi wa kuhifadhi mafuta na gesi asilia pamoja na ujenzi wa bandari kwa ajili ya kusafirishia na kuingiza rasilimali hizo.

Akiwa katika eneo hilo  lililoko Mangapwani-Bumbwini lenye ukubwa wa hekta 399.25 sawa na hekari 986.5, Rais Dk. Shein aliyeongozana na viongozi mbali mbali wa Serikali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, Mawaziri na viongozi wengine wa Serikali, wakiwemo wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, alipata maelezo kuhusu hatua zinazoendelea katika mradi huo.

Kwa maelezo ya Katibu wa Kamisheni ya Ardhi Ahmed Abdulrahman Rashid alimueleza Dk. Shein kuwa eneo hilo lenye ukubwa wa hekta hizo tayari limetengwa kwa ajili ya shughuli zote za mafuta na gesi asilia, bandari pamoja na bohari kuu ya Serikali ya kuhifadhia mafuta.

Aidha, alimueleza Rais Dk. Shein kuwa azma ya mradi huo ni kwamba baada ya kukamilika shughuli zote za mafuta zinazofanywa katika bohari ya Mtoni zitahamishwa na kuhamia katika eneo hilo maalum lililolengwa na Serikali.

Kwa mujibu wa maelezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Ali Halil Mirza, hatua inayoendelea hivi sasa ni kufanywa kwa uchambuzi yakinifu unaotekelezwa  na Benki ya Dunia  ambao utakamilika kwa muda wa miezi sita ijayo.

Mirza alieleza kuwa kukamilika kwa uchambuzi huo yakinifu ndio utaleta mapendekezo ya kulisanifu eneo hilo kwa ajili ya bandari na majengo mengine ya utawala na shughuli nyengine zinazoenda sambamba na mradi huo.

Kwa mujibu wa maelezo ya viongozi wa Wizara hiyo, miongoni mwa sababu ya kutengwa eneo hilo kwa shughuli hizo ni kutokana na kuwa na kina kirefu cha maji ya bahari ambacho kitarahisisha kujengwa kwa bandari hiyo muhimu ambayo itatumika kwa ajili ya kusafirishia gesi asilia na mafuta ndani na nje ya nchi.

Uongozi wa Wizara hiyo, ulieleza kuwa miongoni mwa faida kubwa za mradi huo mara baada ya kukamilika kwake ni pamoja na kuondoa kabisa uhaba wa mafuta hapa nchini sambamba na kuweza kuuza hata nje ya nchi na kuipatia Serikali pato kubwa.

Sambamba na hayo, uongozi huo wa Wizara hiyo ulieleza kuwa Mradi huo ambao utakuwa na bandari, matangi ya mafuta kwa kuwa na sehemu ya bohari ya Taifa ya kuhifadhia gesi asilia na mafuta ni hatua za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha sekta ya nishati hapa nchini.

Wakati huo huo, Dk. Shein akiwa na ujumbe wake alipata fursa ya  kulikagua eneo la Kampuni ya Salama International Trading  Co Ltd, linalojengwa maalum kwa ajili ya kusafisha mafuta na kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Abdallah Said Abdallah na kumueleza hatua zilizofikiwa na Kampuni yake katika ujenzi huo.

Kwa maelezo ya Mkurugenzi huyo, alisema kuwa eneo hilo ambalo ni kwa ajili ya kusafisha mafuta ambalo limefikia asilimia 65 za ujenzi, lina lengo la kujenga jeti kwa ajili ya kushushia mafuta na kutia kwenye matangi yaliopo katika eneo hilo.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa Matenki tani elfu 18, sawa na lita milioni 24 ambayo yanaweza kuhifadhiwa  kwa wakati mmoja, huku akieleza aina za mafuta yatakayohifadhiwa katika matenki hayo yakiwemo mafuta ya diseli, petroli na mafuta ya taa pamoja na mafuta ya kulainisha mitambo huku.

Uongozi huo ulieleza kuwa tayari wanabaraka zote kutoka Serikalini ikiwemo kutoka kwa Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), na kutoa shukurani kwa Serikali kupitia Idara zake zote ikiwemo Mazingira, Ardhi pamoja na (ZIPA) na kutoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa ziara yake hiyo.

Walieleza kuwa kuanzia Februari mwaka huu wataendelea na shughuli za ujenzi zilizobaki shughuli ambazo ziliaza mwaka 2015 kwa awamu tatu ambapo hadi walipofikia washatumia dola milioni 5 kwa awamu ya kwanza na kueleza kuwa watazalisha tani 600 ambazo zitawasidia Wazanzibari wenyewe kwa asilimia 70 na asiliamia zilizobaki watauza nje ya nchi.

Walieleza kuwa Watu wa Bandari, Uhamiaji na Idara zote muhimu zitakuwepo katika eneo hilo ambalo tayari wameshaanza ujenzi wa jengo maalum kwa wahusika hao.

Akiwa katika eneo hilo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya uhifadhi wa mazingira katika mchakato wa usafishaji wa mafuta mara utakapokamilika mradi huo ambapo Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alimtoa wasi wasi na kumueleza kuwa aina ya mafuta wanayokusudia kusafisha haitakuwa na athari zitakazopelekea uharibifu wa mazingira kutokana na aina hiyo ya mafuta ambayo watachukua kutoa nchini Oman na Iran.

Pia, Dk. Shein alitembelea eneo la Kampuni ya Turkey Petrolium (TP), ambalo limetengwa kwa ajili ya gesi na mafuta ambapo uongozi wa Kampuni hiyo chini ya kiongozi wake Taufiq Salim Turkey ulieleza kuwa juhudi za makusudi wanazichukuwa katika kuhakikisha Zanzibar inafaidika kwa gesi mara baada ya kujengwa kwa Chelezo ambapo meli maalum zitaleta gesi moja kwa moja kuanzia mwezi wa sita hapa Zanzibar.

Aidha, uongozi huo ulieleza azma ya kujenga jengo maalum ambalo litasaidia kwa ajili ya kuwaweka wafanyakazi wa Kampuni yao pamoja na Idara nyengine muhimu zinazohusiana na shughuli hizo zikiwemo Uhamiaji na nyenginezo.

Pamoja na hayo, uongozi huo uliiomba Serikali kuwezesha azma yao hiyo kutokana na baadhi ya changamoto zilizopo hivi sasa ikiwemo uhaba wa gesi mara kwa mara kutokana na sehemu wanayochukulia gesi hiyo.

Uongozi wa Kampuni hiyo ya Turkey Petrolium (TP), ulieleza kuwa mashirikiano mazuri yamekuwepo kati yao na Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Wizara ya Biashara.

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa wanunuzi wakuu wa gesi katika Kampuni yao hiyo kwa hivi sasa ni wananchi pamoja na hoteli huku uongozi huo ukisisitiza kuwa kuwepo kwa chelezo kwa ajili ya kuingizia meli ambazo zitaleta gesi moja kwa moja kutawarahisishia zaidi uendeshaji wa mradi wao huo.

Nae Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Haji Kali Haji alieleza mashirikiano yaliopo kati ya Mamlaka yake pamoja na Kampuni hiyo ambapo mapema alieleza mashirikiano na hatua zinazochukuliwa katika kuhakikisha eneo maalum lilotengwa na Serikali kwa ajili ya shughuli za mafuta na gesi asilia linafikia na malengo yaliokusudiwa na Serikali.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.