Habari za Punde

Balozi Seif akutana na Kamishna Mpya wa Polisi Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kulia akizungumza na Kamishna Mpya wa Polisi Zanzibar Mohamed Haji Hassan alipofika Ofisini kwake Vuga kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Na Othman Khamis , OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kulipa ushirikiano wa kina Jeshi la Polisi Nchini katika kuona Amani ya Taifa  pamona na Raia wake inaendelea kudumu muda wote.
Alisema Zanzibar ina changamoto nyingi zikiwemo za Kisiasa, Dawa za Kulevya na ukosefu wa Maadili unaopelekea kuibuka kwa kasi zaidi ya Udhalilishaji  wa Kijinsia ambazo zinahitaji kushughulikiwa ipasavyo ili kuleta ustawi na Utulivu.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Kamishna Mpya wa Polisi Zanzibar Mohamed Haji Hassan aliyefika kujitambulisha Rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli hivi karibuni.
Balozi Seif alisema masuala ya udhalilishaji pamoja na Dawa za kulevya hivi sasa yamekithiri na kuleta sura mbaya ndani ya Jamii kiasi cha kulazimika kutungwa sheria ili kujaribu kupambana na kadhia hiyo inayotoa picha mbaya katika uso wa Dunia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliviagiza vyombo vya Dola kuwasaka na baadae kuwashughulikia ipasavyo wale wote wanaohusika na uingizaji wa Dawa za Kulevya Nchini kwa vile wao ndio chanzo cha balaa zote zinazotokea katika Mitaa mbali mbali Nchini.
Hata hivyo Balozi Seif alikemea tabia ya baadhi ya Maofisa wa Vyombo vya Dola kujaribu kufifilisha kesi za Dawa za kulevya kwa kuwapa afuweni Watuhumiwa huku wakizingatia zaidi kupokea Rushwa badala ya kuwaonea huruma wale wanaoathirika kutokana na wimbi la Dawa hizo.
Alifahamisha kwamba tabia hii hupelekea mwenye hatia kuachwa huru  na hatimae kuonekana kudunda Mitaani kifua mbele huku akianza majisifu na kutia hofu Wananchi wanaomuelewa madhambi yake.
Akigusia suala la Kisiasa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Kamishna Mpya huyo wa Polisi Zanzibar kwamba ni vyema vyombo vya Dola kwa kushirikiana na Wananchi wema wakaelewa kwamba vurugu na Fujo si jambo la kupewa nafasi.
Balozi Seif alisema Zanzibar licha ya kipindi cha Kampeni za Uchaguzi  inahitaji kuendelea kubakia kuwa ya amani muda wote ili Raia wake wafanye shughuli zao za kujitafutia riziki bila ya vikwazo vyovyote.
Alimpongeza Kamishna wa Polisi wa Zanzibar kwa wadhifa aliopewa na Taifa ambao anastahiki kuusimamia katika misingi ya Maadili na nidhamu ili lengo la kupewa nafasi hiyo likamilike ipasavyo.
Mapema Kamishna wa Polisi Zanzibar  Mohamed  Haji Hassan alisema suala la Amani ndio kazi kubwa na ya msingi atakayohakikisha anaisimamia kwa nguvu zake zote kwa kushirikiana na Viongozi na askari wenzake ili kutoa fursa kwa Wananchi waendeshe maisha yao kama kawaida.
Kamishna Mohamed alisema changamoto zilizopo pamoja na udhaifu wa baadhi ya Maafisa na Askari wa Jeshi hilo unaweza kuondoka au kupungua kwa kiasi kikubwa kama nguvu za ushirikiano zitapewa nafasi pana zaidi kwa pande zote husika.
Aliiomba Serikali licha ya uchumi duni lakini bado upo umuhimu wa kufikiria kununua mashine za kisasa za uchunguzi wa Dawa za Kuelevya hasa katika maeneo ya Uwanja wa Ndege na Bandarini.
Kamishna Mohamed alisisitiza kwamba katika jitihada za kukabiliana na wimbi la uingizaji, uuzaji na utumiaji wa Dawa za kulevya ipo haja ya Wananchi kuendelea kulipa ushirikiano wa karibu zaidi Jeshi la Polisi katika mbinu za kuvurugu soko la uuzaji wa Bidhaa hiyo haramu.
Hata hivyo Kamishna Mohamed Haji Hassan alieleza kwamba Viongozi wa Dini bado wana nafasi ya kuwaelimisha Waumini wao hasa Vijana kujiepusha na wimbi hilo la Dawa za Kulevya kwa kutumia  Kongamano, semina pamoja na Hotuba.
Alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba makosa mengi yanatokea na kuripotiwa lakini ikichunguza kwa undani inatokana na Watu kukosa Doria za Kiimani

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.