Habari za Punde

Hutuba ya Makamu wa Pili Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kuahirisha Mkutano wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo.


HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI WAKATI WA KUTOA HOJA YA KUAKHIRISHA MKUTANO WA TISA WA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI, TAREHE 28 FEBUARI, 2018

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, mwingi wa rehma, mwenye kuneemesha neema zote hapa ulimwenguni na kesho Akhera, kwa kutujaalia hali ya uzima na afya njema ambayo imetuwezesha kuwepo hapa wakati huu baada ya kufanikisha vizuri Mkutano wa Tisa wa Baraza hili Tukufu la Tisa la Wawakilishi ulioanza tarehe 07 Febuari, 2018.  Shughuli zote zilizopangwa katika ratiba ya Mkutano huu zimekamilika kwa wakati na kwa ufanisi wa kupigiwa mfano.

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kukupongeza wewe mwenyewe binafsi Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Naibu Spika Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma pamoja na Wenyeviti wote wa Baraza kwa kuviendesha vyema vikao vyetu kwa hekima, busara na weledi mkubwa na kukifanya kikao hiki kumalizika kwa mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu na uzito wa kipekee nampongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, kwa kuisimamia vyema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Chama chetu cha Mapinduzi (CCM). Usimamizi wake huo umetuletea mafanikio ya kupigiwa mfano ambayo tunajivunia na kutufanya twende kifua mbele.

Mheshimiwa Spika, nampongeza tena Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kukamilisha ziara yake ya nchi ya Falme za Kiarabu. Safari ambayo italeta manufaa makubwa ya kuinua uchumi wa nchi yetu ikiwemo masuala ya utafiti na uchimbaji wa mafuta, Sekta ya Utalii, Sekta ya Biashara, Sekta ya Afya, ushirikiano wa kidiplomasia, uanzishaji wa viwanda vidogo vidogo pamoja na ujenzi wa barabara.  Lakini pia, ziara hiyo imeimarisha uhusiano wetu mzuri uliopo baina ya Zanzibar na UAE.  Mapokezi aliyoyapata yana dhihirisha kuimarika huko kwa uhusiano wetu huo.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha na kuhamasisha michezo nchini, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein ametimiza ahadi yake aliyoitoa kwa wanamichezo wetu na kuwapa zawadi mbali mbali wanamichezo wetu wa timu ya Taifa ya Zanzibar Heroes na Sand Beach Heroes kwa kila mchezaji na viongozi wa timu hizo kwa juhudi na moyo waliouonyesha kwa kuipatia sifa nchi yetu na kufungua ukurasa mpya katika tasnia ya michezo katika ramani ya dunia.

Mheshimiwa Spika, vile vile, napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kumteua Ndg. Mohammed Hassan Haji kuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar. Uteuzi huo unaonesha imani ya Mheshimiwa Rais aliyonayo kwa utendaji wake wa kazi. Ninaamini kwamba Kamishna Haji ataendelea kuliimarisha Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa majukumu ya ulinzi wa raia na mali zao hapa Zanzibar kwa uadilifu na umakini mkubwa pamoja na kuitunza amani ya nchi yetu. 

Mheshimiwa Spika, kadhalika tunakipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kutimiza miaka 41 tokea kuzaliwa kwake mwaka 1977 kwa mafanikio makubwa sana. Chama hichi kimeweza kuisimamia amani, umoja, utulivu na mshikamano katika nchi yetu na kuendelea kutoa maelekezo na miongozo kwa viongozi na watendaji mbali mbali wa Serikali na kuleta ufanisi katika utendaji wetu wa kazi za kuwatumikia wananchi wetu. Tunaamini kwamba, miongozo na maelekezo hayo yanasaidia sana katika kuongeza uweledi na uwajibikaji unaotoa mchango mkubwa wenye kuleta maendeleo endelevu nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekamilisha na kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wake wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 kwa muda wa miaka miwili kuanzia mwezi Oktoba, 2015 hadi Septemba, 2017 na kuwasilishwa katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika mwezi Disemba, 2017 Mkoani Dodoma. Taarifa hiyo imeonesha utekelezaji halisi wa maagizo ya Ilani yetu na tayari karibu asilimia 60 ya maagizo hayo yamekamilika utekelezaji wake. Nazisihi Taasisi zote za Serikali kuendelea na utekelezaji wa maagizo yaliyobakia kwa kufuata taratibu na miongozo inavyotuelekeza.

Mheshimiwa Spika, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na watendaji wote kwa kusimamia vyema utekelezaji wake na nawaomba waendelee na juhudi hizo ili lengo la Serikali likamilike kwa wakati. Ofisi yangu itaendelea kuziratibu Taasisi za Serikali ili kuhakikisha utekelezaji wa Ilani unafikia asilimia 100 ifikapo 2020.

Mheshimiwa Spika, katika mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, Serikali inaendelea kuchukua hatua kali za kisheria juu ya wote watakaobainika kushiriki katika kadhia hii ikiwemo wafanyaji na wale wote wanaoshiriki katika kuwalinda na kuwakingia kifua wahalifu wa udhalilishaji.  Aidha, Serikali haitamvumilia wala kumuonea aibu wala muhali mtu yeyote wa cheo chochote na ngazi yeyote pindi ikibainika kutenda jambo hilo. Waheshimiwa inatupasa tutambue kwamba, sheria ni msumeno.

Mheshimiwa Spika, navisihi vyombo vya ulinzi na usalama kupambana zaidi juu ya mambo hayo yanayoitia aibu nchi yetu pamoja na kuharibu maisha ya wananchi wetu. Ni wajibu wa jamii kutoa ushirikiano wa kutosha ili kukabiliana na tatizo hilo, kwa kuwafichua na kutoa taarifa za matukio hayo, kutozimaliza kesi hizi majumbani na nawasihi wahusika kufika mahakamani na kutoa ushahidi ili sheria iweze kuchukua mkondo wake na haki itendeke na hatimae kuvimaliza vitendo hivi katika nchi yetu. 

Mheshimiwa Spika, tayari Baraza lako Tukufu limekwishapitisha sheria ya adhabu. Sheria ambayo imeweka bayana kuwa mtuhumiwa yeyote wa kosa la udhalilishaji hatopaswa kupewa dhamana.  Sheria hiyo sasa inangojea kuwekwa saini na Mheshimiwa Rais tu ili iwe Sheria ambapo Mheshimiwa Rais ataifanya kazi hiyo baada ya muda sio mrefu.

Mheshimiwa Spika, katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Serikali kupitia Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya imeendelea na juhudi mbali mbali ikiwemo kutoa taaluma za athari za matumizi ya dawa za kulevya kwa makundi ya kijamii zikiwemo skuli 446 za Msingi na Sekondari, ambapo tayari Tume imewafikia wanafunzi 54,532.  Tume pia imetoa taaluma katika vyuo vya elimu ya juu, maeneo mbali mbali ya kazi pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama. Kadhalika, Tume imeandaa na kurusha vipindi 456 vya taaluma. Aidha, Serikali inaendelea kuzisaidia nyumba za upataji nafuu kwa vijana walioamua kwa hiyari zao kuacha matumizi ya dawa za kulevya.  Katika mwaka 2017 jumla ya vijana 370 wameweza kupatiwa huduma katika vituo hivyo Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwahimiza Wajumbe wote wa Baraza lako Tukufu na Viongozi wengine katika ngazi mbali mbali kuunga mkono juhudi za kupambana na dawa za kulevya kwa kuwaelimisha wazee na jamii nzima kwa ujumla kuondoa unyanyapaa kwa vijana ambao wameamua kuacha  matumizi ya dawa za kulevya na tuwe tayari kuwapokea na kuishi nao vijana wetu ili wajihisi kuwa ni sehemu ya jamii na wanathaminiwa na siyo kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa.  Tuwaonyeshe vijana hao kuwa hawatengwi tena na jamii.

Mheshimiwa Spika, suala la upatikanaji wa maji safi na salama mijini na vijijini limekuwa likishughulikiwa ipasavyo na Serikali yetu. Katika kuimarisha hali ya upatikanaji wa maji kwa wananchi Serikali imejipanga kutekeleza miradi mikubwa minne ifuatayo:
     i.        Mradi wa kwanza ni wa Kuimarisha Miundombinu ya Maji na Kuijengea Uwezo Mamlaka kifedha unaofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Afrika wa Awamu ya 12 (ADF 12).
Mheshimiwa Spika, Mradi huu unatarajia  kubadilisha mabomba machakavu na kuweka mabomba mapya yenye urefu wa kilomita 68 katika maeneo ya Bumbwisudi, Kinumoshi, Kianga, Welezo, Mwembe Mchomeke, Amani, Kiponda na Mji Mkongwe; na kujenga matangi 2, Saateni 1 na Mnara wa mbao 1.  Utekelezaji wa Mradi huu tayari umeshaanza na unatarajiwa kugharimu jumla ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 48 hadi kukamilika kwake.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa pili ni kuimarisha Miundombinu ya maji mjini unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).
Mheshimiwa Spika, Mradi huu utatekelezwa kwa ujenzi wa matangi katika maeneo ya Welezo juu, Welezo Magharibi na Zoni ya Migombani kwa ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 120 na uwekaji  wa umeme katika maeneo husika ya utekelezaji wa mradi huu ambao unatarajiwa kugharimu jumla ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 225.

Mheshimiwa spika, mradi wa tatu ni Mradi wa Uimarishaji wa Miundombinu ya Maji Mjini unaofadhiliwa na Serikali ya India. Huu ni mradi mpya utakaohusisha ulazaji wa mabomba katika maeneo ya Zoni ya Mfenesini, Kizimbani, Tunguu na Fumba kwa kuchimba visima, kuweka mabomba ya kuvutia maji pamoja na kuvuta umeme katika maeneo ya visima vitakavyo chimbwa. Mradi huu unatarajiwa kugharimu jumla ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 207 hadi kukamilika kwake; na
Mradi wa nne ni uchimbaji wa visima na usambazaji wa maji vijijini unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Mheshimiwa Spika, Mradi huu unahusisha uchimbaji wa visima 11 katika maeneo ya Chaani, Donge, Kisongoni, Kiboje na Miwani; pamoja na Ujenzi wa matangi 3, Kisongoni 1, Kiboje 1 na Miwani 1; pia ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 20.178 katika maeneo ya Kiboje na Miwani na uvutaji wa umeme. Mradi huu unatarajiwa kugharimu Shilingi za Kitanzania Bilioni 12 hadi kukamilika kwake.

Mheshimiwa Spika, ili miradi hiyo yote iwe endelevu, tunawaomba wananchi waondokane na dhana ya uchangiaji wa maji kuwa ni jukumu la Serikali pekee. Kwa maana hiyo tunawaomba wananchi kuchangia gharama za huduma hizo kwa wale wote wanaopata huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia miradi hiyo na gharama zake, mkopo wa Shs: Milioni 200 uliopendekezwa kutolewa kwa Serikali usingefaa chochote wala lolote.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumekuwepo na upungufu wa mafuta nchini ambao umeathiri shughuli za kiuchumi.  Upungufu huo umesababishwa na kuwepo na foleni kubwa ya upakizi katika bandari ya Dar es Salaam pamoja na kuongezeka kwa idadi kubwa ya matumizi ya nishati hiyo kwa kiwango cha juu kutoka lita Milioni 10 katika mwezi wa Disemba, 2017 hadi kufikia lita Milioni 17 kwa mwezi wa Januari, 2018.  Aidha, Serikali ilikuwa inatumia mfumo wa uingizaji wa mafuta kwa pamoja (BPS) ambao ulituwezesha kujua idadi halisi ya matumizi ya mafuta Zanzibar kwa wakati huo pamoja na kudhibiti ubora wa mafuta unaoingizwa nchini, ambapo kwa sasa mfumo unaotumika ni kila kampuni kuingiza mafuta yake wenyewe (Multiple Importation).

Mheshimiwa Spika, Serikali inalishughulikia suala la upungufu wa mafuta kwa umakini wa hali ya juu na imejipanga kuchukua hatua za muda mfupi, wa kati na mrefu ili suala la upungufu wa mafuta liwe historia nchini mwetu.  Kwa taarifa zaidi zitaelezwa kwa undani katika bajeti ijayo.  Hivyo, natoa wito kwa wananchi kuwa wastahamilivu na kwani sio nia ya Serikali kuwapa wananchi wetu usumbufu.  Serikali inalitambua suala hilo inakereka nalo na haifurahii kuwepo kwa tatizo hili hapa nchini na iko mbioni kulimaliza suala hili lisitokee tena.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ulipaji umeme kwa deni la TANESCO kwa upande wa Zanzibar, Serikali iliamuru Shirika la umeme ZECO lilipe deni la umeme kwa TANESCO kwa kiwango cha Shilingi Bilioni mbili kila mwezi na Wizara ya Fedha kulipa deni hilo kwa kiwango cha TZS Bilioni moja kila mwezi,  Shirika la umeme na Wizara ya Fedha walianza utekelezaji huo.

Katika utekelezaji huo changamoto zimejitokeza kwa upande wa Shirika la Umeme ZECO kwa kutoweza kuendelea kulipa kwa ukamilifu kiwango kilichoagizwa na Serikali cha TZS Bilioni 2 kila mwezi. ZECO imeweza kulipa deni hilo kwa kiwango kilichoagizwa na Serikali kwa kipindi cha miezi minne (4) kuanzia Juni, 2017 hadi Oktoba, 2017, miezi mengine iliyobakia ililipa deni hilo chini ya kiwango kilichoagizwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, kutoweza kutimiza agizo hilo ni kutokana na changamoto ya ukusanyaji wa mapato yanayotokana na Ankara za matumizi ya umeme kutoka kwa baadhi ya Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na zile za Muungano zilizopo Zanzibar ambayo inapelekea kutokuwa na mapato ya kutosha kulipa deni hilo kila mwezi kama ilivyoagizwa na Serikali baada ya kukidhi mahitaji mengine ya msingi ya kuliendesha Shirika hilo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ulipaji wa Ankara za matumizi ya umeme kwa Taasisi za Serikali, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliagiza Wizara ya Fedha kulipa deni la Ankara za matumizi ya umeme kwa Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi mwezi wa April, 2017. Pia, kuanzia mwezi wa Mei, 2017 Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ziliagizwa kuendelea kulipa Ankara za matumizi yao ya umeme ya kila mwezi, naamini Taasisi hizo zimeendelea kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, Viongozi wetu Wakuu Wastaafu wameitumikia nchi yetu na watu wake kwa juhudi, maarifa, uweledi na mapenzi makubwa. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitenga fedha maalum katika bajeti yake ili kuwaenzi na kuwahudumia viongozi wake hao kwa mujibu wa Sheria na hakuna hata kiongozi mmoja miongoni mwao aliyewahi kulalamika kwa kukoseshwa huduma wanazostahiki kwa mujibu wa Sheria. Nakuombeni sana Waheshimiwa Wawakilishi kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kutoa hoja zenu au kuchangia mijadala katika Baraza lako Tukufu.  Sio busara wala haikubaliki kutoa hoja kwa ajili ya kujijengea umaarufu tu bila ya kuchunguza na kuthibitisha ukweli wa hoja inayotolewa. Hii itasaidia sana kuondoa mizozo na migongano miongoni mwa wananchi na kuifanya mijadala hiyo kutokuwa na tija.

Mheshimiwa Spika, suala la kupunguza umasikini ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali yetu. Serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini TASAF Awamu ya Tatu, kwa mwezi wa Januari – Februari 2018 imelipa jumla ya TShs. Bilioni 1,096,244,000/ kwa Walengwa 30,543 Unguja na Pemba. Hivi sasa walengwa wa mpango huo wanaendelea na kazi za ajira za muda Unguja na Pemba na hivyo kuwapunguzia ukali wa maisha.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kufuatilia kwa umakini utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo unaohusisha kusaidia miradi midogo midogo inayoibuliwa na wananchi katika majimbo yote ya Unguja na Pemba. Ninawaomba Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kufuata sheria zake na kufanya marejesho kwa wakati ili Serikali iweze kukamilisha taratibu nyengine za mfuko huo.  Serikali haitatoa fedha kwa Jimbo lolote ambalo halitafanya marejesho ya matumizi ya fedha iliyotolewa awali.

Mheshimiwa Spika, elimu ndio msingi mkubwa wa mafanikio yetu katika kukuza maendeleo na mustakbali wa nchi yetu na wananchi wake. Kwa kulitambua hilo, Serikali inaendela na ujenzi wa majengo mapya ya skuli pamoja na kufanya matengenezo kwa majengo yaliyochakaa Unguja na Pemba.  Lengo ni kuwa na miundombinu iliyo bora na salama ambayo itapelekea kupata elimu bora na ya uhakika. Hivyo basi, natoa rai kwa walimu na wazazi kuwahamasisha watoto wasome kwa bidii pamoja kusimamia malezi yaliyo bora kwa watoto wetu ikiwa ni pamoja na kuzingatia mila, utamaduni na silka zetu, hususan katika kipindi hichi cha utandawazi. Vile vile, Serikali inaahidi kusimamia zaidi suala la Elimu ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya kukalia, maabara na vitabu vya kiada na ziada ili kuwa na matokeo mazuri katika mitihani yao.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina jukumu la msingi la kuhakikisha huduma za afya zinatolewa na kupatikana na wananchi wote.  Kutokana na hali hiyo, Serikali inaendelea kuimarisha utoaji wa huduma hiyo mijini na vijijini. Pamoja na hayo, Serikali inatumia fedha nyingi ili kuwanusuru wananchi wake kukabiliana na maradhi ya aina mbali mbali ikiwemo maradhi ya malaria pamoja na maradhi mengine yasiyoambukiza, kama vile sukari. pressure na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha ni kuona baadhi ya wananchi wanakataa kupigiwa dawa za mbu na vidudu vingine vinavyoweza kusababisha maradhi na wataalamu wetu. Ninawaomba wananchi waachane na tabia hizo pamoja na imani walizonazo juu ya dawa hizo. Serikali inawajali na inatambua umuhimu wa kazi hiyo kwa mustakabali wa watu wake na haipo tayari kuona jamii inakumbwa na matatizo. Ninawaomba Wajumbe wa Baraza lako Tukufu wawasimamie wananchi katika majimbo yao ili wakubali nyumba zao kupigiwa dawa na kujiepusha na maradhi yanayosababishwa na mbu.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha makaazi na kuweka mandhari nzuri ya Mji wetu wa Zanzibar, Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii - Zanzibar inaendelea na ujenzi wa nyumba za makaazi katika eneo la Mbweni Zanzibar ambao umeanza mwezi Novemba, 2015.  Mradi huu utakuwa na majengo 18 na kila jengo litakuwa na ghorofa yenye nyumba 14. Ifikapo mwishoni mwa mwezi wa Machi, mwaka huu tunategemea kukabidhiwa majengo matano (5) ambayo ni sawa na nyumba 70. Napenda kuchukua nafasi hii kuwataka wananchi kujitokeza kununua au kukodi nyumba hizi za ZSSF ambazo ni za bei nafuu.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanda Vikubwa, vya Kati na Vidogo vidogo ikiwa na madhumuni ya kukuza uchumi wa nchi, ajira na kuongeza kipato cha mtu binafsi. Kwa muktadha huu, Serikali inawaomba na kuwataka wawekezaji wa ndani na wa nje kuwekeza katika sekta hii muhimu ili kufikia katika uchumi wa kati kupitia ujenzi wa viwanda.  Viwanda vitasaidia sana uchumi wan chi na pia vitasaidi upatikanaji wa ajira kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi kijacho tunategemea kupata mvua za masika ambazo zina manufaa makubwa sana kwa nchi yetu. Nawaomba wakulima watumie vizuri mvua hizo kwa kuotesha mazao ya chakula na biashara kwani ni njia moja muhimu sana ya kuongeza vipato vyetu na kuondokana na umasikini. Hata hivyo, tunawasihi wale ambao bado wanakaa katika njia za maji na mabondeni kuchukua tahadhari kubwa sana juu ya ujio wa mvua hizo kwani nchi yetu ilikumbwa na majanga yatokanayo na mvua yakiwemo mafuriko katika kipindi kilichopita.  Mafuriko yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali.  Mamlaka husika zitaendelea kutoa tahadhari na tunapaswa kuchukua hatua kukabiliana na hali hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika mkutano wetu huu wa Tisa jumla ya Maswali ya Msingi 74 na Maswali ya Nyongeza ….. yaliulizwa na yalijibiwa na Waheshimiwa Mawaziri.  Mkutano wetu pia, umejadili kwa kina miswada mitatu muhimu ambayo ni:

i)        Mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya    Kusimamia    mwenendo wa Biashara na kumlinda           mtumiaji ya   Zanzibar Nam. 2 ya Mwaka 1995 na Kutunga   Sheria Mpya ya Ushindani Halali wa           Biashara na Kumlinda Mtumiaji, Kuweka Masharti       Bora zaidi pamoja na Mambo Mengine           Yanayohusiana na    Hayo;

ii)       Mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya Adhabu na kutunga Sheria Mpya ya Adhabu, Kuweka           Masharti Bora zaidi pamoja na Mambo Mengine          Yanayohusiana na Hayo; na

iii)  Mswada wa Sheria ya kufuta Sheria ya Mwenendo wa Jinai Nam. 7 ya mwaka 2004 na kutunga           Sheria Mpya ya Mwenendo wa Jinai na Kuweka Utaratibu Bora wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Usikilizaji wa Kesi za za Jinai na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.

Mheshimiwa Spika, Miswada yote hii ilichangiwa kwa kina na sasa tayari tumeshaipitisha kuwa sheria ambazo zitatuwekea utaratibu ulio bora zaidi wa kushughulikia kero za wananchi wetu katika maeneo ya biashara na utoaji wa haki.  Kwa kuwa Miswada hii ilijadiliwa vya kutosha sina haja ya kuongeza jambo lolote.  Hata hivyo, napenda mtambue kwamba, sheria hizi hazitafanya kazi vizuri kama hazitotungiwa kanuni baada ya kupitishwa kama tulivyokumbushwa na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Sheria Ndogo Ndogo, na kusisitizwa na Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili Tukufu.  Hivyo, nawasihi Mawaziri wote ambao bado hawajazitungia kanuni sheria zinazohusu Sekta zao wafanye hivyo mara moja.

Mheshimiwa Spika, kadhalika mkutano wetu ulipokea na kujadili Ripoti za Kamati za Kudumu za Baraza letu ambazo ni:-
1.      Ripoti ya Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Mwaka 2017/2018.
2.       Ripoti ya Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum ya Mwaka 2017/2018.
3.      Ripoti ya Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ya Mwaka 2017/2018.
4.      Ripoti ya Kamati ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii ya Mwaka 2017/2018.
5.      Ripoti ya Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Mwaka 2017/2018.
6.      Ripoti ya Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Mwaka 2017/2018.
7.      Ripoti ya Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali (PAC) ya Mwaka 2017/2018 na
8.      Ripoti ya Kamati ya Bajeti ya Mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Spika, vile vile Baraza lako Tukufu lilipokea na kujadili Ripoti ya Serikali kuhusu hoja binafsi ya Mjumbe kuhusu kuweka miundombinu bora kwa watu wenye Ulemavu katika majengo, barabara, makaazi, maeneo ya kupumzikia na maeneo mengine; Ripoti ya Serikali kuhusu maombi ya wananchi wa Kisakasaka Zanzibar kuhusu namna wanavyoweza kufaidika kutokana na machinjio ya wanyama yaliopo kwenye maeneo yao; pamoja na Ripoti ya Mapendekezo ya Muelekeo wa Mpango wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa maelezo ya jumla kuhusu ripoti zilizotolewa naomba uniruhusu kuzungumzia kidogo Ripoti ya Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC).
Serikali inaelewa wazi kuwa heshima yake mbele ya macho ya wananchi wake inategemea kwa kiasi kikubwa jinsi tunavyoshughulikia wabadhirifu wa mali ya umma. Bila shaka, Serikali yetu haitaifumbia macho Ripoti ya Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC). Watumishi wote walioguswa na ripoti hii watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria zetu. Serikali imekuwa ikifanya hivyo na itaendelea kufanya hivyo bila ya kumuonea mtu.

Mheshimiwa Spika, Ripoti zote hizi kwa jumla zinaonyesha umahiri na kiu ya maendeleo waliyokuwa nayo Wajumbe wako ya kuitaka nchi yetu iondoke hapa ilipo na ielekee kwenye maendeleo makubwa zaidi yanayojali maslahi ya wengi.  Napenda kuwaahidi Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu pamoja na wananchi kuwa, mapendekezo ya Waheshimiwa Wajumbe waliyoyatoa katika ripoti zote hizo yatafanyiwa kazi ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, Napenda kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa umakini wao wa kuyatolea ufafanuzi wa kina maswali yote yaliyoulizwa. Nawaomba tuendelee kwa bidii kutekeleza na kusimamia kazi zetu ili kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, Kwa mara nyengine tena napenda kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Wenyeviti kwa kuliendesha vyema Baraza hili. Hekima na busara zenu zimesaidia sana katika kuumaliza mkutano huu salama. Aidha, kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wote kwa kushiriki kikamilifu na kutoa michango na mapendekezo ya kuimarisha utendaji wa Serikali. Nawaomba muendelee na moyo wa kuijali Serikali na wananchi wake.

Mheshimiwa Spika, naomba kumalizia hotuba yangu kwa kuwashukuru wananchi wote kwa kuendelea kuchapa kazi na kushirikiana na Serikali yao katika maendeleo ya kila siku. Kwa mara nyengine tena napenda kuvishukuru vyombo vyetu vya habari vyote vyote vya Serikali na binafsi, pamoja na Wakalimani wetu wa lugha za alama kwa kazi zao nzuri za kuwajuvya wananchi wetu mambo yanayoendelea kwenye Baraza letu Tukufu.

Mheshimiwa Spika, mwisho napenda kuwaombea Waheshimiwa Wajumbe safari njema ya kurejea kwenye vituo vyao salama ili wakawatumikie wananchi wao na kuwaletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Baada ya kuyasema hayo, sasa naomba kuchukua fursa hii kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu liahirishwe hadi siku ya Jumatano tarehe 9 Mei, 2018 saa 3.00 barabara za asubuhi Mwenyezi Mungu akitujaalia.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.