Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia)akisalimiana na Kamishna Mpya wa Jeshi la Polisi Zanzibar Bw.Mohamed Haji Hassan alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kujitambulisha baada ya uteuzi wake na dhamana alizopewa
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Kamishna Mpya wa Jeshi la Polisi Zanzibar Bw.Mohamed Haji Hassan alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kujitambulisha baada ya uteuzi wake na dhamana alizopewa.[Picha na Ikulu.]
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja kwa
Jeshi la Polisi kuendelea kufanya kazi zake vyema hapa Zanzibar ili kuimarisha amani na utulivu iliyopo
hasa ikizingatiwa kuwa uchumi wa Zanzibar unategemea Utalii ambao unahitaji
kuwepo kwa usalama ambao ndio kivutio kikubwa cha watalii.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Kamishna wa
Polisi Zanzibar, Mohamed Haji Hassan aliyefika Ikulu kwa ajili ya
kujitambulisha kwa Rais ambapo Dk. Shein katika mazungumzo hayo alimuahidi
kumpa mashirikiano makubwa Kamishna huyo.
Katika maelezo yake,
Dk. Shein alimueleza Kamishna huyo mpya kuwa uchumi wa Zanzibar unategemea kwa
kiasi kikubwa utalii, hivyo ni vyema usalama ukaimarishwa, ili sifa ya Zanzibar
ikiunganishwa na vivutio vilivyopo izidi kuimarika na kuendelea kuwavutia
watalii kutoka pande zote za duniani.
Alieleza kuwa mapato
ya Zanzibar yamezidi kuongezeka sambamba na Pato la Taifa kutokana na
kuongezeka kwa watalii kila uchao na kupelekea kukua kwa uchumi wa Zanzibar, ambapo
hiyo yote inatokana na kuwepo kwa usalama mkubwa kwa wananchi na wageni
wanaokuja kuitembelea Zanzibar.
Hivyo, Dk. Shein
alisisitiza haja ya Jeshi hilo kuendeleza doria katika maeneo yote hapa nchini
hasa katika ukanda wa hoteli za kitalii sambamba na kuhakikisha watalii hawabughudhiwi
na badala yake wanapata huduma zote za kitalii zilizo nzuri na zenye usalama.
Aidha, Dk. Shein
alimueleza Kamishna huyo mpya wa Polisi Zanzibar haja ya kushirikiana vyema na
jamii katika kupiga vita suala la udhalilishji wa kijinsia kwa akina mama na
watoto hasa ikizingatiwa kuwa Jeshi hilo ndio linaloshughulikia mashauri ya
matukio hayo.
Aliongeza kuwa katika
kipindi cha hivi karibuni mabadiliko makubwa yametokea katika kupiga vita
vitendo hivyo, baada ya kuundwa Kikosi Kazi ambacho kinafanya kazi vizuri sambamba
na kuwepo kwa Mahakama ya Watoto huku akimueleza hatua zilizofikiwa na Serikali
katika Sheria ya Udhalilishaji
iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar hivi karibuni.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumueleza Kiongozi huyo haja ya kuwepo kwa
mashirikiano katika kupambana na rushwa hapa Zanzibar na kumueleza hatua
zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kupambana na suala hilo
ikiwemo kutunga Sheria na Sera yake pamoja na kuundwa kwa Mamlaka ya Kuzuia
Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ambayo inaendelea na kazi zake vyema.
Dk. Shein pia,
alimueleza Kamishna huyo mpya wa Polisi Zanzibar, haja ya kuwepo kwa umakini
kwa askari wa usalama barabarani katika kuhakikisha sheria za usalama
barabarani zinafuatwa.
Alieleza kuwa kumekuwa
na matukio mengi ya ajali za barabara ambazo hupelekea vifo na nyengine
husababisha ulemavu wa kudumu kwa wananchi hali ambayo inatokana na baadhi ya
madereva kutofuata sheria za usalama barabarani.
Akisisitiza suala
hilo, Dk. Shein alieleza kuwa hata yeye mwenyewe kwa upande wake amekwua
akisisitiza suala la kufuata sheria za usalama barabarani katika hotuba zake,
zikiwemo zile za Idd El Fitri na Idd El
Hajj ambazo huwataka wananchi wakiwemo madereva wa gari kufuata sheria za usalama
barabarani katika vipindi vya sikukuu na katika siku za kawaida.
Alieleza kuwa lakini, bado
kuna ugumu wa baadhi ya madereva kutofuata sheria hizo, sambamba na baadhi ya askari
wa usalama barabarani kutokuwa na kasi ya kuhakikisha sheria hizo zinafuatwa.
Hivyo, alieleza haja
ya kuwafundisha wananchi juu ya sheria za barabarani, licha ya juhudi
zinazochukuliwa na baadhi ya viongozi wa Jeshi la Polisi kutoa elimu kupitia
vyombo vya habari lakini ipo haja ya kuongeza kasi kwani hali hairidhishi katika
jambo hilo sambamba na kueleza haja ya kuwepo mashirikiano na Idara husika ya
leseni katika kuhakikisha utoaji wa leseni unafanywa kwa taraibu na sheria
zilizopo.
Nae Kamishna wa Polisi
Zanzibar Mohamed Haji Hassan alimueleza Rais Dk. Shein azma yake ya kuhakikisha
anatoa ushirikiano mkubwa na Jeshi la Polisi linaendelea kufanya kazi zake
vyema, ili kuendeleza usalama kwa wananchi, mali zao pamoja na wageni wanaokuja
kuitembelea Zanzibar.
Sambamba na hayo,
Kamishna huyo alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Dk. Shein uzoefu wake wa kazi
katika Jeshi hilo pamoja na mafunzo yake aliyoyapata ndani na nje ya Tanzania.
Mnamo Februari 10,
2018 Rais, Dk. John Pombe Magufuli alimpandisha Cheo Kamishna Mohamed Haji
Hassan kutoka Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na kuwa Kamishna wa Polisi (CP)
na kisha kumteua kuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar.
Kufuatia uteuzi wake
huo, mnamo Februari 12 mwaka huu, kwa niaba ya Rais Dk. Magufuli Mkuu wa Jeshi
la Polisi (IGP) Simon Nyakoro Sirro alimuapisha Kamishna Hassan kuwa Kamishna
wa Polisi Zanzibar na kushika nafasi iliyowachwa wazi na Kamishna wa Polisi ndugu
Hamdani Omar Makame ambaye amestaafu.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment