Habari za Punde

Makamu Mwenyekiti wa UWT Thuwaiba Kisasi Akiwa Ziarani Kutembelea Afisi za Jumuiya.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi (UWT),Thuwayba Kisasi, amesema maendeleo yaliyopatikana ndani ya Umoja huo yametokana na juhudi, uchapakazi na ushirikiano wa kudumu wa waasisi, viongozi na watendaji wa zamani wa Umoja huo.
Kauli hiyo ameitoa katika mwendelezo wa ziara yake ya kuwatembelea viongozi hao wa zamani  waliowahi kufanya kazi ndani ya Umoja huo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, amewataka viongozi na watendaji wa sasa kutumia ushauri na maelekezo ya viongozi wa zamani kama nyenzo ya kuongeza ufanisi katika UWT.
Ndugu Thuwayba alisema ili Umoja huo uweze kuendelea kufanya kazi zake vizuri kisiasa, kiutendaji na kiuongozi ni lazima viongozi na watendaji wa taasisi hiyo, kushirikiana na kufanya kazi kwa mujibu wa miuongozo ya kikanuni na Katiba ya CCM ya mwaka 1977 kwa lengo la kutekeleza kwa vitendo mambo mema yaliyotekelezwa na wastaafu hao.
Makamu Mwenyekiti huyo aliwataja viongozi hao wa zamani kuwa ni hazina inayotakiwa kuenziwa kwani wakati wa uongozi wao wamefanya mambo yenye manufaa kwa Taifa ambayo ndio chimbuko la Chama cha Mapinduzi  kuwa imara tangu enzi za ASP.
“ Viongozi wetu wastaafu wa UWT wametulea katika misingi bora inayotuwezesha leo kuwa na uwezo wa kusimama popote kujenga hoja imara na kuwaongoza wengine bila hofu.
Lakini huu ni mwanzo tu bali tutaendelea kukutembeleeni mara kwa mara ili muweze kutuongoza sambamba na kuzifanyia kazi kwa wakati nasaha zenu.”, alisema Makamu Mwenyekiti huyo.
Nao waasisi hao wakizungumza kwa wakati tofauti wamesifu kasi ya kiutendaji ya Makamu Mwenyekiti huyo na kumuelekeza aendelee kufanya ziara za mara kwa mara kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili Akina mama na wananchi wote na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Kwa upande wake Bi. Mtumwa Fikirini aliyewahi kushika nyadhifa mbali mbali za Uongozi toka enzi za ASP, alisema ili UWT iendelee kuwa imara ni lazima viongozi na watendaji wawe sehemu ya kukabili changamoto za Wanawake na wananchi kwa ujumla.
Aliwashauri Viongozi hao wa UWT kuhakikisha wanakuwa karibu na vijana wa UVCCM ili kuwafunza mambo mema ya uongozi, maadili na siasa zenye tija kwa wananchi wote, kwani vijana hao ni muhimu kuwaanda hivi sasa kwa lengo la kuwa viongozi wazuri wa baadae.
Naye Bi.Mariam Mohamed amewasisitiza UWT kuendelea na utamaduni wa Umoja na mshikamano katika maisha yao ya kila siku, huku wakikilinda na kukipigania Chama cha Mapinduzi kwa kila Uchaguzi kiendelee kuongoza nchi kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Ziara hiyo imeendelea katika Mkoa wa UWT Mjini na Kusini Unguja na kuwatembelea viongozi hao akiwemo Bi.Sihaba Farhan Ismail, Bi, Mvita Mussa Kibendera, Bi.Asha Simba, Bi. Panya Sariboko, Bi. Mtumwa Fikirini, Bi. Khadija Jabir pamoja na Bi. Mariam Mohamed.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.