Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. Azungumza na Ujumbe UNICEF na KOICA.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa Pili kutoka Kulia akizungumza na Ujumbe wa Viongozi kutoka Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa {UNICEF} na ule wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la Korea { KOICA} hapo Baraza la Wawakilishi Chukwani.
Balozi Seif  kushoto akisisitiza jambo akiwa pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya EK Heavy Industries ya Korea Kuisni Bibi Bong-chol Lee wakati wa mazungumzo yake na Ujumbe wa Taasisi hizo.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Viongozi kutoka Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa {UNICEF} na ule wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la Korea { KOICA} mbele ya Jengo la Baraza la Wawakilishi mara baada ya mazungumzo yao.
Balozi Seif akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya EK Heavy Industries ya Korea Kuisni Bibi Bong-chol Lee mbele ya Jengo la Baraza la Wawakilishi mara baada ya mazungumzo yao.
Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Korea { KOICA} Bwana Joonsung Park akimsisitiza Balozi Seif nia ya Kampuni yake kutaka kuendelea kuunga mkono maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar
Mkurugenzi  Idara ya Kinga Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Fadhil Abdullah wa Pili kutoka Kushoto akifafanua jambo katika mazungumzo ya Balozi Seif na Ujumbe wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto {Unicef} na ule wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Korea {Koica}.Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema maradhi ya Kipindupindu yanayoibuka baadhi ya wakati Nchini yanaweza kutoweka na kubakia kuwa Historia Visiwani Zanzibar iwapo Jamii itazingatia utaratibu sahihi wa utunzaji wa mazingira katika maeneo wanayoishi.
Alisema tabia ya ujenzi holela unaofanywa na baadhi ya Watu usiohusisha Mipango Miji katika maeneo ya mabondeni umekuwa ni chanzo cha Maradhi ya miripuko inayosababishwa na mafuriko ya maji yanayochanganyika na yale yaliyomo kwenye vyoo na Makaro ya Nyumba zinazojengwa sehemu hizo.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Ujumbe wa Viongozi kutoka Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa {UNICEF} na ule wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la Korea { KOICA} ambao hushirikiana katika kuiunga Mkono Tanzania kwenye mapambano dhidi ya maradhi ya Kipindupindu hapo katika majengo ya Baraza la Wawakilishi Chukwani.
Alisema kesi nyingi za maradhi ya kipindupindu huripotiwa kutokea katika maeneo hatarishi ya Mabondeni ambayo baadhi ya Wananchi waliamua kujenga nyumba za makaazi ya kudumu jambo ambalo litaendelea kuleta athari katika maisha yao kama hawakuliepuka hasa wakati wa msimu wa mvua  kubwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alilipongeza Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa {UNICEF}, Shirika la Misaada ya Maendeleo la Korea pamoja na washirika wa Maendeleo kwa jitihada wanazochukuwa za kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwenye ustawi wa Jamii.
Mapema Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Korea          { KOICA} Bwana Joonsung Park alisema Taasisi yake kwa kushirikiana na Unicef  itaendelea kushirikiana na Zanzibar na Tanzania kwa pamoja katika kuona ustawi wa Wananchi wa Taifa hili unaimarika zaidi.
Bwana Joonsung alisema yapo mafanikio makubwa ya juhudi za pamoja zilizochukuliwa na kupatikana katika mapambano dhidi ya Maradhi ya Kipindipindu Nchini jambo ambalo limeleta faraja itakayowapelekea kuongeza msukumo wa uwajibikaji zaidi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Fadhil  Abdullah alisema njia pekee ya Jamii kujiepusha na maradhi ya Mripuko ikiwemo Kipindupindu izingatie usafi wa mazingira.
Dr. Fadhil alisema ujenzi wa vyoo unaokwenda sambamba na utumiaji wa vyakula vilivyohifadhiwa na vyenye vuguvugu ndio kinga pekee ya kujiepusha na maradhi hayo kwa asilimia kubwa.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifanya mazungumzo na Ujumbe wa Viongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya U&I na ile ya EK Heavy Industries ya Korea Kusini hapo Ofisi ya Watu Mashuhuri {VIP} katika Majengo ya Baraza la Wawakilishi Chukwani.
Katika mazungumzo yao Mkurugenzi wa Kampuni ya Drums of Africa ya Zanzibar Bwana Haroun Mohamed ambae Kampuni yake imetiliana saini Mkataba wa Ubia katika Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar na ile ya U&I alisema Taasisi hizo zimekusudia kuanzisha Kiwanda cha kuunganisha simu aina ya Smart Phone.
Bwana Haroun alisema  mradi huo utakaosaidia kutoa ajira kwa Vijana zaidi ya 50 na wengine 10 kupata nafasi za masomo Nchini Korea utasaidia kutoa huduma za biashara za simu katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Drums of Africa alimueleza Balozi Seif kwamba hivi sasa Wataalamu wa Taasisi hizo wako katika hatua ya matengenezo ya Majengo yatakayoenda sambamba na ufungaji wa Mitambo itakayoendesha Kazi hiyo katika kipindi kifupi kijacho.
Akigusia Kampuni ya EK Heavy Industries Co. yenye uwezo wa Teknolojia ya Kisasa  Duniani Bwana Haroun Mohammed alisema Uongozi wa Taasisi hiyo uko tayari kubadilishana uzoefu na Zanzibar katika sekta za Usafiri wa Baharini, ujenzi wa Nyumba za Kisasa, huduma za maji na Umeme.
Alisema ujumbe wa Viongozi wa Taasisi hizo mbili za Korea  ambao upo Nchini tayari umeshafanya mazungumzo na baadhi ya Viongozi waandamizi wa Serikali na kufikia hatua ya matumaini katika Nyanja ambazo wanaweza kuwekeza Miradi ya Kiuchumi Nchini.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliueleza Uongozi wa Taasisi hizo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa kila aina ya msaada  utakaohitajika katika kuona nia yao ya kutaka kuangalia fursa za Uwekezaji Nchini inafanikiwa vyema.
Balozi Seif alisema Zanzibar imefungua milango ya uwekezaji kwa Makampuni, Mashirika na Taasisi zozote za Kitaifa na Kimataifa katika azma yake ya kuimarisha Uchumi, kuongeza Pato la Taifa na kuwafanya Wananchi wake  kustawika Kimaisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.