Habari za Punde

Mwenyekiti Bodi ya Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Zanzibar Azungumza na Watendaji Kisiwani Pemba.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar,Ndg.Abdulghani Himid Msoma,akizungumza na Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo wa Kisiwani Pemba katika Mkutano wake wa kuwaaga baada ya kumaliza muda wake wa nafasi hiyo hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Kiwanja cha Ndege cha Karume Chakechake Pemba. 

Baadhi ya watendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Pemba,wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi inayomaliza muda wake , Abdulghani Himid Msoma , wakati wa kuagana nao kutoka na bodi hiyo kumaliza muda wake.

Na. Bakari Mussa -Pemba.
Uongozi wa mamlaka ya Viwanja vya ndege Zanzibar , umepongezwa kwa juhudi zake kubwa inazozichukuwa katika kutowa huduma bora kwa wageni wanaoingia nchini  hali ambayo imeongeza mapato makubwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akizungumza na Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo, Katika Kiwanja cha ndege cha Karume Pemba, Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka hiyo, Abdughani  Himid Msoma , wakati wa kuagana na Wafanyakazi hao kufuatia kumaliza muda kwa Bodi hiyo , alisema mamlaka ili kumbana na changamoto mbali mbali ikiwemo kuibadilisha kutoka Idara ya 
Anga hadi Mamlaka na hivyo watendaji wake walionesha Uzalendo wa hali ya juu na kufanyakazi kwa uadilifu jambo ambalo mapato yatokanayo na Viwanja vya ndege yameongezeka kwa asilimia kubwa.

Alieleza Bodi ya mamlaka ya Viwanja vya ndege , ilipata mashirikiano makubwa kutoka kwa watendaji wa Viwanja vya Ndege Unguja na Pemba, na hivyo kuiwezesha kufanyakazi kwa weledi na ufanisi ulio mkubwa jambo ambalo limepelekea mapato kuongezeka tafauti na kabla yakuwepo kwa mamlaka hiyo.

Msoma, aliwataka Wafanyakazi na Uongozi wa Mamlaka hiyo kuzidisha ushirikiano , bidii na uaminifu katika kazi zao kwa kusimamia mapato  ili waweze kuisaidia Serikali katika kukusanya mapato makubwa yatakayo iwezesha kumudu kufanya shunghuli mbali mbali za Maendeleo.

“Wafanyakazi wa Mamlaka hii tambueni kuwa mafanikio  makubwa yamekuja kutokana na ushirikiano mkubwa muliokuwa nao baina yenu na Bodi na wafanyakazi na watendaji wenu wakuu , hivyo naomba ushirikiano huu uendelee kwani Serikali inahitaji mapato zaidi kwa ajili ya maendeleo ya Wananchi na kuviboresha zaidi Viwanja vyenu ili viweze kutowa huduma mzuri kwa wageni,”alisema.

Alifahamisha katika Uongozi wake wa kuiongoza Bodi hiyo kwa muda wa miaka sita , alipata mafanikio makubwa na hivyo kuwataka wafanyakazi hao kuwa tayari kupokea mabadiliko yatakayokuja ya Bodi mpya baada ya kuteuliwa kwake sambamba na kuipa mashirikiano makubwa ili iweze kuleta maendeleo zaidi.

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi hiyo inayomaliza muda wake, Bihindi  Nassor Khatib, aliwataka watendajiwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar kuendelea kutowa huduma mzuri kwa Wageni kwani kila mmoja ataweza kuvutika na  namna anavyopata huduma na hivyo wataweza kuongeza mapato.

Aidha, aliiomba mamlaka husika kuangalia uwezekano wa kuongeza asawa wa ajira na hata uteuzi wa wajumbe wa Bodi kwani inaonekana ajira kwa jinsia ya kike na uteuzi ni ndogo akitolea mfano katika Bodi hiyo Mwanamke ni yeye peke yake.

“Tukiangalia hapa jinsia ya kike ni ndogo kwenye ajira za Wafanyakazi wa Mamlaka hii, hata kwatika Uteuzi mjumbe ni mimi peke yangu naomba wakati mwengine lizingatiwe hilo, “ alisema Mjumbe huyo.

Nae , Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Zanzibar, Captein, Said  Iddi Ndumbogani, kwa niaba ya Uongozi wa Mamlaka hiyo aliipongeza Bodi hiyo inayomaliza muda wake kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo jambo imeipatia mafanikio makubwa mamlaka kutokana na busara na maelekezo yao yanalioendana na ufanisi wa kazi za kila siku.

Aliwataka Wafanyakazi kuendelea kufanyakazi kwa bidii sambamba na kufanyakazi kwa kufuata maelekezo yaliokuwa yanatolewa na Bodi hiyo , ili waweze kujiletea maendeleo zaidi .

“Bodi ilikuwa ikituelekeza sana katika mambo mbali mbali ya ufanisi wa majukumu yetu ya kazi za kila siku, hivyo nawaomba wafanyakazi wenzangu tuzidi kushikamana kufanyakazi kwa weledi na Uaminifu kama tulivyokuwa tukisimamiwa na Bodi hii, inayomaliza muda wake,” alieleza.

Nae, Mwanasheria wa Bodi hiyo , Awadhi Ali Said, aliwasihi Wafanyakazi kuendelea kufanyakazi zao kwa bidi na maarifa yatakayopelekea kufikia malengo yaliowekwa na Serikali juu ya kuwepo kwa Viwanja vya ndege vya kisasa Zanzibar kwa ajili ya kukuza Utalii na kuongeza mapato ya Taifa.

Alisema ili kufikia malengo makubwa na ya kweli ni vyema kwa watendaji hao kukaa na kujipima kutokana na huduma wanazozitowa ambazo zitawavutia wageni wanaoingia , ikiwemo Watalii.

Kwa upande wake , Makamo mwenyekiti wa Bodi ya  Mamlaka ya Viwanja vya ndege inayomaliza muda wake , Hamad Bakar Mshindo, aliwataka wafanyakazi kufanyakazi zao kwa kufuata misingi ya kanuni za utumishi wa Serikalini jambo ambalo wataweza kumtumikia mwajiri wao ipasavyo na wao kuweza kupata haki zao bila ya matatizo.

Aliwasihi wafanyakazi hao kuzidisha bidii katika kazi na kuipa mashirikiano ya kiutendaji Bodi mpya itakayokuja kwa misingi ya kuleta mafanikio katika Mamlaka hiyo , kama vile walivyokuwa wakiipa mashirikiano Bodi inayoondoka.


Hivyo Wafanyakazi wa mamlaka hiyo waliipongeza Bodi hiyo kwa utendaji wao ambao ulileta mageuzi makubwa ambayo yameweza kuongeza   makusanyo ya  mapato katika Viwanja vya ndege na kwamba watajitahidi kutowa mashirikiano kwa bodi itakayo fuatia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.