Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akisalimiana na Balozi wa Tanzania Nchini Sweden Mhe.Wilbroad Peter Slaa alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha pia na kumuaga Rais baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo na Rais waJamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.[Picha na Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akisalimiana na Balozi wa Tanzania Nchini Nigeria Mhe.Muhidin Ally Mboweto alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na kumuaga Rais baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo na Rais waJamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.[Picha na Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Balozi wa Tanzania Nchini Sweden Mhe.Wilbroad Peter Slaa (katikati) na Balozi wa Tanzania Nchini Nigeria Mhe.Muhidin Ally Mboweto walipofika Ikulu Mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha na kumuaga Rais baada ya kuteuliwa kushika nafasi hizo na Rais waJamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.[Picha na Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akimsikiliza Balozi wa Tanzania Nchini Sweden Mhe.Wilbroad Peter Slaa (katikati) wakati wa mazungumzo yao na Balozi wa Tanzania Nchini Nigeria Mhe.Muhidin Ally Mboweto (kushoto) walipofika Ikulu Mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha na kumuaga Rais baada ya kuteuliwa kushika nafasi hizo na Rais waJamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.[Picha na Ikulu.]
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akifuatana na Balozi wa Tanzania Nchini Sweden Mhe.Wilbroad Peter Slaa baada ya mazungumzo yao na Balozi wa Tanzania Nchini Nigeria Mhe.Muhidin Ally Mboweto(hayupo pichani) walipofika Ikulu Mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha na kumuaga Rais baada ya kuteuliwa na Rais waJamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kushika nafasi hizo .[Picha na Ikulu.]
STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 26.2.2018
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesisitiza haja kwa Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha
Tanzania nchini Sweden na Nigeria kutilia mkazo Sera ya Diplomasia ya Uchumi
ili Tanzania iweze kutekeleza malengo iliyojiwekea katika kuimarisha uchumi
wake.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na Mabalozi wanaokwenda
kuiwakilisha Tanzania katika nchi hizo, waliofika Ikulu kumuaga Rais pamoja na
kujitambulisha na hatimae kufanya nao mazungumzo.
Mabalozi hao ni Balozi
Wilbroad Peter Slaa, Balozi wa Tanzania
nchini Sweden na Balozi Muhidin Ally Mboweto, Balozi wa Tanzania nchini
Nigeria.
Katika maelezo yake Dk.
Shein alisema kuwa shabaha kuu ya Serikali zote mbili , Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuimarisha sekta
za kiuchumi na huduma za jamii ikiwemo sekta ya viwanda,utalii, uvuvi pamoja na elimu na utamaduni.
Dk. Shein alieleza
kuwa Serikali zote mbili zimedhamiria kutekeleza
Diplomasia ya uchumi katika kuhamasisha uwekezaji hasa katika sekta ya viwanda
kwani ndio kiu ya uchumi wa Tanzania hivi sasa.
Akizungumzia kwa
upande wa Zanzibar, Dk. Shein alisema kuwa licha ya Zanzibar kuwa ni visiwa
ambavyo vimezungukwa na bahari sambamba na kuwa na azma ya kutekeleza uchumi wa
bahari lakini bado hakuna viwanda vya samaki au viwanda vyenye kutumia
rasilimali za baharini.
Alieleza kuwa eneo la
bahari la Zanzibar ni maarufu sana kwa samaki aina ya jodari ambaye ni samaki anaependwa
duniani lakini wamekuwa hawavuliwi ipasavyo na badala yake hutokea meli kubwa za
kigeni za uvuvi ambazo huja kuwavua kwa kuwaiba na kutolea mfano kuwa hivi
karibuni kuna meli zimekamatwa zikifanya uhalifu huo.
Dk. Shein alieleza
kuwa kuwepo kwa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambayo makamo makuu yake yapo hapa Zanzibar maeneo ya Fumba, ni
jitihada maalum za Serikali hiyo katika kuhakikisha Tanzania ikiwemo Zanzibar
inaimarisha sekta ya uvuvi na inapata mafanikio kutoka katika sekta hiyo.
Hivyo, Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuwaeleza Mabalozi hao kuwa Zanzibar inawakaribisha wawekezaji
kutoka Sweden na Nigeria kuja kuwekeza katika viwanda vya samaki.
Aidha, Dk. Shein
alieleza haja ya Mabalozi hao kuitangaza Zanzibar na Tanzania nzima kiutalii
ambapo kwa upande wa Zanzibar sekta hiyo imekuwa ni muhimu kutokana na
kuchangia asilimia 27 ya pato la Taifa na asilimia 80 ya fedha za kigeni.
Dk. Shein alieleza
kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ifikapo mwaka 2020 ni kupokea
watalii zaidi ya laki tano kutokana na mikakati iliyopo hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar
inavivutio vingi vya kitalii vikiwemo viungo.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliwatakia heri na fanaka Mabalozi hao katika utendaji wao wa kazi kwenye Balozi hizo na kuwaahidi kuwa
ataendelea kutoa ushirikiano wake kwa Mabalozi hao kwa lengo la kutekeleza
vyema dhamana zao hizo.
Pia, Dk. Shein
alisisitiza haja ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano na nchi hizo katika
kuimarisha sekta ya elimu hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar ina ushirikiano mzuri
na Nigeria ambayo imekuwa ikileta walimu wa mafunzo ya Sayansi kwa awamu huku
akieleza uhusiano wa kihistoria na Sweden katika kuisaidia Zanzibar kwenye
sekta ya elimu.
Nao Mabalozi hao
walimthibitishia Dk. Shein kuwa
wamepokea maelekezo na miongozo yote aliyowapa na kumuahidi kuyafanyia kazi
hasa kwa maeneo maaluma ya Zanzibar na yale ya Tanzania Bara sambamba na
kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hizo wanazoenda
kufanya kazi.
Akitoa maelezo kwa upande
wake Balozi Wilbroad Peter Slaa, Balozi
wa Tanzania nchini Sweden alimueleza Dk. Shein kuwa watafanya jitihada kwa
nguvu zao zote katika kuhakikisha kuwa lengo la kuimarika kwa Tanzania kiuchumi
linafanikiwa.
Aliongeza kuwa kwa
vile Zanzibar imezungukwa na Bahari, hivyo suala la kuimarishwa kwa sekta ya
uvuvi atalipa kupaumbele hasa ikizingatiwa kuwa nchi anazokwenda kufanya kazi zikiwemo
Sweden, Denmark, Norway, Finland zimepiga hatua kubwa katika sekta hiyo .
Nae Balozi Muhidin
Ally Mboweto, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria alimuhakikishia Rais Dk. Shein
kuwa atafanya juhudi za makusudi katika kuhakikisha mashirikiano katika sekta
ya elimu kati ya Nigeria na Tanzania yanaimarika ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi
ya walimu wa Sayansi kutoka nchini humo kuja
Zanzibar pamoja na kuanzisha mfumo huo kwa upande wa Tanzania Bara ambako kuna
changamoto kama hiyo.
Aidha, alimuhakikishia
Rais Dk. Shein kuwa atachukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha anawavutia
wawekezaji kuja kuekeza katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo
viwanda, uvuvi na sekta nyenginezo.
Mabalozi hao walimuhakikishia
Dk. Shein kuwa katika wadhifa wao huo juhudi za makusudi watazichukua kwa
mashirikiano ya pamoja katika kuhakikisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati
ya nchi hizo na Tanzania unaimarishwa zaidi ikiwa ni pamoja na kuitangaza
Tanzania ikiwemo Zanzibar kiutalii kwa azma ya kuimarisha maslahi ya kiuchumi kwa
pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment