Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akiutubia wakati akiufungua Mkutano Mkuu wa Sita wa Chama cha Walimu Zanzibar katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilushi Kikwajuni Zanzibar leo 10-2-2018.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa bila ya
kuwa na walimu wenye dhamira ya dhati ya kufundisha katika ngazi zote za elimu itakuwa
ni ngumu kupata maendeleo ya kweli yanayokwenda sambamba na mabadiliko na
mwelekeo wa karne ya 21.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko katika ukumbi wa Baraza la zamani la Wawakilishi, Kikwajuni mjini
Unguja katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa Chama cha Walimu
Zanzibar (ZATU).
Katika hotuba hiyo,
Dk. Shein alieleza kuwa hakuna mtaalamu
duniani ambae hakuandliwa na mwalimu kwa njia rasmi au isiyo rasmi, na kuwaeleza
walimu hao jukumu kubwa walionalo katika kuitoa Zanzibar hapa ilipo na
kuipeleka kule ambako wananchi wanataka kwenda.
Dk. Shein alieleza
kuwa mataifa mengi yaliyopiga hatua za haraka katika karne ya 21, yaliweka
mkazo kwa kuwekeza katika elimu kwani fedha pekee yake haiwezeshi Taifa lolote
lile kupata wataalamu wazalendo inaowataka.
“Wataalamu wazalendo
wahitaji kutayarishwa na walimu wazalendo, kuanzia ngazi ya msingi hadi Chuo
Kikuu”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alieleza kuwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimepelekea kuanzishwaa vyuo vikuu
ambavyo tayari vipo vitatu vinavyoendeshwa na wataalamu wazalendo ambapo kwa
mwaka huu wa masomo uliomaliza, vyuo hivyo vimeweza kutoa jumla ya wahitimu
4,287.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein aliipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na walimu wote kwa matokeo
mazuri yaliopatikana kwa niaba yake na Serikali kwa jumla kutokana na ufaulu wa
wanafunzi wote waliofanya mitihani ya Taifa wakiwemo wa darasa la nne, darasa
la sita, kidato cha Pili, Kidato cha Nne na Kidato cha Sita.
Hata hivyo, kutokana
na ufaulu wa kidato cha nne kushuka, Dk. Shein aliuagiza uongozi wa Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Amali uandae mkutano maalum na walimu wa skuli saba za
sekondari za Zanzibar zilizomo katika orodha ya skuli 10 zilizofanya vibaya kwa
Tanzania nzima mwaka 2017.
Alieleza kuwa katika
mkutano huo wajadili sababu zilizopelekea skuli hizo zifanye vibaya sambamba na
kuandaa mkakati maalum ili kuondokana na tatizo hilo na kumtaka Waziri wa Wizara
hiyo kuongoza mkutano huo ambapo alisikitishwa na hali hiyo na kueleza kuwa
wanafunzi wa Zanzibar wanaweza kufanya vizuri iwapo watapata maelekezo mazuri
kutoka kwa walimu wao kwani Zanzibar ina historia nzuri kielemu.
Dk. Shein alisema kuwa
Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya elimu kwa kila mwaka, ili sekta hiyo izidi
kuimarika ambapo TZS Bilioni 120.726 ziliingiziwa Wizara hiyo mnamo mwaka
2015/2016,TZS Bilioni 133.501 mwaka 2016/2017 na TZS Bilioni 197.290 mwaka
2017/2018 na kuahidi kuongeza zaidi kwa mwaka 2018/2019.
Alieleza kuwa wapo
baadhi ya walimu wanaharibu fani ya uwalimu ambayo ni fani yenye heshima kubwa
kutokana na tamaa zao na wale ambao wanaingiza siasa katika fani hiyo huku
akieleza kukerwa na tabia ya baadhi ya walimu kufanya biashara ya urojo na
biskuti skuli huku wakisingizia kushuka kwa elimu wakati wao ndio chanzo.
Aidha, Dk. Shein
alieleza kuwa katika kuongeza ufanisi wa maendeleo ya skuli suala la ukaguzi wa
skuli na walimu ni muhimu lakini kwa bahati mbaya suala hilo limekuwa halifanywi
vizuri.
Pia, Dk. Shein
alieleza kuwa wakati alipofanya ziara za Mikoa mnamo mwezi Agosti 2017 aliagiza
uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, ushirikiane na viongozi wa
Mikoa na Wilaya katika kuzifanyia kazi changamoto ya kuwepo kwa utoro
uliokithiri wa walimu na wanafunzi lakini hadi leo hajapelekewataarifa yoyote.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein aliwaeleza walimu hao kuwa katika ombi lao la kuwapatia posho walimu
wakuu la asilimia 50 Serikali haiwezi kufanya hivyo hadi pale walimu hao nao
kwa upande wao wajue wajibu wao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi
wanafanya vizuri katika masomo yao.
Pia, Rais Dk. Shein
aliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuhakikisha inashirikiana
na Wizara ya Fedha na Mipango inawalipa walimu malimbikizo yao yote wanayodai
ili mwakani kwenye mkutano kama huo wasijekuleta madai hayo na badala yake waelezee
mafanikio na mambo mengineyo kuhusu chama hicho cha walimu Zanzibar na sio
kudai fedha zao za malimbikizo.
Kuhusu Muundo wa
Utumishi wa Wizara ya Elimu, Dk. Shein aliitaka wizara hiyo kwa kushirikiana na
Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuwarudishia walimu
na kuhakikisha wanalipwa haki zao zote pamoja na kuziangalia Wizara nyenginezo
zote kwani tayari ameshatoa agizo ya kufanyiwa kazi suala hilo.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliitaka Wizara ya Elimu kuhakikisha wanakutana na uongozi na wajumbe wa
chama hicho angalau mara mbili kwa mwaka na katika mkutano huo watumie fursa
hiyo kujadili na kupokea maoni kutoka kwa chama hicho yenye mustakbali wa
kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Nae Kaimu Waziri wa
Wizara hiyo, Mahamoud Thabit Kombo, ambaye pia, ni Waziri wa Afya alieleza kuwa
miongoni mwa sababu zinazopelekea kuwepo kwa changamoto katika elimu ikiwemo ya
wingi wa wanafunzi madarasani ni kuongezeka kwa idadi ya watu Zanzibar hasa
ikizingatiwa kuwa katika nchi za Afrika, idadi ya watu Zanzibar imekuwa
ikiongezeka kwa asilimia kubwa.
Nae Rais wa Chama
hicho Mwalimu Seif Mohamed alitoa pongezi zake kwa Rais Dk. Shein kutokana na
juhudi za makusudi anazozichukua katika kuangalia maslahi ya wafanyakazi wa
Serikali wakiwemo walimu.
Mapema Katibu Mkuu wa
Chama hicho cha Walimu Zanzibar Mussa Omar Tafurwa alisoma risala ya Walimu na
kueleza mafanikio iliyoyapata Jumuiya hiyo sambamba na changamoto zilizopo
ikiwa ni pamoja na kueleza haja ya walimu wakuu kupewa posho la asilimia 50 ya
mishahara yao, madai yao na malimbikizo wanayodai pamoja na mambo mengineyo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment