Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk. Shein Azungumza na Balozi wa Nigeria Nchini Tanzania.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akisalimiana na Balozi wa Nigeria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Sahabi Isa Gada  alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akimsikiliza mgeni wake  Balozi wa Nigeria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Sahabi Isa Gada wakati wa mazungumzo yao  alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kwa ajili ya kujitambulisha.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na  Balozi wa Nigeria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Sahabi Isa Gada  alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kwa ajili ya kujitambulisha


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na   mgeni wake  Balozi wa Nigeria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Sahabi Isa Gada (wapili kulia) wakati wa mazungumzo yao  alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kwa ajili ya kujitambulisha akiwa na ujumbe aliofuatana naoRais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akifuatana na mgeni wake  Balozi wa Nigeria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Sahabi Isa Gada baada ya mazungumzo yao  alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kwa ajili ya kujitambulisha.[Picha na Ikulu.] 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Serikali ya Nigeria kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu na kueleza haja ya kuendelea na hatua hiyo kwa sekta nyengine ili kuzidisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na nchi hiyo.

Akizungumza na Balozi mpya wa Nigeria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Sahabi Isa Gada Ikulu mjini Zanzibar,  Dk. Shein alieleza kuwa uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya  Nigeria na Zanzibar una historia kubwa kwani nchi hiyo ni miongoni mwa nchi za mwanzo zilizoiunga mkono Zanzibar katika sekta ya elimu mara tu baada ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.

Katika Mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa hatua ya ujio wa walimu wa Sayansi  kutoka nchini Nigeria kwa ajili ya kuja kusomesha skuli za Sekondari za Zanzibar ni ushahidi mzuri wa kuonesha kuimarika kwa uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo  

Alieleza kuwa katika juhudi za kuiunga mkono Zanzibar kwenye sekta ya elimu ujio wa walimu 16 hapo kesho ambao wanakuja kwa makundi kutasaidia katika kuimarisha sekta ya elimu hapa nchini.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya elimu na kueleza kuwa juhudi hizo ni muendelezo wa uhusiano ulioanzishwa na muasisi wa Taifa la Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati  Benjamin Nnamdi Azikiwe Rais wa kwanza wa Nigeria.

Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi Gada haja ya kuendeleza mahusiano na ushirikiano kupitia vyuo vikuu vya Nigeria na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) hatua ambayo itasaidia kubadilishana uzoefu na utaalamu katika ngazi ya vyuo vikuu.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar ni visiwa ambavyo vimezungukwa na bahari sambamba na kuwa na rasilimali za bahari wakiwemo samaki wanaopendwa duniani aina ya jodari, hivyo inawakaribisha wawekezaji wa Nigeria kuja kuekeza Zanzibar katika sekta ya viwanda vya samaki.

Alisisitiza kuwa kwa vile tayari waekezaji wa nchi hiyo akiwemo muekezaji aliyeekeza kiwanda cha saruji katika maeneo ya Kusini mwa Tanzania hivyo, ni vyema Ubalozi huo ukaitangaza Zanzibar kwa waekezaji wa nchi hiyo ili waje kuekeza katika sekta  nyengine vikiwemo viwanda vya uvuvi.

Aliongeza kuwa tayari kuundwa kwa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo makamo makuu yake yapo hapa Zanzibar maeneo ya Fumba, ni jitihada za makusudi za Tanzania katika kuhakikisha uvuvi wa bahari kuu unaimarishwa.

Dk. Shein pia, alisisitiza haja ya mashirikiano katika sekta ya sanaa na utamaduni kati ya Zanzibar na Nigeria hasa ikizingatiwa kuwa tayari nchi hiyo imepiga hatua katika sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kujiimarisha katika masuala ya filamu na maigizo kupitia kiwanda cha uigizaji filamu cha nchi hiyo Nollywood ili Zanzibar nayo iweze kuwa na kiwanda kama hicho.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja ya kuwepo mashirikaino kwa wananchi na wa pande mbili hizo kutembeleana kwa lengo la kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo sambamba na kuiimarisha sekta ya utalii kati ya Zanzibar na Nigeria huku akipongeza hatua za kuendelea kuimarika kwa uchumi wa Nigeria.

Nae Balozi mpya wa Nigeria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Sahabi Isa Gada alimueleza Rais Dk. Shein kuwa uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo si mpya bali ni wa muda mrefu hivyo aliahidi kuwa nchi yake itauimarisha.

Dk. Gada alimueleza Rais Dk. Shein kuwa walimu 16 wa Sekondari wa Sayansi wanatarajiwa kuwasili nchini hapo kesho wakitoa Nigeria ikiwa ni hatua moja wapo ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na nchi hiyo.

Aidha, Balozi huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa na Ubalozi wake katika kuhakikisha idadi hiyo ya walimu inaongezeka ili kutoa nafasi nzuri ya kuimarika kwa sekta ya elimu hapa Zanzibar.

Sambamba na hayo, Balozi Gada alimueleza Rais Dk. Shein kuwa suala zima la kuwakarisha waekezaji kuja kuekeza Zanzibar atalifanyia kazi kwa kutambua kuwa wapo waekezaji wengi katika sekta hiyo nchini mwake hasa ikizingatiwa kuwa Nigeria nayo ina uzoefu katika sekta ya uvuvi.

Katika ujio wa walimu wa Sayansi kwa ajili kusomesha Skuli za Sekondari hapa Zanzibar kutoka nchini Nigeria, idadi yao mara hii ni walimu 50 na wote ni walimu wa masomo ya Fizikia na Hesabati ambapo tayari wameshafika walimu 8 na kesho wanatarajiwa kuwasili nchini walimu 16 na watakaobaki ambao jumla yao ni  26 watakuja hapo baadae, walimu hao hufundisha kwa muda wa miaka miwili miwili.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.