Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akisisitiza jambo wakati wa hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar wakati akihutubia katika ukumbi wa zamani wa baraza la wawakilishi kikwajuni Zanzibar leo.12-2-2018.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa utawala
wa sheria ndio dira katika utoaji haki na ndio utakaoiwezesha Zanzibar
kudumisha amani na utulivu iliyopo ambayo ndio msingi wa maendeleo katika sekta
zote za kiuchumi na kijamii.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko katika ukumbi wa
Baraza la zamani la Wawakilishi, Kikwajuni mjini Unguja katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Sheria Zanzibar.
Alieleza kuwa utawala
wa sheria ndio utakaoiwezesha Zanzibar kutekeleza mipango ya kuimarisha
viwanda, kukuza sekta ya utalii, kuvutia wawekezaji, kuwa na mfumo mzuri wa biashara,
kuendeleza kilimo, uvuvi na ufugaji wa kisasa pamoja na uhifadhi wa mazingira.
Aliongeza kuwa
inahitajika kuwa na sheria madhubuti katika ukusanyaji wa mapato na kurahisisha
ulipaji kodi, kuwa na mfumo imara wa utoaji huduma za afya, elimu pamoja na
maji safi na salama.
Dk. Shein alisema kuwa
Mahkama kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya sheria ina jukumu kubwa la
kuhakikisha utendaji na uendeshaji wa shughuli zao, unapelekea kuimarikamkwa
hali ya amani na utulivu, hasa kwa kutoa haki kwa kuzingatia misingi ya usawa
na kwa mujibu wa sheria zilizopo.
“Utawala wa sheria
ulio madhubuti, ni ule ambao umeelekeza nguvu kubwa zaidi katika kukinga na
kuzuwia uvunjaji wa sheria usitokezee, badala ya kujipanga katika kushughulikia
kesi na mashauri yanayojitokeza na kuwasilishwa Mahkamani”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alieleza matumaini yake kuwa Mahkama
itajitahidi kuchukua muda ulioelezwa katika sheria au chini ya hapo ili kuweza
kuwavutia wafanyabiashara kuleta mashauri na kumaliza mashauri yao mapema na
kuweza kufanya shughuli za uzalishaji.
Alieleza Mahkama kuwa
inatakiwa kushughulikia migogoro ya ardhi, pia, ni vyema kwa Mahakimu wa
Mahkama za Ardhi na Mahkama Kuu kutoa kipaumbele kwa migogoro ya ardhi iliyo
mbele yao inayohusiana na majengo ya biashara na uwekezaji, ili isichukue muda
mrefu jambo ambalo linaweza kuwakatisha tamaa wawekezaji hao.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza kuvutiwa kwake na kauli mbiu na maudhui ya maadhimisho ya
mwaka huu wa sheria inayosema “ Imarisha Utawala wa Sheria kwa Kukuza Uchumi wa
Nchi” sambamba na kueleza kuvutika kwake na juhudi za Mahkama.
Alieleza kuwa maudhui
hayo, vile vile ynakwenda sambamba na dhamira iliyoelezwa katika Ilani ya CCM
ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015-2020, kwenye Ibara ya 144, kuhusiana na suala
zima la kuimarisha Utawala Bora na Demokrasia nchini.
Pia, alieleza kuwa
Mahkama haina budi kushughulikia migogoro ya ajira kwa haraka kuruhusu
wafanyakazi waendelee na uzalishaji, na kutoa wito kwa watendaji wa kitengo
hicho na Mahkama kutoa kipaumbele kwenye migogoro hiyo.
Alisisitiza matumizi
ya TEHAMA ni muhimu sana ili kuongeza ufanisi na tija katika mfumo wa utatuzi
wa migogoro na hakuna haja kwamba hata kwa jambo dogo wananchi wafike Mahkamani
bali mambo mengine yanaweza kufanyika kwenye mtandao.
Kwa maelezo ya Dk.
Shein ni kuwa Serikali itafanya kila iwezalo kwa lengo la kuziwezesha Mahkama
ili iweze kufanya shughuli zao ipasavyo za kusikiliza na kuamua mashauri kwa
wakati na kuiimarisha miundombinu ya Mahkama katika kuyashughulikia matatizo ya
wananchi.
Dk. Shein, pia,
alirejea kauli yake aliyoitoa hivi karibuni juu ya ujenzi wa Mahkama Kuu huko
Tunguu ambayo kwa maelezo yake panapomajaaliwa amelenga kuifungua yeye mwenyewe
mnamo sherehe za Mapinduzi mnamo mwaka
2020 na kusisitiza kuwa “lazima tuwe na jengo la kisasa la Mahkama linaloendana
na hadhi ya Serikali hii”.
Nae Jaji Mkuu wa
Zanzibar, Omar Othman Makungu alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuhudhuria katika
sherehe hizo kwa mwaka wa saba hivi sasa huku akisema kuwa muhimili wa Mahkama
umekuwa ukifanya kazi vyema kwa lengo la kuimarisha Muungano.
Alisisitiza suala la
amani na umoja kuwa ni nguzo muhimu hapa nchini na ukanda mzima pamoja na dunia
kwa jumla huku akitumia fursa hiyo kueleza mafanikio yaliopatikana na Mahkama
pamoja na mikakati iliyowekwa katika kuhakikisha Mahkama inaimarika hapa
nchini.
Wananchi wanastahili
kupata nakla zao za kesi mapema, Mahkama
imedhamiria kuwa wadau wote wanapata nakla za hukumu ndani ya siku 30, ambapo
mwaka jana wamepata nakla zao kwa wakati hatua ambayo imewasaidia kupelekea
nakla zao katika Mahkama ya Rufaa kwa wakati
huku akieleza lengo lao kuwa hadi kufikia Disemba 2018 suala la
kuchelewa hukumu iwe historia.
Nae Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu kwa
niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na
Utawala Bora alisisitiza haja ya kuhakikisha haki zote za wananchi zinapatikana
na kila mmoja katika taasisi na vyombo husika ili kila mmoja atimize wajibu wake
katika kutekeleza hilo.
Mapema Rais wa Chama
cha Mawakili Zanzibar Omar Said Shaaban alisema kuwa zipo baadhi ya Taasisi au
wakuu wa Taasisi ambao kwao wao kufuata Sheria zilizowekwa wamekuwa wagumu na
matokeo yake wanazorotesha ukuaji wa uchumi.
Alisema kuwa wapo wengine hawaoni tabu hata
kuagiza kufutwa kwa vibali vya uwekezaji na kupendekeza Mwekezaji aondoshwe
nchini bila ya kufata utaratibu uliowekwa na sheria au kufanya mashauriano na
mamlaka nyengine zinahusika za kiuchumi kama vile za kodi au uwekezaji.
Alisisitiza
kuwa Zanzibar inaongozwa na Katiba lakini pia, kupitia Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania tumeridhia mikataba mbali mbali ya Kimataifa yenye kulinda Wawekezaji
na Uwekezaji. Si vyema jitihada za Serikali katika kuwaalika wawekezaji kuja
nchini zikatiwa doa na watu wachache ambao hawajui athari za matendo yao.
Katika
hafla hiyo, burdai mbali mbali zilitumbuizwa ikiwa ni pamoja na tenzi pamoja na
mchezo wa kuigiza kutoka katika Kundi la Black Root chini ya Msanii mahiri
Makombora.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment