Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein Azungumza na Viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R) Semistocles Kaijage akiwa na ujumbe aliofuatana nao walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo (katikati) Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe.Hamid M.Mahmoud
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akimsikiliza  Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R) Semistocles Kaijage (wa pili kulia) alipokuwa akiwatambulisha Viongozi aliofuatana nao  walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kwa mazungumzo na Rais (katikati) Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe.Hamid M.Mahmoud
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na  Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R) Semistocles Kaijage  alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo pamoja na ujumbe aliofuatana nao
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akifuatana na mgeni wake   Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R) Semistocles Kaijage  alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo pamoja na ujumbe aliofuatana nao
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akifurahia jambo alipokuwa akibadilishana mawazo na   Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R) Semistocles Kaijage (kushoto)wakiwepo na Viongozi wengine baada ya mazungumzo yao walipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo,[Picha na Ikulu.]  28/02/2018.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekutana na uongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kusisitiza haja ya kuendeleza umoja na mashirikiano yaliopo kati ya Tume hiyo na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ili Tanzania iendelee kupata heshima ndani na nje ya Bara la Afrika.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ikulu mjini Zanzibar ulipofika kwa ajili ya kujitambulisha ukiongozwa na Jaji Semistocles Kaijage Mwenyekiti wa Tume hiyo akifuatana na Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Hamid Mahmoud Hamid pamoja na Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani.

Katika Mazungumzo hayo, Dk. Shein aliupongeza uongozi huo kwa kuendeleza umoja na mashirikiano uliopo kati ya (NEC) na (ZEC) na kusisitiza haja ya kuendelezwa ili kuendelea kuijengea sifa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuendelea kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.

Alieleza kuwa mashirikiano ya pamoja yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza majukumu kwa Tume zote mbili hasa ikizingatiwa kuwa kila upande una uzoefu wake ambapo kwa Zanzibar masuala ya uchaguzi hasa wa vyama vingi yalianza tokea mwaka 1957 na baadae kuendelea hadi hivi leo.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza matumaini yake makubwa aliyonayo kutokana na uongozi huo wa NEC, chini ya Mwenyekiti wake Jaji Kaijage kutokana na kuanza vyema majukumu waliyopewa.

Alieleza kuvutiwa na mafanikio yaliopatikana na Tume hiyo kutokana na kutekeleza majukumu yao vyema yakiwemo ya kuhakikisha wananchi wanatumia haki yao ya msingi ya kupiga kura, wanaendesha chaguzi, wanasimamia na hatimae wanatoa matokeo kwa wakati.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa ana matumaini makubwa kuwa Mwenyekiti huyo ataendeleza vyema majukumu yake kama alivyofanya Mwenyekiti aliyekuwa kabla yake Jaji Mstaafu Damiani Lubuva ambaye muda wake wa kushika wadhifa huo umemaliza kwa kutoa mashirikiano mazuri na NEC sambamba na kutekeleza vyema majukumu yake.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa suala la Tume hiyo kuwa na Ofisi zake za kudumu hapa Zanzibar ni suala la lazima na juhudi za makusudi zitachukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha hilo linafanikiwa ili kuweza kurahishisha shughuli za Tume hiyo hapa Zanzibar na kuweza kuimarisha mashirikiano na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) hatua ambayo pia, itaweka ukaribu kati ya NEC na wadau wake hapa Zanzibar.

Aidha, Dk. Shein aliuhakikishia uongozi huo kuwa ataendelea kutoa ushirikiano wake kwa kutambua kazi na majukumu makubwa ya Tume hiyo hapa nchini.

Nae Jaji Semistocles Kaijage alitoa pongezi zake kwa Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuingoza vyema Zanzibar kutokana na ushindi mkubwa alioupata katika Uchaguzi Mkuu uliopita ambao umemuwezesha kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa kipindi cha pili.

Aidha, Jaji Kaijage alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kutokana na mashirikiano mazuri inayopata Tume hiyo kutoka kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar sambamba na kuimarika kwa mashirikiano kati ya Tume hiyo na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Jaji Kaijage alimueleza Dk. Shein majukumu ya Tume hiyo pamoja na juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Tume hiyo katika kuhakikisha inatekeleza vyema majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuendesha Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani kwa upande wa Tanzania Bara.

Aliongeza kuwa ili jukumu hilo lifanyike kwa ufanisi wananchi waliotimiza vigezo vya kupiga kura na wale wanaotarajia kupiga kura miaka ijayo lazima wapate elimu sahihi ya Mpiga Kura jambo ambalo wamekuwa wakilitekeleza kwa nguvu zao zote katika kuhakikisha elimu hiyo inatolewa na Tume hiyo.

Aliongeza kuwa katika kupanua wigo wa utoaji wa elimu ya Mpiga Kura kwa wananchi wengi zaidi (NEC) imekuwa ikishiriki katika mikutano mbali mbali ya viongozi ili kutoa elimu hiyo, wameshakutana na wadau wao wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa Tanzania Bara na Zanzibar, kutoa elimu kupitia vyombo vya habari, uimarishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura pamoja na kutoa elimu ya Mpiga Kura kwa skuli za Sekondari katika baadhi ya Mikoa ya Tanzania Bara.

Sambamba na hayo, Jaji Kaijage alimueleza Rais Dk. Shein kuwa tayari Tume anayoiongoza imeshasimamia chaguzi sita za Ubunge ukiwemo uchaguzi wa Jimbo la Dimani hapa Zanzibar  na chaguzi nyengine tano za Ubunge na Chaguzi 79 za Madiwani huko Tanzania Bara.

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) alimueleza Rais Dk. Shein juhudi zinazoendelea kufanyika za kujenga jengo jipya la Ofisi za Tume hiyo huko Dodoma na kusisitiza haja ya kuwa na Ofisi zao za kudumu hapa Zanzibar na kufurahishwa na azma ya Rais Dk. Shein ya kuhakikisha hilo linafanikiwa katika kipindi kifupi kijacho kama ilivyo kwa Ofisi nyengine za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo tayari zina Ofisi zao hapa Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.