Na:
Veronica Kazimoto. Arusha
Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) imekamata na kutaifisha bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na tani moja ya
sukari na chumvi, majani ya chai mifuko 18, mirungi kilogramu 16, vifaranga vya
kuku 5000 na mayai kasha 416 katika mpaka wa Namanga mkoani Arusha zikitokea nchini
Kenya kupitia njia zisizo rasmi.
Akizungumza mara baada ya
kukamata bidhaa hizo, Meneja Msaidizi wa Forodha mkoani hapo Edwin Iwato alisema
bidhaa hizo ni mali ya Joseph Sekino, Innocent Minja na Andrew Lyimo wote
wakiwa ni wafanyabiashara kutokea Tanzania na watachukuliwa hatua kwa mujibu wa
Sheria.
"Tumewakamata
wafanyabiashara watatu ambao ni Joseph Sekino akiwa amepakia tani moja ya sukari
na chumvi na majani ya chai mifuko 18 kwenye gari Na. T 785 AWV, Innocent Minja akiwa na mayai kasha 416 na mirungi kilo
16 kwenye gari Na. T 443 CQU na Andrew Lymo akiwa na vifaranga vya kuku 5000
kwenye gari Na. T 441 DHW wote wakitokea nchini Kenya kuja mkoani Arusha,"
alisema Iwato.
Iwato alieleza kwamba, wafanyabiashara hao waliingiza baadhi
ya bidhaa hizo kwa kutumia vifungashio vya bidhaa nyingine za nchini Tanzania
ili kuficha uhalisia wake huku wakiwa hawana vibali wala kulipa ushuru wa Serikali
kama inavyotakiwa.
Alifafanua kuwa, mirungi
ilikamatwa ndani ya mifuko ya plastiki maarufu kama Rambo ikiwa imefichwa
kwenye boneti ya mbele ya gari aina Noah Na. T 443 CQU sehemu ya injini.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma
na Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Richard Kayombo alisema, tabia ya
wafanyabiashara hao siyo tu inawahujumu wafanyabiashara wenzao bali inakwamisha
azma ya Serikali ya kukusanya mapato kwa ajili ya maendeleo ya kila mwananchi.
"Tabia ya
wafanyabiashara hawa siyo nzuri kwa kuwa inakwamisha ukusanyaji mapato ya
Serikali na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ili iwe fundisho kwa
wengine wanaofikiria kufanya biashara pasipo kutumia njia rasmi na kulipa
ushuru ipasavyo", alisema Kayombo.
Aidha, Kayombo aliongeza
kuwa, bidhaa zote haramu zilizokamatwa zitateketezwa kwa mujibu wa Sheria, zile
zinazofaa kwa matumizi ya binadamu zitagawiwa kwa taasisi mbalimbali za
Serikali zenye uhitaji kwa mujibu na taratibu zilizowekwa na TRA na magari yote
yaliyotumika kusafirisha bidhaa hizo yametaifishwa na Mamlaka ya Mapato
Tanzania.
Utaifishaji wa magari na
bidhaa ambao usafirishaji wake haufuati sheria na taratibu, unalenga kukomesha
shughuli za magendo nchini ambazo kwa kiasi kikubwa zinakwamisha juhudi za
Serikali katika ukusanyaji wa mapato.
No comments:
Post a Comment