Habari za Punde

Wananchi 177 Ngomeni wajengewa barabara yao kwa kiwango cha lami

 MHANDISI ujenzi wa barabara kutoka wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Khamis Massoud, akionesha hatua ya uwekaji wa lami baridi ulipofikia, kwenye ujenzi wa barabara ya Kuyuni-Ngomeni wilaya ya Chake chake, ikiwa ni agizo maalum la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Mhe: Dk Ali Mohamed Shein, (Picha na Haji Nassor).
 ENEO la barabara ya Kuyuni –Ngomeni yenye urefu wa kilomita 5.5, ambapo tayari kilomita 1.3 zimeshatiwa lami, na kilomita 2.2 zilizobakia, zikitarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Machi kumalizika, ambapo ujenzi wa barabara hiyo ni agizo la rais wa Zanzibar,

 Picha na Haji Nassor-Pemba.


 NA HAJI NASSOR, PEMBA.

WASTANI wa wananchi 177 wa kijiji cha Ngomeni shehia ya Mgelema wilaya ya Chakechake Pemba, wanaendelea kutengenezewa barabara yao kwa kiwango cha lami, ikiwa ni agizo maalumu la rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Mhe: Dk Ali Mohamed Shein.

Wananchi hao awali, walitoa kilio chao cha ukosefu wa barabara ya kisasa, mbele ya rais wa Zanzibar wakati alipowatembelea mwaka jana, ndipo alipoitaka wizara husika, kuhakikisha wanaitengeneza ili iweze kupitika kipindi chote.

Baada ya wizara kukamilisha hatua hiyo, wananchi hao walimuomba tena rais huyo wa Zanzibar, sasa kuwajengewa kwa kiwango cha lami, ambapo tayari ujenzi huo umeshaanza na kabla ya kumalizika kwa mwezi Machi mwaka huu, itakuwa imeshakamilika.

 Ujenzi huo unaofanywa na Wizara ya Ujenzi, Miundombinu na Usafirishaji Zanzibar, kwa kiwango cha lami, umaenza miezi mitatu iliopita, na unatarajiwa kukamilika wakati wowote kabla ya mwisho wa mwezi ujao.

Mhandisi ujenzi wa wizara hiyo, Khamis Massoud, alisema hatua ya utiaji wa lami baridi ulishakamika tokea Febuari 16, ndipo hatua ya uwekaji wa lami moto ulipoanza mapema siku tatu baadae, na wanaendelea kwa kasi.

Alisema kama mashine yao moja ilioharibika juzi wa mafundi wataiweza, basi hatua ya kumalizia kilomita 2.2 ziliobakia kwa utiaji wa lami moto, utakamilika sio chini ya wiki tatu zijazo.

Alisema kwa sasa tayari kilomita 1.3 zimeshakamilika kwa utiaji wa lami, na sasa wanajipanga ili kuweka alama za barabarani na baada ya kuimaliza yote kilomita 5.5 wataikabidhi serikalini, kwa hatua za ufunguzi.

“Kwa sasa kazi ya uwekaji lami baridi tumeshakamilisha, na kazi inayoendelea kwa kasi kubwa ni umaliziaji wa uwekaji wa lami moto, na naamini kabla kumalizika mwezi ujao, na sisi tutakuwa tumeshamaliza kazi,”alisema Mhandisi huyo.

Wakati huo huo Mhandisi huyo, alisema wakikamilisha kazi hiyo, watakwenda kwenye barabara ya Kangani- Mkanyageni yenye urefu wa kilomita 5, kwa kufanya matengenezo ya madogo ya kifusi, na kisha uwekaji wa lami.

Sheha wa shehia ya Mgelema Omar Idd Zaina, alisema kwa sasa wananchi wake pamoja na yeye mwenyewe, wamefurahishwa kuona rais analoliahidi analitekeleza kwa wakati.

“Sisi kwa kijiji cha Ngomeni tuko sawa kama wa mjini Chakechake, maana maji yapo, umeme safi, barabara tayari na hospitali keshokutwa,”alisema sheha huyo.

Nae mwananchi Asha Muhsin, alisema sasa hawatakuwa tena na shida, wanapotaka kwenda mjini kwa ajili ya shughuli zao mbali mbali.

“Ilikuwa ukitaka kwenda mjini hasa siku za mvua, kwanza ujipange vyema maana kwanza hakuna hata gari ya abiria, lakini sasa karibu tutapata hata usafiri wa umma,”alisema.

  Mshauri wa rais Pemba Mauwa Abeid Daftari, alisema usafiri wa barabarani 
duniani kote, ndio kifaa pekee cha kuwafikishia maendeleo wananchi.

“Mimi kwanza nimshukuru sana rais wetu, kwa kuamua kutekeleza ahadi zake kwa wananchi hawa, na huku ndio kutelekeza Ilani ya CCM kwa vitendo,”alisema.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 5.5, kwenye miaka ya 75 ilikuwa ikitumiwa na waenda kwa miguu, kabla ya kuanza kuwa kwa ajili ya gari za Ng’ombe na Punda ambapo 14 baadae , ilianzishwa na wakulima wa karafuu na sasa mwaka 2018 in ya kiwango cha lami.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.