Habari za Punde

Wasimamizi wa sheria waagizwa kuacha utashi na kuweka uzalendo mbele wanapotekeleza majukumu yao

Na Miza Kona, Maelezo 
 Wasimamizi wa sheria wa Ulinzi na Usalama wametakiwa kuacha utashi na kuwa wazalendo katika kutekeleza majukumu yao.
Wametakiwa wawe waadlilifu katika ngazi zote ili kuweza kudhibiti uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya nchini.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar Bi Kheriyangu Mgeni Khamis katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkokotoni.
Kikao hicho kiliitishwa na  kujadili namna ya kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya katika mkoa huo.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa, kuna baadhi ya wasimamizi wa sheria hawatekelezi vyema majukumu yao na kupelekea kufutwa kwa baadhi ya kesi na hivyo kurudisha nyuma juhudi za serikali za kutokomeza dawa hizo.
Alieleza kuwa wasimamizi wa sheria wakiwa makini na waadilifu pamoja na kushirikiana na jamii, wanaweza kufanya kazi bila ya migogoro na kuwafichua wahalifu wanaofanya biashara haramu ya dawa za kulevya katika mkoa huo.
Bi Kheriyangu amesema Mkoa wa Kaskazini umekuwa ukiongoza kwa kesi za dawa za kulevya kutokana na wimbi kubwa la uingizaji na utumiaji wa dawa hizo.
Kwa hivyo alisema ni vyema kuzisimamia ipasavyo sheria ili kuweza kuzuia na kudhibiti uhalifu huo usiingie nchini na kuinusuru na nguvu ya taifa isiathirike na matumizi ya dawa za kulevya.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa Tume imejipanga kuimarisha mfumo madhubuti utakaoweza kudhibiti uingizaji wa dawa za kulevya ili jamii iweze kunusurika na janga hilo.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Vuai Mwinyi Mohammed, ametaka kubadilishwa kwa sera na sheria zilizopo ili ziendane na mazingira yaliyopo, pamoja na kuondoa muhali ili kudhibiti tatizo hilo nchini.
Wakichangia majadiliano hayo, washiriki wa kikao hicho wameitaka Tume ya Taifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za kulevya kuweka maofisa katika ofisi za mikoa watakaoweza kuratibu na kushughulikia suala hilo.
Aidha wametaka hatua kali na za haraka zichukuliwa kwa wanaobainika kujihusisha na biashara hiyo ili kuepukana na usumbufu katika ufuatiliaji wa kesi hizo wanaoupata wasimamizi wa sheria.
Aidha wamesema ukosefu wa  vifaa vya kisasa unapelekea kukosa taarifa za haraka na hivyo kusababisha kuongezeka kwa uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya katika mkoa huo.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.