Habari za Punde

Balozi Seif akutana na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya VAULT Tawi la Tanzania

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mAli Iddi kushoto akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya VAULT Tawi la Tanzania Bwana Said Ali Said walipofika Ofisini kwake Vuga kumueleza nia yao ya kutaka Kuwekeza kwenye Ukanda wa Maeneo huru ya Kiuchumi Micheweni Kisiwani Pemba.Kati kati yao ni Mwakilishi wa Kampuni hiyo kutoka Mjini Washington Nchini Marekani Bwana Hirsi Dirir.
Balozi Seif  akizungumza na Ujumbe wa Viongozi Wawili wa Kampuni ya Kimataifa ya VAULT uliofika Ofisini kwake Vuga kumueleza nia yao ua kutaka Kuwekeza kwenye Ukanda wa Maeneo huru ya Kiuchumi Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR
Ukanda wa maeneo huru ya Kiuchumi uliopo Micheweni Mkoa wa Kaskazini  Pemba umeanza kutoa cheche ya matumaini katika sekta ya Uwekezaji kufuatia Kampuni ya Kimataifa ya VAULT yenye Makao Makuu yake Washington Marekani kuonyesha nia ya kutaka kuweka Miradi ya Kiuchumi katika Ukanda huo.
Micheweni ni eneo la Pili Maalum lililotengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya Uwekezaji likitanguliwa na lile la Ukanda wa eneo la Fumba ambalo tayari limeanza harakati za Uwekezaji  wa Miradi ya Kiuchumi.
Akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya VAULT Tawi la Tanzania Bwana Said Ali Said alisema Uongozi wa Kampuni hiyo umefikia uamuzi wa kutaka kuwekeza katika Ukanda wa Micheweni kutokana na maumbile mazuri ya Hifadhi ya Misitu pamoja na Fukwe za kuvutia watalii.
Bwana Said alisema ziara ya Ujumbe wa Viongozi wa  VAULT Visiwani Zanzibar imeliona eneo hilo la Micheweni ambalo bado liko nyuma Kiuchumi wakati limebarikiwa kuwa na Rasilmali nyingi zisizotumika Kiuchumi kwa Maendeleo ya Wananchi wa Ukanda huo.
Alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba VAULT iko tayari kuanza miradi yake wakati wowote  kuanzia sasa iwapo itapata fursa hiyo ikilenga zaidi hapo baadae kujenga Hoteli yenye Hadhi ya Nyota Tano pamoja na  Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano.
Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya VAULT alieleza kwamba tayari wameshakutana kwa mazungumzo na Uongozi wa Wilaya ya Micheweni, Wananchi wa Maeneo husika pamoja na Mkoa wa Kaskazini Pemba katika azma yao ya kutaka kushirikiana na wadau hao kwenye nia yao hiyo ya Uwekezaji.
Alifahamisha kwamba katika hatua za awali za miradi yao VAULT imepanga kutoa ajira zaidi ya wananchi 300 wazalendo wa maeneo ya Ukanda wa Micheweni katika lengo la kuwa karibu na Wananchi hao.
Bwana Said alisisitiza kwamba katika kuimarisha maisha na kipato cha Wananchi hao wa Ukanda wa Micheweni Pemba Wataalamu wa Kampuni ya VAULT wamejipanga kutoa Taaluma  kwa Wananchi katika Sekta ya Kilimo, Ufugaji pamoja na Uvuvi.
“ Jamii ya Wananchi wa Ukanda wa Micheweni itawezeshwa kupata Miradi ya Kijamii katika Sekta ya Ufugaji, Kilimo na Uvuvi ili ijitegemee Kiuchumi”. Alisema Mkurugenzi Mkuu huto wa VAULT Tawi la Tanzania.
Alisema hatua hiyo itawawezesha Wananchi hao kujiajiri wenyewe katika miradi ya ujasiri Amali kupitia Vikundi vya Ushirika  au hata Mtu mmoja mmoja ili wafikie pahali pa kuweza kujikimu Kimaisha kwa kuondoa Umaskini na kuongeza Kipato chao cha kila siku.
Naye Mwakilishi wa Kampuni hiyo kutoka Washington Nchini Marekani Bwana Hirsi Dirir alisema Taasisi za Uwekezaji pamoja na zile za miradi ya Kijamii Nchini Marekani zimelenga kusaidia wananchi wenye kipato cha chini katika Mataifa mbali mbali  Duniani.
Bwana Hirsi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mkazo zaidi wa misaada na Miradi hiyo imeelekezwa zaidi katika Bara la Afrika lenye Nchi nyingi zilizokuwa chini Kitaaluma na hata Kiuchumi.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali imefarajika na muelekeo wa uwekezaji huo katika Ukanda wa Micheweni ambao ni jambo zuri kwa vile litasaidia kutoa ajira kwa Vijana wa Visiwa hivi.
Balozi Seif alisema Ukanda wa Micheweni umechelewa kuanza kutoka huduma iliyokusudiwa ya uwekezaji wa Miradi ya Kiuchumi kutokana na sababu za msingi za ukosefu wa Miundombinu ya Mawasiliano ya Bara bara, Huduma za Umeme pamoja na Maji.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameushukuru na kuupongeza Uongozi wa Kampuni ya VAULT kwa uamuzi wake wa kutaka kuwekeza kwenye  Ukanda wa Micheweni na kuushauri kuangalia uwezekano wa kuipa kipaumbele Miradi ya Uvuvi kwa Vile Visiwa vya Zanzibar vimezunguukwa na Bahari sehemu zote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.