Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Awaapisha Mawaziri Aliowateuwa Jana.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akimuapisha Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amani Salum Ali, Hafla hiyo imefanyika leo Ikulu Zanzibar. 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  leo amewaapisha viongozi aliowateua hapo jana kushika nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hafla hiyo, ilifanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ambapo viongozi walioapishwa ni Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salim Ali, Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Abeid Karume, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Dk. Sira Ubwa Mamboya.
Wengine ni Waziri wa Afya, Hamad Rashid Mohamed, Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Rashid Ali Juma, Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Salama Aboud Talib, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale  Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto  Maudline Cyrus Castico,
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Juma Makungu Juma, Naibu Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Choum Kombo Khamis, Naibu Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Shadia Mohamed Suleiman, Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Dk. Makame Ali Ussi, Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda Hassan Khamis Hafidh.
Pia, Dk. Shein aliwaapisha Wakuu wa Wilaya aliowateua hapo jana ambao ni  Issa Juma Ali alieapishwa kuwa  Mkuu wa Wilaya ya Mkoani, Pemba na  Rajab Ali Rajab alieapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B, Unguja.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar  Omar Othman Makungu, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Mawaziri, Manaibu Mawaziri na Wakuu wa Mikoa.

Wengine waliohudhuria ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih,Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Wakuu wa Vikosi vya SMZ, Washauri wa Rais wa Zanzibar pamoja na viongozi wengine wa Serikali.

Nao viongozi hao walioapishwa waliahidi kuendelea kumsaidia Rais Dk. Shein katika kuhakikisha Zanzibar inazidi kupata maendeleo, waliahidi kuimarisha mashirikiano ya dhati katika kuwatumikia wananchi, kuleta mabadiliko na kufanya kazi kwa vitendo sambamba na kuendelea kusimamia amani na utulivu uliopo nchini.

Hapo jana, Dk. Shein alifanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mapinduzi kwa kuongeza Wizara moja zaidi na kuwabadilisha Wizara baadhi ya Mawaziri.

Kufuatia mabadiliko hayo, shughuli za Vijana zimehamishiwa katika Wizara mpya ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo shughuli za Mazingira zimehamishiwa katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na shughuli za Wakala wa Serikali wa Uchapaji zimehamishiwa Wizara mpya ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale.

Aidha, amewateua Naibu Mawaziri wapya wawili na kumbadilisha Wizara Naibu Waziri mmoja ambapo kufuatia mabadiliko hayo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa itakuwa na Wizara 14.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.ukNo comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.