Na. Abdi Shamna Zanzibar.
MKUTANO wa Wadau wa Usafiri wa Anga Afrika, unatarajiwa kufanyika
hapa Zanzibar April 8, mwaka huu, ambapo
pamoja na mambo mengine utajadili suala la uimarishaji wa biashara ya safari za
ndege pamoja na Usalama wa safari za Anga.
Mkutano huo wa siku mbili utahusisha washiriki zaidi ya 400,
ikiwemo watengenezaji wa ndege, watoa huduma za ndege (booking, vyakula,mifumo
ya viwanja vya ndege) na wamiliki wa mashirika ya ndege.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Zanzibar
Beach Resort, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mashirika ya Ndege Afrika (AFRAA),
Abderahmane Berthe, alisema watendaji kutoka mashirika ya Ndege ya Afrika, yapatayo 40
watashiriki mkutano huo.
Alisema AFRAA imefikia
uamuzi wa kuiteuwa Zanzibar kuwa mwenyeji wa mkutano huo, kwa kigezo kuwa ni
kitovu cha utalii, hivyo hatua hiyo itatowa fursa ya kuendeleza sekta hiyo.
Alisema suala la biashara ya safari za Anga litachukuwa
nafasi kubwa, ili kuona sekta hiyo inaimarika, ikiwemo wadau (watengenezaji wa
ndege) kupata nafsi ya kubainisha ubora wa ndege wanazotengeneza ili kuvutia mashirika
kwa ajili ya ununuzi.
Aidha, alisema kwa kuzingatia umuhimu wa sekta ya utalii ya kuhitaji
usafiri wa uhakika, suala la usalama wa safari za ndege nalo litapewa
kipaumbele.
“Zanzibar ni moja ya nchi za utalii, iwapo suala la usalama
wa safari za anga halitapewa kipaumbele, ni dhahiri kuwa watalii hawatakuwa na
uhakika wa safari zao, watalii wengi wanaokuja hapa huinga nchini kupitia njia za anga”, alisema.
Vile vile alisema, mkutano huo utatowa fursa kwa mashirika
madogo ya ndege kukutana na wadau wengine na kuongeza ushirikiano katika nyanja
hiyo na kuimarisha mashirika yao.
Nae, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (Air
Tanzania) Ladislaus Matindi, alisema AFRAA imeamuwa mkutano huo kufanyika hapa
Zanzibar, ikiwa ni moja ya hatua ya
kuona ‘Air Tanzania’ inaimarika na kurejea katika hadhi yake.
Alisema katika kuhakikisha Shirika hilo linajiimarisha, limeandaa
miakati inayolenga liweze kumiliki ndege 12 za aina tofauti hadi ifikapo mwaka 2022.
“Kwa kuwa mkutano huu utawashirikisha wadau mbali mbali, pia tutapata fursa ya kuwasikiliza
watengenezaji wa ndege, hii ni fursa ya kuangalia maeneo mengine zaidi, wapi
tunaweza kupata ndege bora zaidi, tuna
mikakati ya kuwa ndeeg nyingi zaidi”, alisema.
Alisema kwa sasa Shirika hilo linaendelea na utaratibu wa
kukamilisha ununuzi wa ndege nne aina Bombadier, pamoja na azma ya kununua ndege moja aina ya Boieng.
Mapema, Naibu Waziri, Wizara ya Mawasiliano na Usafirishaji
Zanzibar, Mohammed Ahmada, alisema
mkutano huo wa siku mbili, utasaidia sana kuitangaza Zanzibar kiutalii
na kibiashara.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na
juhudi za kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, ikiwemo kukmailisha ujenzi wa Termina 11, ili kuweka mazingira
bora ya ujio wa watalii na kufikia lengo la kupokea watalii 500,000 ifikapo
2020.
Alisema Serikali kwa
kushirikiana na AFRAA, Kamisheni ya Utalii Zanzibar na ATCL inaendelea na
maandalizi ya mkutano huo unaotarajiwa kufana vyema.
Katika hatau nyengine, Katibu Mtendaji Kamisheni ya Utalii
Zanzibar, Dk. Vuia Lilla, alisema ujio wa mkutano huo, utatowa fursa adhimu ya
kibiashara kwa wadau wa utalii nchini, ikiwemo wamiliki wa hoteli,watembeza
watalii, sambamba na wageni kupata fursa ya kutembelea maeneo tofauti ya kihistoria
na kuona vivutio vya talii.
No comments:
Post a Comment