Habari za Punde

Rais Dk Shein afungua Mkutano wa Saba wa Mashirika ya Ndege ya Afrika {AFRAA}

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiyatembelea maonyesho ya kazi mbali mbali zinazofanywa na Mashirika ya Ndege Barani Afrika kabla ya Kuufungua Mkutano wa Mashirika hayo unaofanyika huko Zanzibar Beach Resort Mazizini
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiyatembelea maonyesho ya kazi mbali mbali zinazofanywa na Mashirika ya Ndege Barani Afrika kabla ya Kuufungua Mkutano wa Mashirika hayo unaofanyika huko Zanzibar Beach Resort Mazizini

 Balozi Seif  akipata maelezo katika Banda la Shirika la Ndege Tanzania {ATCL } Zanzibar Beach Resort Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
  Katibu Mkuu wa Mashirika ya Ndege ya Afrika {AFRAA} Bwana Abdelrahmane  Berthe akitoa Taarifa ya Taasisi yake kabla ya kufunguliwa kwa Mkutano wao.
  Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Dr. Sira Ubwa Maboya akiwakaribisha Wajumbe wa Mkutano wa Saba wa Mashirika ya Ndege ya Afrika kabla ya kufunguliwa na Balozi Seif kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Shein.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa Saba wa Mashirika ya Ndege ya Afrika kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein hapo Zanzibar Beach Resort Mazizini.
Balozi Seif akiagana na Makamu wa Rais wa Mashirika ya Ndege ya Afrika {AFRAA} Bwana Raphael Kuuchi baada ya kuufungua Mkutano wa Mashirika hayo Zanzibar Beach Resort Mazizini.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis, OMPR
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein ameyaagiza Mashirika ya Ndege Barani Afrika {AFRAA} lazima yaendelee kushikamana  katika kuimarisha huduma za Ufafiri wa Anga kwa lengo la kuifanya  Sekta ya Utalii Barani humo kukua zaidi.
Alisema tabia ya kuendelea kuyaachia Mashirika ya Kigeni kutoa huduma kwa Makampuni yanayosafirisha Watalii katika Mataifa ya Afrika  inaweza kuviza azma ya Afrika katika kuitegemea Sekta hiyo Kiuchumi.
Rais wa Zanzibar alitoa Kauli hiyo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiufungua Mkutano wa Saba wa Siku Tatu wa Mashirika ya Ndege ya Afrika {AFRAA} unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Zanzibar Beach Resort Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema Usafiri wa Anga na Utalii ni Sekta muhimu Kimataifa zinazokuwa kwa haraka Kiuchumi na kwenda sambamba katika uendeshaji wake jambo ambalo Mataifa ya Bara la Afrika kupitia Taasisi inayosimamia Mashirika ya Ndege ya Afrika {AFRAA} hayana budi kuhakikisha Sekta hizo zinaendelea kujengewa Miundombinu madhubuti.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dr. Shein alisema Baraza la Usafiri na Utalii Ulimwenguni limetoa Ripoti za Takwimu zinazoonyesha na kuthibitisha kujimarika Kiuchumi kwa sekta hizo mbili katika kipindi cha Mwaka 2018.
Alisema harakati za Usafiri wa Anga zinazowaunganisha Watalii wanaotembelea maeneo mbali mbali Duniani  zinatarajiwa kuongeza Mapato ya Nchi husika sambamba na fursa za Ajira  kwa zaidi ya Milioni 400,000,000/-.
Dr. Ali Moh’d Shein alivitolea mfano Visiwa vya Zanzibar vilivyopiga hatua kubwa Kimaendeleo na Uchumi katika Sekta ya Utali kutokana na kuimarika kwa huduma za usafiri wa anga zinazowaunganisha Watalii kutoka pambe mbali mbali Duniani.
Rais wa Zanzibar aliwaeleza wajumbe hao wa Mkutano wa Saba wa Mashirika ya Ndege ya Afrika {AFRAA} kwamba idadi ya Watalii walioingia Zanzibar imefikia  Laki 433,166 kwa Mwaka 2017 ikilinganishwa na idadi ya Watalii  Laki 479,242  kwa Mwaka 2016.
Dr. Shein alifahamisha kwamba wakati Idadi ya Watalii  wanaoingia Zanzibar ikiongezeka na kufikia asilimia 14.2%  ongezeko hilo linatarajiwa kufikia  Watalii Laki 500,000 ifikapo Mwaka 2020.
“ Nimefarajika sana kutokana na Uamuzi wa Mashirika ya Ndege ya Afrika {AFRAA} kufanya Mkutano wao Zanzibar jambo ambalo Visiwa vya Zanzibar vitapata fursa ya kujitangaza Kiutalii kupitia Mkutano huo”. Alisema Dr. Shein.
Alieleza kuwa juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinakusudia kuvifanya Visiwa vya Zanzibar  kuwa na hadhi ya juu katika uimarishaji wa Sekta ya Utalii kwenye Ukanda wa Bahari ya Hindi.
Dr. Shein alisema Miundombinu inayoendelea kuwekwa katika ujenzi wa Maegesho ya Ndege za Kimataifa sambamba na Jengo la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume ni uthibitisho wa juhudi hizo za Serikali.
Rais wa Zanzibar aliyashauri na kuyakumbusha Mashirika ya Ndege Barani Afrika  kuongeza juhudi za kuziongezea safari za nje ya Bara hilo ili Watalii wanaopanga kufanya safari za ndege ndani ya Mataifa ya Bara hili yatumie ndege zao jambo ambalo litachangia kuongeza Mapato.
Akitoa Taarifa Katibu Mkuu wa Mashirika ya Ndege ya Afrika {AFRAA} Bwana Abdelrahmane Berthe alisema muingiliano wa uwajibikaji wa Mashirika ya Usafiri wa Anga Afrika katika kutoa huduma zao lazima yaoane ili kuleta tija kwa maeneo yote ya Dunia.
Bwana Abdelrahmane  alisema soko la Utalii linalotarajiwa kuchukuwa nafasi ya kwanza kwa mapato ya Uchumi Ulimwenguni badala ya Mafuta na Gesi asilia bado halijafikia lengo.
Alieleza kwamba hali hiyo inatokana na baadhi ya Maeneo yenye rasilmali za asili kwa biashara ya Utalii kutofikiwa na huduma za Usafiri wa Anga kwa kukosekana kwa miundombinu ya Sekta hiyo.
Alifahamisha kwamba mikakati zaidi inahitajika kuwekwa hasa katika Mataifa wanachama wa AFRAA katika kuona Nchi hizo hazitawekwa nyuma kwenye Biashara ya Utalii Duniani.
Naye Makamu wa Rais wa  Mashirika ya Ndege ya Afrika Bw. Raphael Kuuchi alisema Takwimu zinaonyesha kwamba zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 72 zinakusanya  kila Mwaka kutoka na Biashara ya Sekta ya Usafiri wa Anga Barani Afrika.
Bwana Kuuchi alisema kiwango hicho kimekuja kutokana na ongezeko kubwa la Idadi ya Watalii wanaoingia na kutoka Barani Afrika.
Mkutano wa Sita wa Mashirika ya Ndege ya Afrika  ulifanyika Mwezi Mei Mwaka 2017 katika Mji wa Hammamet Nchini Tunisia ukiwa chini ya Ushirikiano na Shirika la Ndege la Nchi hiyo Tunisair.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.