Habari za Punde

LEO NI SIKU YA TATU YA KAMPUNI YA ASAS DAIRIES KUGAWA MAZIWA KWA WANAFUNZI IRINGA

NA FREDY MGUNDA,IRINGA.

Leo ni siku ya tatu kwa kampuni ya maziwa ya Asas Dairies Ltd toka imetenga pakiti 120,000 za maziwa yenye thamani ya Sh Milioni 60 zilizoanza kugaiwa bure kwa wanafunzi zaidi ya 30,000 wa shule za msingi za serikali na binafsi za mjini Iringa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho yake ya wiki ya maziwa.

Kampeni ya kugawa maziwa hayo  ilizinduliwa juzi katika shule za manispaa ya Iringa huku Mratibu wa maziwa wa kampuni hiyo, Lipita Mtimila akisema hatua hiyo ni muendelezo wa mikakati yao ya kudumu inayolenga kuhamasisha jamii ya wana Iringa kuongeza kiwango cha unywaji maziwa kutoka chini ya asilimia 10 za sasa hadi asilimia 40.
Alisema takwimu za sasa zinaonesha kiwango cha maziwa yanayouzwa kwa siku katika mji huo kinakadiriwa kuwa lita 3,500 ambazo kati yake lita 1,500 ni zile zilizosindikwa na lita 2,000 zinazouzwa kwa walaji bila kusindikwa.

“Tunawahimza wadau wote wa maziwa kushirikiana na kampuni yetu ya maziwa ya Asas kuhamasisha unywaji wa maziwa, sio mjini Iringa pekee lakini pia na maeneo mengine yote nchini,” alisema.

Wakiipongeza kampuni hiyo na kampeni yake ya unywaji maziwa mjini Iringa baadhi ya walimu walisema maziwa ni chakula ambacho kama kitatumiwa kama inavyoshauriwa mchango wake ni mkubwa katika kutokomeza magonjwa yanayotokana na ukosefu wa lishe bora ukiwemo utapiamlo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mshikamano,  Haiba Roy alisema ipo haja ya kuanzisha kampeni ya unywaji wa maziwa mashuleni kila siku, mpango utakaowasaidia kiafya wanafunzi wengi wakiwemo wale wanaokwenda shule wakiwa hawajapata mlo wowote toka majumbani mwao.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mtwivilla, Frolian Kilumile aliipongeza kampeni ya kampuni hiyo akisema inasaidia kuwakumbusha wazazi kuwa na utamaduni wa kununua maziwa kwa kuzingatia mahitaji ya watoto.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hizo walisema wengi wao hawajawahi kunywa maziwa wakiwa majumbani mwao na hawaelewi sababu za kukosa kinywaji hicho chenye ladha nzuri na kinachoelezwa kuwa na faida nyingi kwa ukuaji wa mwili na akili zao.

Mmoja wa wanafunzi hao, Thobias Mlanzi alisema amekunywa mara kadhaa maziwa kupitia kampeni ya kampuni hiyo na anaona haja ya kuwashawishi wazazi wake aliosema wana uwezo wa kumudu gharama kumtengea Sh 500 kila siku kwa ajili ya maziwa hata kama wao hawana mapenzi na kinywaji hicho.

Akizungumzia mipango ya kusogeza zaidi huduma ya maziwa karibu na mlaji, Mtimila alisema mbali na kupatikana katika maduka mbalimbali mjini Iringa na maeneo mengi nchini, wako mbioni kutumia teknolojia mpya ya uuzaji wa bidhaa hiyo kwa mfumo unaofanana na mashine za kutolea au kuweka fedha (ATM).

“Tutafunga mashine za kuuza maziwa zinazofanana na ATM, mteja anayehitaji maziwa atatumbukiza fedha katika mashine hiyo ambayo itatoa maziwa kulingana na thamani ya fedha aliyotumbikiza,” alisema.

Pamoja na mpango huo, mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Ahmed Salim Abri alisema kampuni yao inaendelea na upanuzi wa kiwanda chao cha Iringa utakaokwenda sambamba na matumizi ya teknolojia ya UHT kutengeneza aina mbalimbali za maziwa.


"Teknolojia hii ya Ultra High Temperature inawezesha maziwa yanayosindikwa kukaa kwa muda mrefu, hadi miezi sita bila kuharibika hata yakiwekwa katika maeneo yasio na mashine za kuyapooza," alisem.


Alisema matumizi ya teknolojia hiyo yatakiwezesha kiwanda chao kuongeza uzalishaji na kupanua soko lake hadi katika maeneo ambayo matumizi ya majokofu ni madogo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.