Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Azunguumza na Ujumbe wa Rais wa Kampuni ya Kichina ya CCECC, Alipofika Ofiosini Kwake Vuga Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kulia akisalimiana na Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya CCECC ya China Bwana Zuang Shangbiao Vuga Mjini Zanzibar.
Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya CCECC ya China Bwana Zuang Shangbiao wa Tatu kutoka Kulia akiel;ezea shukrani zake kwa SMZ kwa kuiamini Kampuni yake kujenga Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni kupitia Mahonda na Kinyasini.Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed.
 Balozi Seif kushoto akisifu umahiri wa Kampuni za Kichina zinazofanya kazi Nchini Tanzania wakati akibadilishana mawazo na Rais wa Kampuni ya CCECC Bw. Zhuang Shangbiao aliyekaa upande wa Kushoto.
Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya CCECC ya China Bwana Zuang Shangbiao Kushoto akimkabidhi zawadi ya Picha ya Ukuta Umkuu wa China { Great Wall} Balozi Seif mara baada ya mazungumzo yao.
Bwana Zuang Shangbiao Kushoto akifurahia zawadi ya  viungo aliyokabidhiwa na Balozi Seif baada ya mazungumzo yao.(Picha na – OMPR – ZNZ.)

Na.Othman Khmais OMPR.
Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi ya  { CCECC } kutoka Nchini China Bwana Zhuang  Shangbiao alisema kitendo cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar cha kuwapa kazi ya Ujenzi wa Bara  bara Nchini kimeleta Heshima kubwa na ya kipekee kwa Kampuni hiyo.
Alisema kazi iliyo mbele kwa Uongozi na Wahandisi wa Kampuni hiyo hivi sasa ni kujipanga vyema katika kuhakikisha heshima waliyopewa na SMZ wanailinda katika kuwajibika ipasavyo  wakati wa utekelezaji wa jukumu hilo zito katika misingi ya ari na bidii kubwa.
Bwana Zhuang  Shangbiao akiuongoza Ujumbe wa Viongozi 7 wa Taasisi hiyo ya Civil Engineering Construction Corporation alisema hayo wakati akitoa shukrani katika mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema kasi ya Ujenzi iliyokuwa nayo Kampuni hiyo ya CCECC kwa zaidi ya Miaka 50 iliyopita inahamishiwa Zanzibar  katika Ujenzi wa Bara bara inayoanzia Bububu, Mahonda  kupitia  Kinyasini hadi Mkokotoni yenye urefu wa Kilomita 31.
Bwana Zhuang alimthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Wahandisi wa Ujenzi wa Kampuni ya CCECC watakamilisha kazi hiyo kwa wakati na katika kiwango kinachokubalika Kimataifa kwa vile wana utaalamu na uzoefu wa kutosha.
Alifahamisha kwamba CCECC  iliyokwishasaini Mikataba ya Kazi kwa Zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 240 Duniani Mwaka uliopita hivi sasa inashikilia nafasi ya 58 kwa ubora kati ya 500 Duniani katika masuala ya jenzi wa Miundombinu ya Madaraja, Bara bara na mambo mengine.
Rais  huyo wa Kampuni ya CCECC alieleza kuwa Uongozi wake ambao tayari umeshafungua Matawi takriban katika  Mataifa 18 Duniani na Bara la Afrika karibu Nchi zote umelenga kusaidia huduma za Kijamii katika kuhakikisha uhusiano wake na Mataifa hayo unaendelea kudumu.
Alisema CCECC yenye utaalamu mkubwa iko tayari pia kuwekeza katika miradi ya ujenzi wa Nyumba za Makaazi na biashara sambamba na kuitikia wito wa uanzishaji wa Viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya uvuvi wa Bahari Kuu utakaotoa ajira pana zaidi kwa Vijana.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Kampuni za Kichina zinastahiki kupongezwa  kutokana na bidii kubwa ya Wahandisi wake katika ujenzi wa Miundombinu tofauti hapa Nchini.
Balozi Seif alisema takwimu zinaonyesha wazi kwamba hivi sasa Kampuni za Kichina zinaongoza kwa kuaminiwa kupewa miradi mbali mbali ya Ujenzi katika Taasisi tofauti za Umma na hata zile Binafsi.
“ Kampuni za Uhandisi wa Ujenzi ya Jamuhuri ya Watu wa China hazina tabia ya kukimbia kazi zinazopewa tofauti na baadhi ya Kampuni nyengine za kigeni zinazoingia mitini baada ya kushindwa kukamilisha kazi ”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Rais huyo wa Kampuni ya CCECC kwamba kukamilika kwa Ujenzi wa Bara bara hiyo ya Bububu, Mahonda kupitia Kinyasini hadi Mkokotoni kutasaidia kuleta matumaini makubwa kwa Wananchi waliowengi.
Balozi Seif aliushauri na kuuomba Uongozi huo wa Kampuni ya CCECC kuwa mabalozi wa kuitangaza Zanzibar zaidi kwa Makampuni mengine ya Uwekezaji ya Nchini China kufikiria kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi hata kwa njia ya Ubia Visiwani Zanzibar.
Bububu, Mahonda kupitia Kinyasini hadi Mkokotoni  ni Moja ya miongoni mwa Mradi wa Ujenzi wa Bara bara Nne za Unguja uliotiwa saini mnamo Tarehe 8 Novemba Mwaka 2017 hapo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “A” Mkokotoni na kushuhudiwa pia na Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Mradi huo unaojumuisha pia Bara  bara za Pale  - Kiongele, Matemwe – Muyuni pamoja na Fuoni – Kombeni zinazotarajiwa kuwa na Urefu wa Kilomita 52 unagharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kupitia Mkopo nafuu wa fedha wa shilingi Bilioni 58 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika {ADB}.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.