Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Waandishi wa Redio Uhuru na Gazeti la Uhuru na Mzalendo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akifanya Mahojiano Maalum na Timu ya Wanahabari wa Redio Uhuru pamoja na Magazeti ya Chama cha Mapinduzi ya Uhuru na Mzalendo waliotaka kujua Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa upande wa Zanzibar kwenye Ofisi ya Uratibu ya SMZ Jijini Dar es salaam.
Balozi Seif Ali Iddi akizungumza  na Mkurugenzi wa Idara ya Asia wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania Bibi Justa Matari Nyange Ofisi ya Uratibu wa SMZ Jijini Dar es salaam.
Mazungumzo hayo yalijikita katika kuangalia hatua zinazoendelea katika maandalizi ya Ushiriki wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara yanayotarajiwa kufanyika katika Jimbo la Guangzhou Nchini China mnamo Mwezi wa Septemba  Mwaka huu.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.                                                                                           
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uagizaji wa baadhi ya bidhaa ikiwamo chakula na Matunda nje ya Zanzibar  umepungua kutokana na hamasa kubwa waliyonayo Wananchi hasa Wakulima katika muelekeo wa kuwekeza zaidi kwenye Sekta muhimu ya Kilimo.
Alisema Sekta ya Kilimo ni miongozi mwa maeneo yaliyopewa msukumo wa kwanza na Chama cha Mapinduzi wakati kikiomba ridhaa ya kutaka kuongoza Dola Nchini Tanzania kwenye Kampeni za Uchaguzi Mkuu kilipokuwa kikitangaza Sera na Ilani yake.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo wakati alipofanya amahojiano Maalum na Timu ya Wanahabari wa Redio Uhuru pamoja na Magazeti ya Chama cha Mapinduzi ya Uhuru na Mzalendo waliotaka kujua Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa upande wa Zanzibar kwenye Ofisi ya Uratibu ya SMZ Jijini Dar es salaam.
Alisema kutokana na Serikali za CCM kusamehe Ushuru wa forodha kwenye vifaa vya Kilimo vinavyoingizwa Nchini sambamba na kuendeleza mafunzo ya kisasa kwa wadau wa Kilimo, Wakulima wengi Nchini hasa wale wanaojishughulisha na kilimo cha Matunda wameongeza mara dufu uwezo wa uzalishaji.
Balozi Seif alisema katika kipindi cha Miaka Mitatu iliyopita mara baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu Wakulima wengi wamekuwa wakilalamikia ufinyu za soko la bidhaa wanazozalisha jambo ambalo imefikia wakati baadhi ya bidhaa hizo zikisafirishwa kupelekwa upande wa Tanzania Bara.
Alisema hatua hiyo imeonyesha mabadiliko makubwa yaliyokuwa yamezoelekea kwa muda mrefu katika kushuhudia Bidhaa nyingi hasa zile za nafaka, Mizizi, mboga mboga  pamoja na Matunda zikiingizwa Zanzibar kutokea Mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba kwa vile Kilimo ndio uti wa Mgongo wa Taifa Wananchi na hasa Wakulima wanapaswa kuendelea kuzalisha mazao yao katika kiwango kinachokubalika Kitaalamu ili Taifa liendelee kupunguza kasi ya kuagiza bidhaa kutoka Nje ya Nchi.
Balozi Seif alisema Serikali imelazimika kufidia pembejeo kwa Wakulima na kupunguza bei ya Dawa ili kuhamasisha Wananchi walio wengi zaidi Vijana kuelekeza nguvu zao katika Sekta ya Kilimo yenye uwezo wa kutoa ajira pana zaidi na kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa.
Akigusia Sekta nyengine za Kiuchumi  akitolea mfano zile za Utalii, Viwanda, Elimu, Afya pamoja na Miundombinu ya Mawasiliano ya Bara bara na Anga Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali chini ya Uongozi mahiri wa Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein imeweza kupiga hatua kubwa katika uimarishaji wa Miundombinu kwenye maeneo hayo.
Alisema ujenzi wa eneo la Maegesho ya Ndege kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Gati ya Malindi na baadhi ya Bara bara zinazoelekea katika maeneo ya Utalii ni mfano hai unaothibitisha utekelezaji wa kasi wa Ilani na Sera ya CCM ya Mwaka 2015/2020 uliofanikiwa ndani ya Miaka Mitatu.
Balozi Seif aliieleza Timu hiyo ya Wanahabari wa Redio Uhuru na Magazeti ya Chama ya Uhuru na Mzalendo kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la kupokea Watalii zaidi ya Laki 500,000 ifikapo Mwaka 2020 inaanza kutoa sura zaidi kwa vile hivi sasa inakadiriwa kufikia zaidi la Laki 350,000.
Kwa upande wa makusanyo ya Mapato Balozi Seif  alisema yapo mafanikio makubwa yiliyofikiwa kutokana na Serikali Kuu kuongeza udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali.
Alisema hatua hiyo imeisababishia Serikali kupitia Taasisi zake kukusanya Mapato yanayokadiriwa kufikia shilingi Bilioni 400,000/- lengo likiwa kuondokana na utegemezi ambao kwa sasa umefikia Asilimia 7% kutoka asilimia 20% katika kipindi cha Mwaka 2013 hadi 2016.
Balozi Seif alifahamisha kwamba mianya ya rushwa imewezeshwa kupungua kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali, Taasisi za Umma pamoja na Wananchi Wazalendo.
Kuhusu suala la Amani na Utulivu wa Taifa Balozi Seif  kupitia Kipindi hicho Maalum cha Mahojiano aliwanasihi Wananchi Bara na Zanzibar kuendelea kuitunza Lulu hiyo iliyo adimu kupatikana katika baadhi ya Mataifa mengi Duniani yakiwemo yale ya Bara la Afrika.
Alisema Viongozi Wakuu kwa kushirikiana na wasaidizi wao wamekuwa mstari wa mbele katika kuisisitiza Jamii kudumisha Amani na Utulivu ambayo ndio ngao kubwa ya kuendeleza mshikamo uliojengeka kwa Watanzania walio wengi Mjini na Vijijini.
Alikumbusha kwamba Serikali zote mbili zitaendelea kusimamia ulinzi wa Amani iliyopo Nchini muda wote hata wakati unapowadia wa Taifa kuingia katika harakati za Uchaguzi Mkuu ambazo huonekana baadhi ya wafuasi wa Vyama vya Siasa wakati mwengine kujaribu kuitikisa Amani hiyo.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa Mazungumzo na Mkurugenzi wa Idara ya Asia wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania Bibi Justa Matari Nyange Ofisi ya Uratibu wa SMZ Jijini Dar es salaam.
Katika Mazungumzo yao Viongozi hao walizungumzia hatua zinazoendelea katika maandalizi ya Ushiriki wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara yanayotarajiwa kufanyika katika Jimbo la Guangzhou Nchini China mnamo Mwezi wa Septemba Mwaka huu.
Balozi Seif alimueleza Mkurugenzi huyo wa Asia kwamba Jamuhuri ya Watu wa China imekuwa Mashirika mkubwa wa Tanzania katika masuala ya Utamaduni, Biashara pamoja na Historia mara tuu baada ya Uhuru wa Tanzania na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Alisema uhusiano huo kupitia mialiko na muingiliano wa ziara za mara kwa mara za pande hizo mbili ni vyema vikaendelea kujengewa mazingia ya kuimarishwa siku hadi siku kwa faida ya Jamii ya sasa na ile ijayo ya pande zote mbili.
Naye Mkurugenzi wa Asia wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania Bibi Justa Matari Nyange alisema kwa vile Kamati za maandalizi ya Maonyesho hayo Chini ya Uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje zimeshaundwa kwa sehemu zote mbili, ipo haja ya kukutanishwa pamoja katika njia ya kupata mafanikio ya jumla.
Bibi Justa alisema kinachotarajiwa kwenda kuwakilishwa katika Maonyesho hayo ya Kibiashara ni ushiriki wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kikamilifu unaojumuisha makusanyo ya Wajumbe wa pande zote mbili za Muungano.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.