Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Akimuapisha Mwenyekiti Mpya wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Ikulu Zanzibar.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto)akimuapisha  Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Mhe.Hamid Mahmoud Hamid kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)  katika hafla iliyofanyika leo katika Ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar,ambapo Viongozi mbali mbali walihudhuria.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  leo amemuapisha Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Hamid Mahmoud Hamid kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein amewaapisha Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ambao aliwateua hivi karibuni kushika nyazifa hizo ambapo Wajumbe walioapishwa ni Mabruki Jabu Makame, Feteh Saad Mgeni, Makame Juma Pandu, Dk. Kombo Khamis Hassan, Jaji Khamis Ramadhan Abdalla na Jokha Khamis Makame.

Hafla hiyo, ilifanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali  ya Mapinduzi ya Zanzibar, akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar  Omar Othman Makungu, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Mawaziri pamoja na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji,Wakuu wa Vikosi vya SMZ, Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Khatib Abrahman Khatib, Washauri wa Rais wa Zanzibar, viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wanafamilia wa viongozi walioapishwa.

Mara baada ya kuapishwa viongozi hao wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) walieleza jinsi walivyoupokea uteuzi huo na kuahidi kutekeleza majukumu yao kwa kufuata Katiba, Sheria na Kanuni za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na kuwaomba Wazanzibari wote kutoa mashirikiano yao kwa Tume hiyo ili kuweza kufanya kazi zake kwa ufansi sambamba na kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini.

Nae Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Hamid Mahmoud Hamid aliahidi kutumia uzoefu alikuwa nao katika masuala ya uchaguzi kwa muda wa miaka saba akiwa Makamo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika kuhakikisha anatekeleza jukumu hilo la kuongoza Tume kwa kufuata Katiba, Sheria na Kanuni zilizopo tena bila ya upendeleo.

Nao viongozi wa vyama vya siasa wamempongeza Rais Dk. Shein kwa kuheshimu Katiba ya Zanzibar na kukidhi matakwa ya Katiba hiyo ya mwaka 1984 ambayo inataka miongoni mwa Wajumbe wawili wa Tume ya Uchaguzi wawe ni kutoka vyama vya upinzani.


Dk. Shein kwa kutumia uwezo aliopewa chini ya Kifungu 119 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 alifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar akiwemo Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid.

Kuteuliwa na hatimae kuapishwa kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) pamoja na Wajumbe hao kumekuja baada ya Wajumbe wa Tume iliyopita kumaliza muda wao  chini ya Mwenyekiti wake Jecha Salim Jecha ambao walifanya kazi kwa kipindi cha miaka mitano kilichoanzia tarehe 30 April, 2013 hadi tarehe 29 April, 2018 walipofikia ukomo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.