Habari za Punde

DK.BASHIRU ASEMA WANAOHUJUMU MALI ZA CCM WATACHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA.

KATIBU Mkuu wa CCM Tanzania akizungumza na viongozi na wanachama wa mikoa miwili ya CCM Pemba katika ukumbi wa skuli ya Fidel Castro Mkoa wa Kusini Pemba.

Na.Is-haka Omar.- Zanzibar..
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania 
Dk.Bashiru Ally amesema Chama hicho kinadhibiti mianya 
ya ubadhilifu wa rasilimali fedha na mali zake ili kijitegemee 
kiuchumi.

Alisema endapo rasilimali hizo zitatumika vizuri na 
kuanzishwa kwa miradi mingine mikubwa ya uzalishaji wa 
kipato katika ngazi mbali mbali za chama na jumuiya kwa  
kuwanufaisha  wanachama wote badala ya watu wachache.

Kauli hiyo aliitoa jana katika mwendelezo wa ziara yake 
kisiwani Pemba wakati akizungumza na viongozi na 
wanachama wa Chama cha Mapinduzi wa Mikoa Miwili 
katika ukumbi wa Fidel Castro uliopo, Mkoa wa Kusini 
Pemba.

Dk.Bashiru alieleza kuwa lengo la kusimamia dhana ya 
ukuaji wa uchumi ndani ya chama kupitia vyanzo vyake vya 
mali na fedha ni kukiondosha chama katika mazoea ya 
kutegemea ufadhili wa watu wenye fedha wanaokuwa na 
malengo ya kujinufaisha wenyewe kisiasa.

Pia aliyataja malengo mengine kuwa ni uimarishaji wa 
maslahi ya watumishi wa CCM na jumuiya zake kwani bado 
maslahi yao ni ya kiwango cha chini ambayo hayaendani na 
hadhi ya taasisi yenyewe.

“ Kwa miaka mingi chama chetu kimeondoka katika misingi 
ya kujitegemea na badala yake kujitokeza kwa watu wenye 
fedha kukichangia chama wakati wa uchaguzi na mazoezi 
mengine ya kitaasisi, sasa katika mageuzi haya ya kimuundo 
tuna dhamira ya chama chetu kukiondosha uko na tukaweza 
kutumia mali zetu wenyewe kujiendesha kitaasisi.” 
Alifafanua Dk.Bashiru.

Alieleza kuwa malengo hayo yakifanikiwa utakuwa ni 
ushindi mkubwa kwa wanachama wa CCM wote kwani tabia 
za rushwa na makundi ya kusaka nafasi za uongozi kwa 
kutumia fedha yatakuwa yamedhibitiwa.

Aliwataka viongozi wote wa taasisi hiyo kuunga mkono 
malengo hayo kwa kuhakikisha wanapunguza matumizi 
holela ya fedha na badala yake waanzishe miradi 
itakayowasaidia kujiendesha ili kulinda heshima na hadhi ya 
CCM mbele ya jamii.

Pamoja na hayo alizitaka jumuiya zote hasa ya umoja wa 
vijana (UVCCM) kuhakikisha wanakuwa wabunifu kwa 
kutumia rasilimia walizonazo kwa kuanzisha miradi 
mikubwa ya kilimo, uvuvi na viwanda vidogo vidogo ili 
vijana wajiajiri wenyewe.

Katibu Mkuu huyo Dk.Bashiru aliweka wazi msimamo wa 
Chama Cha Mapinduzi kuwa wale wote waliohusika na 
kutapeli na kujimilikisha mali za taasisi hiyo kinyume na 
utaratibu wote watachukuliwa hatua za kisheria.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla 
Juma Mabodi alisema wanachama wote wana haki ya 
kuunga mkono mambo mema yanayotekelezwa na taasisi 
hiyo kwa nia ya kuongeza ufanisi.

Alisema wakati wa vyama vya ukombozi vya ASP na TANU 
viongozi wa wakati huo walifanikiwa kupanga mambo ya 
maendeleo yaliyodumu kwa muda mrefu kutokana na umoja 
na mshikamano waliokuwa nao hasa katika masuala ya 
kuvijenga kimaendeleo vyama vyao.

Dk. Mabodi alieleza kuwa suala la uzalendo katika 
kusimamia maslahi ya kitaifa ni jambo muhimu hasa kwa 
viongozi wanaoaminiwa na kupewa dhamana za kuongoza 
jamii.

Akizungumzia ushindi wa CCM visiwani Zanzibar mwaka 
2020 alisema mpaka sasa Zanzibar hakuna upinzani bali 
kuna vikundi vidogo vidogo vya watu wanaojivisha joho la 
upinzani wakati wao ni madalali wa kisiasa waliofilisika 
kifikra.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema CCM itashinda kisayansi 
kutokana na serikali zake kutekeleza mahitaji ya wananchi 
wa mijini na vijijini kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi 
ya mwaka 2015/2020.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.