Na. Abdi Shamnah.
Ilikuwa ni
asubuhi tulivu, jua likiwaka bila kuathiri shughuli za kibinadamu, huku pepo
mwanana za bahari zikivuma na kupunguza makali ya joto, ambalo yumkini tayari limeanza
kuvinyemelea visiwa vya Zanzibar.
Shamra shamra, chereko chereko,
nderemo na hoi hoi zilihanikiza katika viunga vya Ofisi za Shirika la Hudma Maktaba,
ziliopo Maisara, kuashiria kuna jambo kubwa linalojiri.
Hakika ilikuwa ni tukio la
kihistoria, ni muendelezo wa matukio yanayojiri takriban kila mwaka, kwani
kilichofanyika viwanjani hapo kililenga kumuelekeza, kumfahamisha na
kumtanabahisha Mzanzibari, juu ya umuhimu wa kutumia huduma za maktaba.
KUANZISHWA
HUDUMA ZA MAKTABA ZANZIBAR
Mnamo miaka ya 1980, Huduma za
Maktaba zilianzishwa rasmi hapa Zanzibar, na ilipofika mwaka 1993 Baraza la
Wawakilishi likapitisha Sheria Nam.7 ya 1983 uanzishaji wa Bodi ya Huduma za
Maktaba (ZLSB).
Aidha, mnamo mwaka 2009, huduma hizo
ambapo kabla zilikuwa katika Jengo Serena, Shangani mjini hapa, zikahamishiwa katika jengo jipya na la kisasa
Zaidi liliopo Maisara.
Lengo likiwa ni kuwa na taasisi inayotowa
huduma bora za kimaktaba mijini na vijijini , ili wanafunzi wa nagzi zote
pamoja na jamii kwa ujumla , ipate huduma hizo na kujifunza bila malipo, ili hatimae kuwa na kizazi kilichoelimika.
Katika makala hii, mwandishi
anangalia vipi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kupitia Shirika la Huduma za
Maktaba lilivyoungana na jumuiya ya kimataifa, kuadhimisha siku hii muhimu na adhimu kwa lengo la kuhakikisha jamii ya
Wazanzibari inahamasika katika matumizi bora ya huduma za maktaba.
YALIYOJIRI
KATIKA MAADHIMISHO
Maadhimisho yam waka huu yalitanguliwa
na maandamo yaliyoongozwa na watoto wanaotumia huduma za maktaba, wakiwa na
mabango yenye kaulimbiu inayosomeka ‘kusoma
na kuendeleza ujuzi’.
Aidha,
yalipambwa kwa aina tofauti za maonyesho, ikiwemo yale ya vitabu , usomaji wa tenzi, nyimbo na onyesho maalum la ‘English-Debate’, ambapo
kundi moja la wanafunzi kwa mtazamo wao wanahisi lililo bora kwao katika matumizi ya vita bu ni
kurudufu nakala za vitabu (kutowa kopi), huku kundi jingine likisisitiza
umuhimu wa kununua vitabu, kama njia sahihi ya kufikia azma ya kujifunza.
Hata hivyo, kupitia onyesho hilo lililoendeshwa
kwa lugha ya kiingereza, ufumbuzi sahihi ukafikiwa kuwa njia ilio bora ni ‘kwenda
maktaba pekee, mahala ambapo huduma za vitabu, majarida, magazeti na machapisho
mengine hupatikana na mtu kujisomea bila malipo’.
Suluhisho hilo likabainishwa kwa hoja,
kuwa utaratibu wa kutowa kopi nakala za
vitabu una changamoto zake, ikiwemo Haki miliki ya muandishi, jambo ambalo
lapaswa kufanyika kwa ridhaa ya muandishi. Lakini pia hoja ya kununua vitabu vipya, nayo ikabainishwa
changamoto zake ikiwemo ya kuwa na uwezo wa kutosha kwa maana ya fedha nyingi,
kwa kuzingatiwa muhusika atakuwa na
mahitaji ya vitabu zaidi ya kimoja.
Kuambatana na onyesho hilo ufafanuzi
ukatolewa kuwa Huduma za Maktaba hutolewa bure kituo hapo, ambapo kimsingi
kinachohitajika ni kujisajili.
Imeelezwa kuwa kwa mwanafunzi wa
skuli ya msingi itamlazimu kulipia shilingi 1,000/-, mwanafunzi wa Sekondari shilingi
3,000/- na kwa wale walioko Vyuo vikuu
wanahitajika kulipia shilingi 5,000, ambapo fursa kubwa watakayoipata ni pamoja
na kujisomea vitabu hivyo nyumbani.
NASAHA ZA
WADAU
Sichana Haji Foum ni Mkurugenzi wa
Shirika la Huduma za Maktaba Zanzibar, anasema mkusanyiko huo unalenga
kuwakutanisha wadau na kuwahamasiha umuhimu wa kupenda kusoma na kuandika.
Anabainisha kuwa Shirika la Elimu,
Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) mnamo mwaka 1965 lilibaini
kuwepo kwa tatizo kubwa la watu kutokujua kusoma na kuandika, hivyo mnamo mwaka
1966 maadhimisho hayo yalianza.
Anasema lengo ni kutathmini mafanikio
na changamoto zinazoikabili jamii katika kufanikisha dhana ya kujua kusoma na
kuandika.
Aidha anasema kwa vile Shirika la Huduma za Maktaba Zanzibar
ni wadau, hivyo kuna kila sababu za kujumuika
na kuadhimisha siku hiyo.
Kwa mnasaba huo, analitolea pongezi
Shirika la Book Aid International kutoka nchini Uingereza kwa misaada mbali
mbali inayotowa kwa shirika hilo, ikiwemo uaptkanji wa vitabu, ambavyo hatimae
husambazwa skuli mbali mbali Unguja na Pemba, ambapo nao huanzisha maktaba zao.
“Sio rahisi kwa wazazi kuwa na uwezo
wa fedha za kutosha kununua vitabu kwa ajili ya wanafunzi, hivyo wenzetu hawa
wamekuwa wakiondowa hiyo ‘gape’ iliopo kati wenye
nacho na wasio nacho”, anasema.
Aidha, anasema ni jambo gumu kwa
mwanafunzi au jamii kwa ujumla kujifunza iwapo haiwezi kusoma, na kubainisha
kuwa wale wanaosoma wanakuwa katika nafasi nzuri ya kuendeleza ujuzi walionao.
“Iwe mwanafunzi, iwe mwalimu, iwe
mkulima au jamii kwa jumla, shughuli zako utazifanya kwa ufanisi”, anaongeza.
Mkurugenzi Sichana akawakumbusha
wadau, jinsi kitabu kitakatifu cha Qoraan kilivyokuja na kuhimiza umuhimu wa suala
la kusoma, ikiwa ni njia ya kupanuwa wigo wa ufahamu kwa binadamu.
Akatowa wito kwa wadau wote
kuishajiisha jamii kujenga utamaduni wa kupenda kusoma na kuandika, sambamba na
kuzitumia kikamilikfu huduma za maktaba ili kujiongezea maarifa.
Nae, Mwalimu Ali mwalimu, Katibu wa Jumuiya
ya Waandishi wa Vitabu Zanzibar, akabainisha shughuli zinazofanywa na jumuiya
hiyo, kuwa ni pamoja na kuihamasisha jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa
ujumla, umuhimu wa kusoma vitabu.
Anasema chanzo cha kuanzishwa Jumuiya
hiyo kuliotokana na changamoto iliyokuwepo ya wananchi kutokuwa na utamaduni wa
kupenda kusoma vitabu, hivyo kuundwa kwake kulilenga kumuamsha Mzanzibari juu ya umuhimu wa jambo hilo.
Anasema, “kuanzia hapo tulianza
kufanya juhudi za kuandika na ndio leo hii unakuta kuna vitavu vingi
vilivyoandikwa na Wazanzibari”.
“Hivi sasa kuna umuhimu kwa wadau
kukaa na kutafakari, kwani hali ya usomaji wa vitabu haiko vyema, hakuna
utamaduni wa kusoma vitabu’, anasema.
Amewataka wadau walioshiriki katika
maadhimisho hayo kutumia fursa hiyo kuishajiisha jamii kujenga utamaduni wa
kusoma vitabu, akibainisha jinsi Jumuiya yake, ilivyojidhatiti katika jambo
hilo, kwani ina kipindi maalum kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar( ZBC TV).
Anaedelea kuitanabahisha jamii kuwa suala
la matumizi yaa huduma za mkataba, hayapo kwa ajili ya wanaafunzi pekee, bali
ni kwa ajili ya watu wote.
Aidha, anashauri kuziunga mkono na
kuziimarisha maktaba za skuli, kwa kigezo kuwa haziko vyema na zinakabiliwa na chanagmoto
kadhaa, ikiwemo ukosefu wa vitabu, sambamba na maktaba za Wilaya ambazo bado
hazijaanzishwa.
“Kuna maktaba za wananchi, ni mfano
ule ule utakuta kwenye majumba yetu, mtu kaweka ‘shockest’ lake ukumbini, kuna
vitu kadhaa vya thamani……..vikombe, visahani na vingine kadha wa kadha, lakini
huwezi kukuta vitabu………”, anaonyesha mshangao.
Anasema kuna haja kwa skuli kuanzisha
maktaba zao ili wanafunzi watumie fursa ya kujifunza kikamilifu.
Nae, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la
Huduma za Maktaba Fatma Hassan Kingwaba, akaitanabahisha jamii juu ya thamani
ya elimu na gharama zinazowakabili wazazi katika kufanikisha azma ya kuwapatia
elimu bora watoto wao.
Anasema Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa kulifahamu hilo, imelazimika kuanzisha miundombinu ya elimu,
ikiwemo Shirika la Huduma za Makatba, kwa lengo la kusaidia juhudi za
wananchi/wazazi kuwapatia elimu watoto.
“Ninaiomba jamii ithamini juhudi za
Serikali za kuanzisha huduma hizi za maktaba tofauti, ikiwemo za shule. Tujenge
utamaduni wa kupenda kusoma vitabu, kuna vitabu vimetungwa na watunzi wetu;
vimezingatia lugha, mila, silka na maadili yetu”, anafafanuwa.
Hudhaifa Haji ni Mkutubi katika
Shirika la Huduma za Maktaba Zanzibar, anasema huduma hizo zinapatika kwa watu
wa aina zote, ikiwemo wanafunzi wa skuli za msingi, sekondari, vyuo vikuu
pamoja na wananchi wengineo.
Anasema kuna utaratibu uliopangwa kwa
watoto wanaosajiliwa kujifunza katika siku za ijumaa, ambapo hupata fursa ya
kufundishwa namna bora ya kusoma, kuchora, kuimba pamoja na kushiriki michezo
mbali mbali inayolenga kuimarisha uwezo wao wa akili.
Anatowa wito kwa wazazi na walezi
kuwapeleka watoto wao katika shirika hilo ili kupata mwanga na kuwa na msingi
bora wa kielimu.
“Tunaiomba jamii ihamasike na
kuwaleta watoto wao hapa, angalau kwa siku ya Ijumaa, ili kuwafanya watoto
wajenge utamaduni wa kupenda kusoma na kuandika”, anasema Hudhaifa.
Katibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Amali Zanzibar, Dk. Muslih Hijja ambae alikuwa mgeni rasmi katika
maadhimisho hayo akimuwakilisha Naibu Waziri wa Wizara hiyo. Anasema, kwa
mujibu wa Shirika la Kimataifa la UNESCO katika taarifa iliyotolewa mwaka 2016,
inakadiriwa zaidi ya watu Milioni 775 hawajui kusoma wala kuandika Duniani kote.
Akinukuu takwimu za Shirika hilo
anasema kila penye watu wazima watano (5), basi kuna mtu mmoja ambae hajuwi
kusoma na kuandika, ambapo miongoni mwao, asilimia sitini na sita (66%) ni wanawake.
“Hii inaonyesha kwa kiasi gani tatizo
hilo lilivyo kubwa na juhudi madhubuti zinazohitajika kuchukuliwa ili kupunguza
au ikiwezekana kuliondosha kabisa tatizo la kutojua kusoma na kuandika”,
anasema.
Aidha, anasema maktaba zina
mchango mkubwa sana kwa jamii katika kuhakikisha wananchi wanapata fursa
za kusoma kupitia vitabu na machapisho mengine kama vile magazeti, majarida na huduma
za mitandao (internet).
Anasema kuna muhimu kwa Shirika hilo kuendelea
kuihamasisha jamii kuchangamkia fursa hizo, kwa kigezo kuwa kuna nafasi kubwa
ya kuwanyanyuwa kiuwezo katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni
na pia kwenda sambamba na maendeleo ya Ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia.
Anaeleza kuwa katika kuhakikisha
wananchi wa Zanzibar wanaweza kusoma na kuandika, Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inafanyakazi kwa karibu na wadau mbali mbali wa elimu ndani na nje ya
nchi.
Akatumia fursa hiyo kulipongeza
Shirika la ‘Book Aid International’ la Uingereza, kwa kuwa mstari wa mbele
kusaidia juhudi za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kupunguza tatizo la
kutokujua kusoma na kuandika.
“Serikali yetu inapenda kulishukuru
sana Shirikia hili kutokana na jitihada zake ambazo leo hii sote ni mashahidi
kwamba Shirika la Maktaba, lililo chini ya Wizara Elimu na Mafunzo ya Amali
limekuwa likipokea msaada wa vitabu vipya na vizuri ambavyo husaidia kuendeleza
maktaba za Jamii, skuli na hata maktaba
za Vyuo”, anasema.
Anasema hayo yanafanyika kwa lengo la
kuyabadili maisha ya wananachi , akiamini kuwa mtu asiyejuwa kusoma na kuandika
ni sawa na yule anaeishi gizani.
Dk. Muslih anasema kuna kila sababu
ya Serikali kuwahimiza wananchi wake kuongeza bidii katika kusoma pamoja na
matumizi ya maktaba.
Akiziainisha sababu hizo, anasema ni
pamoja na ukweli kuwa kusoma ndio msingi mkuu katika mafanikio ya kielimu na
katika maisha.
Anasema kusoma kunaongeza uwezo wa
ubongo kufanya kazi, kama ilivyo kwa wanaofanya mazoezi ambapo huongeza uwezo wao
wa misuli.
Anasema pia kusoma kunaongeza ukwasi
wa misamiati, “ kadri unavyosoma vitabu vingi kutoka kwa waandishi mbali mbali,
ndivyo unavyojitajirisha katika suala la misamiati”.
Aidha, anasema hatua ya kuwa na misamiati mingi kunasaidia sana katika maisha
ya kila siku, kwani humfanya mtu kujiamini na kujenga uwezo mzuri wa kuzungumza
mbele ya hadhira.
“Kusoma kunaimarisha stadi za uandishi,
waandishi mahiri ni wale waliopata msukumo kutokana na usomaji wa kazi za waandishi
wengine hususan waliobobea”, anaeleza.
Katika hatua nyengine, anasema kusoma
kunaongeza maarifa, ambapo humpa mtu taarifa mpya, jambo linalomfanya mtu kuwa
na utajiri wa maarifa, ikiwa nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto
zinazojitokeza maishani mwake.
Katibu Mkuu huyo, akatanabahinisha
jinsi kusoma kunavyoweza kuongeza uwezo wa kufikiria na kupambanuwa mambo,
sambamba na kuleta burudani isiyo na gharama.
“Ni kweli vitabu vingi vizuri huuzwa
kwa bei ghali, lakini usisahau kuwa unaweza kupata burudani ya karibu ya bure
kupitia vitabu, kwa kujenga mazoweya ya kutembelea maktaba katika eneo lako”,
anabainisha.
Anaeleza kuwa Maktaba huwa na
mchanganyiko wa vitabu vya kila aina, kuanzia riwaya hadi taaluma mbali mbali.
Katika hatua nyengine Injinia huyo
anatowa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wote
waliofika umri wa kusoma wanapatiwa fursa endelevu za kielimu ili kuondokana na
tatizo sugu la kutojua kusoma na kuandika kwa maslahi ya Taifa.
“Wazazi na walezi ni watu muhimu sana
katika kuwasimamia watoto kujua kusoma na kuandika, suala hili si la walimu
peke yao, ila ni la jamii nzima, tushirikiane pamoja ili tuweze kulipatia
ufumbuzi wa kudumu”.
Dk. Muslih anabainisha njia za
kufuatwa na wazazi pamoja na walezi katika kumsaidia mtoto ili kumuwezesha kujua
kusoma na kuandika, kuwa ni pamoja na kusoma pamoja na watoto hao na
kuwasikiliza wanaposoma, sambamba na kuweka vitabu nyumbani.
Aidha, anawataka wazazi/walezi
kufanya ushawishi kwa kuwapeleka watoto
maktaba ili waweze kusoma vitabu pamoja na kuchukuwa nyumbani kwa ajili ya
kujisomea.
Anasema endapo kutakuwa aa usimamizi
mzuri, bila shaka watoto na jamii kwa ujumla itajenga utamaduni imara wa
kupenda kusoma na kuongeza ufaulu katika masomo yao, sambamba na kuwa na uwezo
wa kuendeleza ujuzi katika mambo mbali mbali.
Nidhahiri kuwa suala la kubadili
mitizamo kwa wanafunzi na jamii ya Wazanzibari kwa ujumla, hususan katika suala
zima la kutumia huduma za maktaba linahitajika.
Kuna ukweli kuwa bado jamii ya
Wazanzibari haina utamaduni wa kutumia huduma za maktaba, kwa kile
kinachoonekana kutokuwepo utamaduni wa kupenda kusoma na kuandika.
Hivyo ni wakati sasa kwa Wazanzibari
kubadilika na kuhamishia nguvu zao katika kujenga utamaduni wa kupenda kusoma vitabu, ikizingatiwa kuna
vipaji vingi vya waandishi mahiri wa vitabu, hususan vya Kiswahili hapa nchini.
Wakati Wazanzibari wakiungana na Jumuiya za
Kimataifa kuadhimisha siku ya Kujua kusoma na kuandika, ni wakati pia wa
kutafakari kwa kiasi gani tunachukuwa hatua maridhawa katika kuwasaidia watoto na
jamii kwa ujumla kujua kusoma na kuandika
No comments:
Post a Comment