Habari za Punde

Maamuzi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania Kuhusu Rufaa ya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani Utakaofanyika Tarehe 13 OKTOBA 2018.

TAARIFA KWA UMMA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea Rufaa moja (1) kutoka kwa mgombea 
Udiwani wa Kata ya Kibutuka katika Halmashauri ya Wilaya Liwale, Tume 
imefanya hivyo kwa kuzingatia Kifungu cha 44(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya 
Serikali za Mitaa kikisomwa pamoja na Kanuni ya 28(1) ya Kanuni za 
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2015.

Rufaa hiyo iliwasilishwa na mgombea Udiwani kutoka Chama cha Wananchi CUF, Ndugu Mdohoma Bashiru Ismaili akitaka arejeshwe kuwa mgombea udiwani katika Kata ya Kibutuka kupitia chama hicho.

Kuenguliwa kwake kulitokana na kuwekewa pingamizi na mgombea mwenzake kwa madai kuwa majina yake katika fomu ya uteuzi yalitofautiana  na Msimamizi wa uchaguzi kukubaliana na pingamizi hilo na hivyo kumuengua.

Tume katika kikao chake cha tarehe 30 Septemba 2018, imekubaliana na maelezo ya mrufani na kuelekeza arejeshwe kuendelea kuwa mgombea Udiwani katika Kata ya Kibutuka, Halmashauri ya wilaya ya Liwale kwa kuwa imejiridhisha kwamba mrufani wakati wa kujaza fomu yake ya uteuzi Na. 8C alianza na jina la mwisho likifuatiwa na majina mengine kwa kuwa ndilo alilotaka lianze kuandikwa kwenye karatasi ya kupigia kura.
Kwa mujibu wa Maelekezo ya Tume kuhusu ujazaji wa fomu Na. 8 C ya Uteuzi katika kipengele namba (2) yanatoa uhuru kwa mgombea kuanza na jina ambalo angetaka liandikwe kwa herufi kubwa kwenye  karatasi ya kupigia kura.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inavikumbusha Vyama vya Siasa na Wagombea 
wanaoshiriki uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Liwale na Udiwani 
katika Kata mbalimbali za Tanzania Bara, utakaofanyika tarehe 13 Oktoba 
2018 kuzingatia Sheria na Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na 
Madiwani ya Mwaka 2015, wakati wote wa kampeni na hata Siku ya 
Uchaguzi.
Imetolewa leo  tarehe  30 Septemba ,2018

Hamis Mkunga
KAIMU MKURUGENZI WA UCHAGUZI

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.