Habari za Punde

Umuhimu Mkubwa wa Kwa Jamii Kuwa na Uhakika wa Lishe Bora Ndio Nguzo Imara Kulinda Uhuru na Kuondoa Utegemezi -Dkt. Shein.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein(kushoto) alipokuwa akitoa hutuba yake katika sherehe za uzinduzi wa maonesho ya Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika leo katika kijiji cha  Chamanangwe Wilaya ya Wete Mkoa  wa Kaskazini Pemba,[Picha na Ikulu .]11 Oct 2018.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa upo umuhimu mkubwa kwa jamii kuwa na uhakika wa chakula na lishe bora kwa sababu hio ndio nguzo imara ya kuulinda uhuru na kuondoa utegemezi.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika sherehe za ufunguzi wa maonesho ya Siku ya Chakula Duniani, ambapo kwa Zanzibar zimefanyika Chamanangwe, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na wananchi.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kuwa uhakika wa chakula na lishe bora ni muhimu katika kuimarisha afya za wananchi na kuchangia katika kuondoa umasikini.

Aliongeza kuwa sababu hiyo ndiyo iliyopelekea maonesho hayo yakapewa uzito mkubwa katika mipango muhimu ya Serikali ukiwemo MKUZA Awamu ya 3, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020, Sera na mikakati ya kiserikali ikiwemo mkakati wa Mapinduzi ya Kilimo.

Alisema kuwa mikakati ya jumla inayotolewa na mipango iliyopo inalenga katika kuongeza uzalishaji, ujenzi na upatikanaji wa miundombinu, utiaji wa thamani na uhifadhi wa chakula kwa lengo la kuongeza tija, kipato na kuondoa umasikini hapa Zanzibar.

Rais Dk. Shein alisema kuwa katika awamu mbali mbali za uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Serikali imebuni na kuitekeleza mikakati na program mbali mbali ili uzalishaji wa mazao mbali mbali yakiwemo ya chakula na biashara unaongezeka na kupata tija zaidi.

Alieleza kuwa katika Awamu ya Saba ya Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jitihada maalum zimefanywa kwa lengo la kuongeza mavuno ya mpunga kwa upande wa mazao ya chakula na zao la karafuu kwa mazao ya biashara.

Alisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kupunguza kiwango cha uagiziaji mchele nje ya nchi na kujitosheleza kwa mchele angalu kutoka asilimia 39.9 ya sasa hadi asilimia 60 ifikapo mwaka 2020 jambo ambalo linawezekana ambapo tayari jitihada za wakulima na serikali zimeanza kuonekana.

Dk. Shein alisema kuwa katika kufikia dhamira ya kuwa na uhakika wa chakula na lishe bora Serikali inatambua na kuendelea kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili wakulima na sekta yote ya kilimo.

Alitumia fursa hiyo kutoa wito na indhari wka wale wote wanaojenga majengo ya makaazi katika mabonde ya mpunga kuonoka wenyewe huku akiwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya  kuanza kulichukulia hatua suala hilo.

Aliongeza kuwa katika kuzitatua changamoto hizo Serikali imetenga jumla ya TZS bilioni 63 kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya kilimo nchini ikiwemo uzalishaji wa mazao, mifugo, mazao ya  biashara, uimarishaji wa huduma na miundombinu, usarifu pamoja na utekelezaji wa miradi mengine ya maendeleo.

Rais Dk. Shein aliwahakikishia wakulima na wananchi kuwa Serikali itaendelea kuitekeleza dhamira yake ya kutoa ruzuku kwa wakulima wa mpunga ili kuhakikisha kuwa malengo ya kuongeza mavuno yanazidi kupata mafanikio.

Kwa maelezo ya Rais Dk. Shein Serikali inaendelea na jitihada za kupunguza utegemezi wa mvua katika kilimo cha mpunga kwa kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji maji ambapo katika mradi wa kuongeza uzalishaji wa mpunga (ERPP), Serikali itajenga miundombinu hekta 193 Unguja na Pemba kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu za mpunga.

Alieleza kuwa hivi sasa tayari hatua za ujenzi na upelekaji wa umeme zinaendelea katika mabonde ya Dodeani, Machigini, Dobi, Kwalempona kwa upande wa Pemba na katika mabonde ya Mtwango, Koani, Bandamaji, Mchangani na Kibondemzungu kwa upande wa Unguja.

Kadhalika alisema kuwa Serikali imechukua mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 50 kutoka Banki ya Exim ya Korea kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji wa hekta 1,524 sawa na ekari 3,810 katika mabonde ya mpunga ya Cheju, Kilombero na Bumbwisudi kwa Unguja na Makwararani na Mlemele kwa upande wa Pemba.

Katika kuhakikisha Zanzibar inahifadhi ya mazao na kujikinga na balaa la njaa, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeandaa mpango madhubuti wa kuanzisha ghala la chakula cha akiba ambapo tayari ghala moja limeshatayarishwa.

Alisema kuwa ghala hilo limefanyiwa matengenezo makubwa yaliyogharimu TZS 254,767,000 ghala ambalo lipo Malindi mjini Unguja na lenye uwezo wa kuhifadhi tani 6000 za mchele kwa wakati mmoja na linatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni na katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali imedhamiria kulifanyia matengenezo makubwa ghala la Tibirinzi huko Pemba.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha sekta ya ufugaji na uvuvi ili nazo ziwe kuchangia katika kuyafikia malengo ya kuwa na uhakika wa chakula na lishe bora.

Alisema kuwa kwa lengo la kuzidi kuimarisha sekta ya uvuvi, Serikali imeanzisha Kampuni ya uvuvi na hivi sasa inatengeneza meli mbili za uvuvi nchini Maldives na Sri Lanka zenye uwezo wa kuvua tani 90 za samaki kwa wiki kwenye bahari kuu.

Aliwanasihi vijana wazitumie fursa za ajira zilizopo katika sekta ya kilimo,ufugaji na uvuvi katika kukabiliana na changamoto za uhaba wa ajira Serikalini na Serikali iko tayari kuwawezesha. Alisema kuwa tayari kuna mwekezaji kutoka nchini China ambaye analengo la kuja kisiwani Pemba kuekeza kiwanda cha samaki.

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali  imeanzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, Wakala wa matrekta na zana za kilimo na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoikabili sekta za kilimo kwa ujumla wake na kubuni njia bora za kuongeza uzalishaji kulingana na mazingira yaliopo.

Alisisitiza kuwa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi lazima ihakikishe inaziwezesha Taasisi za utafiti kwa kila hali na kuzisimamia vizuri ili zitoe matunda ya kazi zao kwa lengo la kuongeza tija katika sekta ya kilimo na ufugaji.

Alisema kuwa Serikali itaendelea kupambana na misumeno ya moto na inayopatiakana hivi sasa itaendelea kuchomwa moto huku kukiandaliwa taratiu za kuwepo sheria za kuwashtaki wanaokutwa na misumenohiyo, ambapo pia aligusia umuhimu wa uhifadhi wa mazingira. Dk. Shein alitembelea mabanda mbali mbali ya maonesho.

Nae Waziri wa Kilimo, Maliasili na Uvuvi Rashid Ali Juma alieleza kuwa uongozi wa Wizara unatoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa uwamuzi wake wa kuagiza sherehe hizo kwa mwaka huu zifanyika kisiwani Pemba na kueleza maamuzi hayo ni ya busara katika kuimarisha kilimo.

Alieleza kuwa  kauli mbiu ya mwaka huu ni “Juhudi zetu ndio hatma yetu” Dunia bila ya njaa inawezekana ifikapo 2030” na kusisitiza kuwa kwa juhudi za makusudi hilo linawezekana huku akisema kuwa misumeno ya moto 295 imekamatwa na inaendelea kuteketezwa.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Maliasili na Uvuvi Maryam Juma Saadallah alieleza kuwa eneo hilo lililofanyiwa maonesho lina ukubwa wa ekari 85 ambapo Wizara imetenga ekari 17 kwa ajili hiyo ambapo katika kufanikisha shughuli hiyo jumla ya milioni 116 zimetumika.

Alisema kuwa siku ya chakula duniani kwa mwaka 2018 yatafikia kilele chake tarehe 16 Oktoba 2018 ambapo lengo ni kuwaweka pamoja wadau wa sekta za kilimo wakiwemo wataalamu, wakulima, wafugaji, wavuvi, wajasiriamali na wafanyabiashara.

Nae Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la FAO na IFAD Tanzania Dk. Mwatima Abdalla Juma alisema kuwa Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayojishughulisha na kilimo na ufugaji yataendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.