Habari za Punde

WAZIRI MKUU AWAONYA WAAGIZAJI WA TAULO ZA KIKE *Ni wale wazaoziuza kwa bei ya juu licha ya Serikali kuziondolea kodi *Asisitiza kwamba Serikali haitasita kuwafutia leseni zao za uagizaji

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewatakabaadhi ya waagizaji wa taulo za kike ambao wanaziuza kwa bei ya juu licha ya kufutwa kwa kodi, waache mara moja na Serikali haitasita kuwafutia leseni zao za uagizaji mara watakapogundulika kutotekeleza maelekezo hayo.


Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Jumatano, Novemba 7, 2018) wakati akizindua mkakati wa Bunge wa masuala ya kijinsia, Bungeni jijini Dodoma. Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanawake wanawekewa mazingira mazuri yatakayowawezesha kupiga hatua zaidi.

Amesema hatua hizo ni pamoja na kuondoa kodi ya  taulio za kike ili kuwezesha wanafunzi wa kike ambao walikuwa wanaacha masomo kutokana na changamoto ya kununua taulo za kike kwa ajili ya kujisitiri wakati wa hedhi wazipate kwa gharama nafuu.

Waziri Mkuu amesema hatua nyingine ni mpango wa Serikali wa kujenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya katika kila kata kwa lengo la kupunguza vifo vya wanawake na watoto vilivyokuwa vinasababishwa na uhaba wa huduma za afya ya mama na mtoto. 

Amesema mpango huo wa Serikali unatarajiwa kuongeza tija kwa wanawake hususan katika kuwapunguzia muda ambao wamekuwa wakiutumia katika kutafuta huduma hizo ambazo zilikuwa zinapatikana kutoka umbali mrefu.

“Imethibitika kupitia tafiti za kitaifa na kimataifa kwamba uzazi wa mpango huweza kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa hadi asilimia 44 na vifo vya watoto kwa hadi asilimia 35.

 Pamoja na kulinda afya ya mama na mtoto, huduma hizi zinawasaidia wanawake na wasichana kupata nafasi za kujiendeleza zaidi pamoja na familia zao na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi, kijamii, na kimaendeleo.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuwahamasisha wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi sambamba na kuwawekea mazingira wezeshi. 

Amesema hatua nyingine ni mpango wa Serikali wa kuwasomesha wanawake katika ngazi ya uzamili ili waweze kushika nafasi nyingi zaidi za uongozi Serikalini na mahali pa kazi. Zoezi hilo linaratibiwa na Idara Kuu ya Utumishi.

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu amesema mifumo yetu, mila na historia vimewafanya wanawake na wasichana wabaki nyuma kwa kujiajiri kwenye sekta isiyo rasmi na isiyo na kipato cha uhakika wala maslahi na kubaki wakiwa wategemezi kiuchumi. 

Amesema hivi karibuni Serikali imeanza  kutekeleza kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani. Kampeni hiyo inalenga kuwaondolea wananchi hususani wanawake tatizo la upatikanaji wa haraka wa huduma ya maji safi na salama. 

Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema Bunge linaendeshwa kwa kuzingatia uwiano wa kijinsia kwa kiwango cha kuridhisha. “Hata tunapoteua baadhi ya wabunge kwa ajili ya kutuwakilisha katika mikutano mbalimbali huwa tunazingatia uwiano wa kijinsia.

Amesema atahakikisha Bunge linaendeleza azma ya Serikali ya kujenga Taifa lenye usawa wa kijinsia inatimia, ambapo amewataka mawaziri wanapowasilisha hotuba za makadirio ya mapato na matumizi ya wizara zao waeleze namna walivyotekeleza jambo hilo.

Imetolewa Na:
Ofisi ya Waziri Mkuu,
S. L. P. 980,  41193 – Dodoma
Jumatano, Novemba, 7, 2018.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.