Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Azungumza na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la China

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China Cai Dafeng, ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China Cai Dafeng, ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma 
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akutana na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China Cai Dafeng, ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mahagama, akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China Cai Dafeng, ofisini kwa Waziri Mkuu Mlimwa jijini Dodoma 
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa, akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China Mr.Cai Dafeng,alipofika Ofisini kwake Jijini Dodoma kwa mazungumzo.(Picha na OWM)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameishukuru Serikali ya China kwa kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanyika nchini hivi sasa chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano.

Ametoa shukrani hizo jana jioni (Ijumaa, Novemba 16, 2018) alipokutana na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China, Bw. Cai Dafeng ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

“Tunaishukuru Serikali ya China kwa sababu tumepokea misaada na mikopo ya gharama nafuu na kuendeleza miradi mbalimbali kama vile mradi wa umeme wa Kinyerezi, awamu ya pili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Zanzibar,” alisema.

Alisema Serikali ya China imekuwa pia na mahusiano ya muda mrefu na Serikali ya Tanzania na hasa kwenye sekta ya afya ambapo kuna wanafunzi wengi wa Kitanzania ambao wako China wakisomea udaktari na masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

“Tuna mahusiano mazuri kwenye sekta ya afya na sasa hivi tuna madaktari 20 ambao wanasoma huko na wengine wanasomea masuala ya TEHAMA. Pia tuna mahusiano mazuri baina ya Bunge la Tanzania na China,” alisema.

Waziri alisema Tanzania imejipanga kuinua uchumi wake kupitia ujenzi wa viwanda na sekta nyingine kama utalii kutokana na vivutio vilivyopo nchini kama vile Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama za Serengeti na visiwa vya Zanzibar. “Nimefurahi kusikia kuwa hivi karibuni tutapata idadi kubwa ya watalii kutoka China,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China, Bw. Cai Dafeng alisema amefurahishwa na jinsi Serikali ya awamu ya tano inavyoendelea kubadili hali ya uchumi wa nchi na maisha ya Watanzania chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli.

Alisema China itaendelea kuiunga mkono Tanzania kwenye masuala ya kiuchumi na haiko tayari kuona ikiingiliwa masuala yake ya ndani na mataifa kutoka nje.

Akizungumzia kuhusu masuala ya uwekezaji baina ya Tanzania na China, Bw. Cai alisema China itaendelea kuyahimiza makampuni ya nchi hiyo ili yawekeze zaidi nchini Tanzania kwenye maeneo mbalimbali kama vile ujenzi wa bandari ya Bagamoyo. “China inataraji kuongeza uwekezaji kwenye kilimo, nishati na miundombinu,” alisema.

Kuhusu elimu, Bw. Cai alisema Serikali ya nchi hiyo inaangalia uwezekano wa kuanzisha masomo ya lugha ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili Watanzania wengi zaidi waweze kujifunza lugha hiyo.

Kuhusu afya, alisema China itaendelea kutuma madaktari wake ili waje kutoa huduma kwa Watanzania na inatamani kuona mahusiano baina ya mtu mmoja mmoja kutoka nchi hizo mbili ikiendelea kukua.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.