Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Balozi Kuwait Nchini Tanzania leo.

Balozi wa Kuweit Nchini Tanzania Bwana Mubarak Mohammed Al – Sehaijan Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika kujitambulisha Rasmi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiishukuru Kuweit kupitia Balozi wake Nchini Tanzania kwa jitihada za kuendelea kuiunga Mkono Tanzania katika Miradi ya Maendeleo na Uchumi.
Balozi Mubarak Mohammed Al – Sehaijan akisisitiza umuhimu wa Nchi yake kuangalia maeneo mengi ya kuunga mkono harakati za Kiuchumi za Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis.OMPR.
Balozi wa Kuweit Nchini Tanzania Bwana Mubarak Mohammed Al – Sehaijan alisema Zanzibar bado ina nafasi ya kutumia fursa iliyotolewa na Kuweit kwa Zanzibar ya kuangalia maeneo ambayo inaweza kuungwa mkono katika kuona Miradi ya Wananchi inazidi kuimarika zaidi.
Alisema zipo Sekta za Kiuchumi na Maendeleo za Zanzibar kama Afya, Elimu na Mawasiliano zilizopata msukumo Kutoka Serikali ya Kuweiti kupitia Mfuko wake wa Misaada { Kuweit Fund } lakini bado Nchi hiyo ina kiu ya kuona na Sekta nyengine zinapata mafanikio makubwa.
Balozi Mubarak Mohammed Al – Seijan alisema hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali alipofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa na Nchi yake kushika wadhifa huo wa Kidiplomasia.
Alisema wakati Zanzibar inapaswa kutafakari maeneo mapya ya kuungwa mkono,  Kuweit kwa sasa tayari imeshaandaa mpango Maalum wa kukisaidia Chuo Kikuu cha Sumeit kiliopo Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar katika kukiongezea nguvu kwenye fani za Biashara na Sayansi.
Balozi Mubarak alieleza hatua hiyo imelenga kustawisha Jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa Ujumla katika masuala ya Taaluma ambayo ni muhimu katika mazingira ya Binaadamu hasa ikizingatiwa mabadiliko makubwa ya kasi ya Sayansi na Teknolojia yanayoizunguuka Dunia kwa sasa.
Akizungumzia Sekta ya Utalii inayozidi kushika kasi Zanzibar, Balozi huyo wa Kuweit Nchini Tanzania alisema wakati umefika kwa Taasisi zinazosimamia Sekta hiyo kuwa na agenda maalum ya kuyatangaza Maeneo na vivutio vya Utalii vinavyopatikana Visiwani Zanzibar.
Alisema Zanzibar ina Historia kubwa ya harakati za Kibiashara kati yake na Mataifa yaliyopo Ghuba ya Uajemi  ambayo inapaswa kujumuishwa katika Agenda hiyo itakayosaidia kuieneza kwa Kizazi cha sasa na kile kijacho.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza na kuishukuru Kuweit kupitia Shirika lake la Misaada ya Maendeleo {Kuweit Fund} kwa jitihada zake za kuunga mkono Miradi ya Maendeleo na Kiuchumi Visiwani Zanzibar iliyochangia kuimarisha Ustawi wa Wananchi wake.
Balozi Seif  alisema uimarikaji wa Sekta ya Afya kwa kuongezeka kwa Vifaa vya Kisasa pamoja na Miundombinu ya Mawasiliano ya Bara bara inayotokana na Misaada ya Nchi hiyo kumeleta faraja kwa Wananchi waliowengi wanaoendelea kupata huduma kupitia miradi hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Balozi huyo wa Kuweit Nchini Tanzania kwamba Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano wake Na Taifa hilo la Kiarabu hasa katika diplomasia ya Kiuchumi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.