Habari za Punde

Kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Na Ali Issa-Maelezo Zanzibar. 8/2/2019
Uongozi wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar unatarajia kukutana na Wafanyabiashara  wa Mikate ya Boflo ili kujadili kupanda bei Bidhaa hiyo muhimu kwa matumizi ya chakula Visiwani Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Hassan Khamis Hafidh huko Baraza la Wakilishi wakati ajibu swali la Mwakilishi wa Mpendae Mohamed Said Dimwa aliyeuliza kuhusu kupanda bei Mikate hiyo.
Amefafanua kwamba Serikali inafuatilia suala hilo na watakutana siku ya Jumapili wiki hii ili kujua sababu za Wafanyabiashara hao kupandisha bei bidhaa hiyo ambayo ni kimbilio la Wananchi wengi katika maisha yao ya kila siku.
Waziri huyo alisema kuwa biashara Zanzibar ipo huria, hivyo kila Mwananchi anaweza kufanya biashara kwa mujibu wa uwezo wa kifedha alio nao pamoja na kuzingatia sheria za nchi.
Amesema hadi sasa Serikali inaamini kuwa mfumko wa biashara Zanzibar unakwenda kwa hali ya kuridhisha na kwa ufanisi ambapo kwa wakati wote Serikali imekuwa katika juhudi za kuhakikisha kuwa biashara za Zanzibar inakua yenye maendeleo kwa kuweka miundo mbinu ya sera na sheria za uendeshaji biashara.
Aidha Naibu huyo aliongeza kusema kuwa serikali iko makini juu ya bei za bidhaa muhimu za chakula kama vile mchele, unga wa ngano na sukariambapo bidhaa hizo ni muhimu kwa matumizi ya wananchi wa Zanzibar.
Hata hivyo alisema alisema kuwa wafanya biashara hupanga bei za bidhaa kwa mujibu wa gharama za ununuzi, gharama za usafirishaji kutoka nchi za nje na gharama za kodi wanazo lipa katika tasisi za Serikali.
Bei ya Mkate mmoja wa Boflo kwa sasa Zanzibar imepanda na kuuzwa kati ya Shilingi 200 hadi 350 wakati bei ya awali ilikuwa shilingi 150 hadi 200.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.