Habari za Punde

Ligi Kuu Zanzibar kutimua vumbi kesho

Na Hawa Abdallah ,ZANZIBAR
PAZIA la michuano ya ligi kuu ya Zanzibar mzunguko wa lala salama unatarajia kuanza kutimua vumbi kesho (FEBR 16 )   siku ya jumaa mosi kwa kupigwa michezo minne katika Dimba la Amaan kisiwani Unguja na Gombani kule kisiwani Pemba.
Katika uwanja wa Amaan majira ya saa  nane mchana JKU ambayo  inashirikilia nafasi ya pili katika msimo wa ligi hiyo  kwa kufikisha alama  38   itapepetana na timu ya Chipukizi kutoka kisiwani Pemba  ambayo ipo nafasi ya 11 ikiwa  na alama 18.
Mchezo wa majira ya Saa kumi utaukutanisha  Vinara wa ligi hiyo Maafande wa KVZ   wenye alama 41 watavaana na timu ya  New star kutoka kisiwani Pemba  ambayo ipo nafasi ya  14 na ikiwana na alama 14.
Huko katika uwanja wa Gombani  Opec watavaana na  timu ya Malindi majira ya saa nane mchana ambapo majira ya saa kumi timu ya Mbuyuni itashuka Dimbani kuumana na Muhustadhi wa Chuoni.
Kocha wa KZV ambae  timu yake inaongoza ligi hiyo Shekha Khamis alisema ni vigumu kusema moja kwa moja kama timu yake itachukua ubingwa wa ligi kuu kwani bado ni mapema mno.
Alisema mara nyingi timu zinapotoka katika Dirisha dogo baadhi huwa zinafanya usajili mzuri na kufanya vizuri ikilinganishwa na mzunguko wa Kwanza jambo ambalo  linakuwa gumu kujipa uhakikia wa kunyakuwa Ubingwa wa ligi kuu kwa msimu huu.
Aidha alisema  hata yeye timu yake inayonafasi ya kunyakuwa ubingwa endapo wachezaji watajituma uwanjani na kutoruhusu kufanya makosa ya kupoteza nafasi watakazo zipata.
“Kama tutafanya vizuri mzunguko huu pia basi tutachukua ubingwa wa Zanzibar, kikubwa wachezaji kujituma tu uwanjani na kutoruhusu magoli  maana mzunguko wa pili kila timu inakuja na kasi mpya ili kujinasua na kushuka daraja.”Alisema.
Katika Msimu huu jumla ya timu sita zitashuka Daraja na katika msimamo wa ligi kuu timu sita za mwisho ambazo zipo katika mstari wa hatari wa kushuka daraja zinatokea  kisiwani Pemba ambazo ni New star, Slem View, Mbuyuni,Hard Rock,Opec  na timu ya Kzimbani ambayo inaburuza mkia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.