Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Ajumuika na Vijana Walioshiriki Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 55 ya Mapinduzi Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. DSk. Ali Mohamed Shein, akiwa na Viongozi  wa meza Kuu baada ya kuwasaili katika Viwanja vya Kambi ya KVZ Mtoni Zanzibar, kulia Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zuberi Ali Maulid, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma na kushoto Kiongozi wa Vijana Walioshirika Halaiki Ndh Ali Mohammed Bakari.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,leo amejumuika pamoja katika chakula cha mchana na mamia ya vijana na wananchi walioshiriki katika sherehe za maadhimisho ya miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar, yaliofanyika kisiwani Pemba Januari 12,  mwaka huu.

Hafla hiyo cha chakula iliyoandaliwa na Rais Dk. Shein, imefanyika  Makao makuu ya Kikosi Cha Valantia, Mtoni mjini hapa, ambapo vijana wa Halaiki kutoka Unguja na Pemba, Umawa na wananchi kwa ujumla walishiriki.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Rais, Waziri wa nchi (OR) na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji ussi ‘’Gavu” amesema ni jambo la faraja kwa Rais kutenga muda na kushirikiana na vijana hao katika chakula hicho , kwa kutambua juhudi kubwa waliyofanya katika kufanikisha vyema sherehe za Mapinduzi mwaka huu. 

Alisema ushiriki wa vijana wadogo katika sherehe hizo  ni kielelezo cha kupanda mbegu njema katika ustawi wa taifa.

Alisema mkusanyiko huo unatowa taswira kwa kiasi gani Wazanzibari wanaweza kujitawala kama ilivyo kwa nchi kadhaa Barani Afrika. 

Aidha, alisema  wananchi wote walioshiriki katika hafla hiyo wameguswa na kujawa na uzalendo na  mapenzi makubwa kwa nchi yao.

Waziri Gavu alitumia fursa hiyo kutoa shukrani za dhati za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa wananchi wote walioitikia wito wa kushiriki katika hafla hiyo adhimu.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein alipokea pongezi kutoka kikundi cha Muziki cha Mafunzo ‘Wajelajela’, baada ya kufanikisha upatikanaji wa vifaa vya muziki kwa ajili ya kukiendeleza kikundi hicho.

Nae, Mwakilishi wa makundi ya washiriki wa sherehe za madhimisho ya miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Mohamed Baraka, alimshukuru Dk. Shein kwa kuwapatia wananchi hao nafasi hiyo.

Ni utamaduni wa kila mwaka unaofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyektii wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wa kula chakula cha mchana pamoja   na makundi yote yanayoshirki katika sherehe za maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Abdi Shamnah, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822  
 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.