Habari za Punde

Saudi Arabia Yaipatia Tanzania Mashine za Kusafishia Damu

Na.Mwandishi Wetu.Dar es Salaam.
SERIKALI kupitia wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yaendelea kusogeza huduma za matibabu ya figo kwa kupokea jumla ya mashine 62 za kusafishia damu kwa wagonjwa wa figo na kuzisambaza katika hospitali za Rufaa za mikoa nchini.
Hayo yamejiri jana katika tukio la kupokea mashine hizo kutoka kwa kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief wakiongozwa na ubalozi wa Saudi Arabia nchini zenye jumla ya shilingi bilion 1.55, lililoongozwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Faustine Ndugulile katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam.
Dk. Ndugulile alisema kuwa serikali inaendelea kusambaza na kuboresha huduma na kwa sasa zinapatikana katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hospitali ya Rufaa Mbeya, hospitali ya Bugando, hospitali ya KCMC na baadhi ya hospitali binafsi.
“Sisi kama serikali tumeendelea kuboresha hizi huduma, kwa sasa hivi zinapatikana Muhimbili, hospitali ya Rufaa Mbeya, hospitali ya Bugando, hospitali ya KCMC na baadhi ya hospitali binafsi”, alisema.
Aliendelea kusema kuwa, serikali inaendelea kuboresha huduma licha ya kuwepo changamoto ya idadi kubwa ya wahitaji wa huduma hizi huku akidai kuwa hospitali ya Taifa Muhimbili kuna mashine 42 huku zikifanyika sesheni tatu kwa siku, na zinafanyika kwa siku 6 katika kila wiki,
Aidha, Dk. Ndugulile alisema kuwa, msaada huo wa vifaa vitavyosambazwa katika mikoa tisa nchini ikiweko mikoa ya Tanga, Mwanza, Kigoma, Kagera, Arusha, Iringa, Mtwara, na Zanzibar, hali itayosaidia kupunguza gharama kwa kuwasogezea wagonjwa huduma hizo.
Mbali na hayo, Dk. Ndugulile alisema kuwa ndani ya miaka mitatu serikali imefanikiwa kupunguza magonjwa ya kuambukiza kwa asilimia 50, huku akikiri kuwa bado kuna changamoto kubwa katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, presha na figo.
“Timepiga hatua kubwa sana katika magonjwa ya kuambukiza, ambayo tumeyapunguza kwa asilimia 50 ndani ya miaka mitatu, tumepunguza vifo na maambukizi ya Malaria, lakini tumepunguza vile vile maambukizi ya Ukimwi, sasa changamoto inayotukabili ni magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama, kisukari, presha na magonjwa ya figo”,alisema Dk. Ndugulile.
Akiongea kwa niaba ya kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief Naibu Balozi wa Saudi Arabia nchini Ahmed Bin Saleh Alghamdi ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa jitihada inayoendelea kuchukua katika kutatua changamoto kwenye sekta ya Afya na aliahidi kuendeleza ushirikiano huo baina ya nchi hizo mbili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.