Habari za Punde

SERIKALI IMEPOKEA GAWIO LA SH. BILIONI 6.8 KUTOKA CRDB

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiipongeza Benki ya CRDB, kwa kuwa Benki ya mfano kwa kutoa gawio la jumla ya Sh. bilioni 10 kwa Serikali, mashirika na taasisi za umma zilizowekeza hisa zao katika Benki hiyo, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Bw. Ally Laay, akieleza kuhusu Benki yake kutoa mikopo katika mradi wa maendeleo wa umeme wa mto Rufiji na ujenzi wa Reli ya Kisasa yenye kiwango cha kimataifa-SGR, wakati wa hafla ya kukabidhi gawio kwa Serikali, mashirika na taasisi zake la Sh. bilioni 10 , katika ukumbi wa Wizara ya Fedha jijini Dodoma.
Baadhi ya wadau waliohudhuria katika hafla ya Serikali  kupokea gawio la Sh. bilioni 10 kutoka Benki ya CRDB, wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani), alipokuwa akizitaka Benki na taasisi zingine za Fedha kutumia mfumo wa malipo kwa njia ya kielektroniki- GePG, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha na Mipango)
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati) akiwa ameshika hundi kifani ya Sh. bilioni 6.8 aliyoipokea kama gawio la Serikali kutoka Benki ya CRDB, kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo  Dkt. Khatibu Kazungu, kushoto ni Balozi wa Denmark nchini Tanzania Bw. Einar Jensen,  wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Bw. Ally Laay na wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw. Abdulmajid Nsekela, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa tano kulia), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa taasisi, mashirika ya umma na Mamlaka ya Serikali za Mitaa waliopata gawio kutoka Benki ya CRDB, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), akipeana mkono na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Bw. Ally Laay, baada ya kupokea gawio kwa niaba ya Serikali, mashirika na taasisi mbalimbali za umma la Sh. bilioni 10, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango,  Dkt. Khatibu Kazungu (kulia), akipeana mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki CRDB, Bw. Abdulmajid Nsekela, baada ya hafla ya Benki hiyo kutoa gawio la Sh. bilioni 10 kwa Serikali, mashirika na taasisi mbalimbali za umma,  katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo  Dkt. Khatibu Kazungu (kulia), Balozi wa Denmark nchini Tanzania Bw. Einar Jensen (kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Bw. Ally Laay (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw. Abdulmajid Nsekela (wa pili kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na wadau wengine baada ya Benki ya CRDB kutoa gawio la Sh. bilioni 10 kwa Serikali, mashirika na taasisi mbalimbali za umma, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha na Mipango)
Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, Dodoma
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  imepokea kiasi cha shilingi bilioni 6.8 ikiwa ni gawio linalotokana na uwekezaji wa asilimia 21 za hisa katika Benki ya CRDB, ikiwa ni sehemu ya shilingi bilioni 10 ambazo benki hiyo imetoa kama gawio kwa mashirika na taasisi mbalimbali za umma zenye hisa katika Benki hiyo kutokana na faida iliyopatikana Mwaka 2018.
Makabidhiano ya mfano wa hundi za gawio hilo yalifanyika jijini Dodoma ambapo Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Philip Isidor Mpango (Mb) alipokea gawio hilo kwa niaba ya Serikali na kukabidhi baadhi ya mashirika na taasisi za umma zilizopata gawio kutoka Benki hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Mpango, aliupongeza uongozi wa benki hiyo kwa kurudisha fadhila kwa mwananchi na kuzitaka benki na taasisi zote za fedha nchini kuiga mfano wa benki hiyo kwa maendeleo ya nchi.
“Benki ya CRDB na benki zingine muongeze jitihada ili kuongeza gawio kwa Serikali ili iweze kuwahudumia wanachi katika huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu na maji”,  alieleza Dkt. Mpango  
Alizitaka benki na taasisi za fedha kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa huduma za benki ili waweze kujikomboa kiuchumi na kuiwezesha nchi kupata gawio kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo.
Dkt. Mpango aliipongeza benki hiyo kwa kuwekeza katika teknolojia hasa katika matumizi ya Mfumo wa Malipo ya Serikali kwa njia ya Kielektroni (GePG) na kuzitaka benki na taasisi zingine za fedha kutumia mfumo huo.
Aidha, Dkt. Mpango alipongeza taasisi na mashirika ya umma yaliyopata gawio kutoka benki hiyo huku akizitaka Serikali za Mitaa nchini kuiga mfano wa Halmashauri za Lindi, Shinyanga na Mbinga ambazo zimepata gawio, ili ziweze kujiendesha na kukuza uchumi wa nchi.
“Serikali za Mitaa zinaweza kufanya njia nyingine mbadala za kujiongezea kipato kama hii ya kuwekeza kwenye Sekta ya fedha “, alisistiza .
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB Bw. Ally Laay alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2018, Benki yake ilitengeneza faida ya shilingi bilioni 64.1 baada ya kukatwa kodi ikilinganishwa na faida ya sh. bilioni 36.2 iliyopatikana Mwaka 2017, huku akichagiza mafanikio hayo na matumizi ya mfumo wa Serikali wa malipo kwa njia ya kielektroniki (GePG).
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Bw. Abdulmajid Nsekela Alisema CRDB imewekeza fedha kwenye mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji katika Mto Rufiji mkoani Pwani na kwamba benki yake iko tayari kuwekeza kwenye ujenzi wa miradi mingine ukiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa kiwango cha Kimataifa (SGR).
Mashirika na taasisi za umma zilizopokea gawio ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma PSSSF (Bil. 2.4), Mfuko wa Hifadhi ya Taifa-NSSF (Mil. 111.5), Mfuko wa Mafao kwa Wafanyakazi wa Serikali-GEPF (Mil. 56,7) , Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar-ZSSF (Mil. 6.5)
Mashirika na taasisi nyingine zilizopokea gawio hilo ambalo ni sehemu ya faida ya shilingi bilioni 21 baada ya kodi kwa mwaka 2018 ni  Mfuko wa Maendeleo Lindi -(Mil. 111.5, Halmashauri ya Manispaa ya Mbinga (Mil. !.3), Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga (Mil. 13.3 na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya-NHIF (Mil.243.5)
Aidha, Chama cha ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi kimepokea gawio la shilingi milioni 228.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.