Kamishina wa Uraia na Pasipoti, Gerald Kihinga
Akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo) Pichani kuhusu kushikiliwa kwa
Mwanahabari, Erick Bendera, katika Mkutano
uliofanyika Ofisi za Idara ya Uhamiaji kanda ya Dar es Salaam.
(Picha na Mpiga
picha Wetu).
Na.
Mwandishi Wetu.31.07.2019.
Serikali kupitia
Idara ya Uhamiaji imetoa ufafanuzi kuhusu Mwandishi wa kujitegemea Erick
Kabendera baada ya kusambaa kwa taarifa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya
kijamii, kuwa amekamatwa na anahojiwa kuhusu uraia wake na Idara ya Uhamiaji
Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Jijini
Dar es Salaam, Kamishna wa Uraia na Pasipoti wa Idara ya Uhamiaji Gerald
Kihinga, amesema kuwa Erick Kabendera
ameshikiliwa na Jeshi la Polisi na Uhamiaji Jijini Dar es Salaam kwa mahojiano
zaidi ili kuweza kupata taarifa juu ya uraia wake.
Kamishna huyo wa
Uhamiaji amesema Idara ya Uhamiaji inadhamana kubwa ya kusimamia na kutekeleza
Sheria ya uraia wa Tanzania sura ya 357 rejeo la 2002, inayotoa mamlaka kwa
taasisi hiyo kuchunguza na kuthibitisha uraia wa mtu yeyote.
“Idara ya Uhamiaji ni
chombo kilichopewa dhamana kubwa ya kutekeleza na kusimamia uraia wa Tanzania,
kwa hiyo siyo mara ya kwanza kufanya hivyo, sisi tunamshikilia Kabendera kwa
mahojiano kuhusu uraia wake, na siyo yeye tu aliyefanyiwa hivyo, idara ya Uhamiaji
inatimiza matakwa ya sheria ya uraia nchini na wala si vinginevyo” Alisema.
Alieleza kuwa idara
ya Uhamiaji ilipata taarifa za Erick Kabendera kutoka kwa raia wema na ikaamua
kumtafuta ili kufanya naye maojiano lakini hakuwa tayari kutoa ushirikiano
ikiwa ni pamoja na kukataa kufika ofisi za Uhamiaji, hali iliyopelekea
kukamatwa na sasa anaendelea kuhojiwa.
Mkuu huyo wa masuala
ya uraia na Pasipoti alifafanua kuwa, kushikiliwa huko kwa Erick Kabendera na
kuendelea na mahojiano ni swala ambalo limekuwepo kwa raia wote ambao uraia wao
una utata, wakiwemo watu wa kawaida, watu mashuhuri na wengine wowote ambao
kutaonekana uhitaji.
Amesema kumekuwa na
ushirikiano baina ya Uhamiaji na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ikwemo Polisi,
ili kutekeleza majukumu mbalimbali ya kiusalama kwa nchi hivyo kukamatwa kwa Kabendera
siyo jambo geni bali Idara inatimiza majukumu yake chini ya Sheria ya uraia wa
Tanzania sura ya 357 rejeo la 2002.
No comments:
Post a Comment