Habari za Punde

Waziri Mhe. Mpina Awapiga Nyundo Nzito Wanaokula Najma za Kumuhujumu Rais Magufuli.

Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Malwilo Kata ya Tindabuligi jimboni Kisesa kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM na mwelekeo ya Serikali ya awamu ya tano.
 Wananchi wa Jimbo la Kisesa wakimpokea Mbunge wao, Luhaga Mpina wakati akiwasili uwanja wa mkutano katika Kijiji cha Malwilo Kata ya Tindabuligi kuwaelezea wananchi juu ya utekelezaji wa  Ilani ya CCM pamoja na mwelekeo wa Serikali ya awamu ya tano.
 Wananchi wa Jimbo la Kisesa wakisalimiana na Mbunge wao Luhaga Mpina wakati akiwasili kwenye uwanja wa mkutano Kijiji cha Malwilo Kata ya Tindabuligi
 Katibu wa CCM Wilaya ya Meatu, Charles Mazuri (katikati) akimpokea Kiongozi maarufu wa CHADEMA Jimbo la Kisesa, Chekinorisi baada ya kujiunga na CCM kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Malwilo Kata ya Tindabuligi. Kushoto ni  Mbunge wa Kisesa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina
Mbunge wa Kisesa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akizungumza na wananchi wa jimbo hilo katika mkutano uliofanyika Kata ya Tindabuligi.

Na Mwandishi Wetu, Simiyu 
MBUNGE wa Jimbo la Kisesa (CCM) Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu, Luhaga Mpina amewashukia  baadhi ya watu waliowahi kupewa nyadhifa za juu serikalini na kwenye Chama cha Mapinduzi kuendesha mikakati na kula njama za kutaka kumuondoa Rais Dk. John Pombe Magufuli kwenye ajenda kuu ya kuwahudumia wananchi na kutaka taifa lijadili mambo ya watu binafsi.

Akizungumza na maelfu ya wananchi wa Jimbo la Kisesa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Malwilo Kata ya Tindabuligi na kuhudhuriwa na wananchi wote wa jimbo hilo, Mpina amesema watanzania wanaimani kubwa na Serikali ya awamu ya tano na kwamba mikakati na njama hizo kamwe hazitafanikiwa.

Mpina amesema viongozi hao hao waliowahi kupewa nafasi za juu ndani ya CCM na Serikali lakini watanzania walishuhudia usimamizi dhaifu wa shughuli za chama na kusababisha makundi makubwa ya viongozi na wanachama kuhamia vyama vya upinzani na kuisababishia CCM na Serikali kuchukiwa na wananchi.

Mpina amesema baada ya Mwenyekiti wa CCM na Rais Dk. Magufuli kufanikiwa kusuka upya mifumo, kufumua mikataba na sheria mbalimbali na kuongeza udhibiti na usimamizi wa rasilimali za nchi pamoja na kupambana na rushwa kwa vitendo na kukomesha mambo machafu yaliyokuwa yanaumiza wananchi ndio wanaibuka watu wachache kutoa waraka na kutaka kuwahamisha wananchi kwenye ajenda kuu ya maendeleo ili wajadili mambo binafsi kwa masilahi yao.

“Walanguzi na wala rushwa waliokuwa wanaiba fedha za taifa hili wamedhibitiwa, mishahara hewa ililipwa miaka nenda rudi viongozi  wakawa wanaimba mishahara hewa kana kwamba hakuna mtu aliyetakiwa kuchukua hatua leo Mheshimiwa John Pombe Magufuli amekuja mishahara hewa yote imekuwa historia” alisema Mpina.

Pia amesema Rais Magufuli amerekebisha mifumo  kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo  sekta ya madini hali iliyowezesha Serikali kuwa na hisa kwenye migodi hiyo ambapo sasa Serikali inapata mabilioni ya fedha kutoka kwenye madini, rasilimali zetu zilikuwa zinaibwa kana kwamba hakuwepo mtu wa kuchukua hatua.

“Uvuvi haramu kila kona samaki walikuwa hakuna Taifa lenye maziwa makubwa kuliko nchi yoyote Afrika na Dunia Taifa lenye bahari samaki tunanunua za kutoka nje Mh. Magufuli akasema uvuvi haramu hapana Mpina nenda pale kakomeshe uvuvi haramu, uvuvi haramu umekoma nchi hii wananchi wanakula samaki wengi na wakubwa kila sehemu na mauzo ya nje yameongeka ”alisema Mpina

Mpina amesema mambo mengine makubwa yaliyosimamiwa na Rais Magufuli ni pamoja na kudhibiti utoroshaji fedha nje ya nchi, biashara ya dawa za kulevya, matumizi ya pombe za viroba, utoroshaji magogo nje ya nchi, uingizaji holela wa bidhaa toka nje na kuua viwanda vya ndani, mikopo ya serikali, matumizi holela ya fedha za umma yote yameshughulikiwa na Serikali ya awamu ya tano.

“Sasa wengine wanaanza kujitokeza na mawaraka yao wataendelea kuyasoma wenyewe watanzania wako bize na maendeleo hawahitaji waraka hatuhitaji waraka sisi, sisi tunahitaji umeme wa uhakika, sisi tunahitaji elimu bora na maji, sisi tunahitaji soko na bei nzuri ya pamba, sisi tunahitaji malisho ya mifugo, sisi tunahitaji usafirishaji wa uhakika treni, ndege, barabara, madaraja na viwanda, sisi tunahitaji hospitali nzuri, tunahitaji dhuluma zote dhidi ya wananchi zikomeshwe, mambo hayo Mhe. Magufuli amekuwa akishughulika nayo kufa na kupona.. sisi hatuhitaji waraka…..waraka wakasome wao na familia zao “alisema Mpina na kuungwa mkono na wananchi.

Amesema mageuzi makubwa aliyoyafanya Rais Magufuli katika kipindi kifupi cha uongozi wake Tanzania haita msahau na Wana CCM hawatamsahau kwa juhudi kubwa alizofanya za kuweka mifumo imara ndani ya Serikali na CCM.

 “Kama ni kwenye chama nani katika historia ya nchi yetu aliyeweza kufanya kama Mh. John Pombe Magufuli nani katika utawala ambaye ameweza kurudisha wabunge 10, madiwani 200 na halmashauri 4  kutoka  upinzani na kujiunga na CCM, huyo ndiye Mhe. John Pombe Magufuli Rais wa wanyonge na hata wagombea wenyewe wa urais kukimbia vyama vyao na kujiunga na CCM rekodi hii haijawahi kuvunjwa na kiongozi yoyote ” alisema Mpina.

Hivyo akawataka watanzania wote waendelee kumuunga mkono Rais Dk. Magufuli ndani ya CCM ndani ya Serikali ili aendelee kupambania maendeleo ya watanzania na kwamba mambo mengi yaliyoshindikana yanatekelezwa katika kipindi chake cha Serikali ya awamu ya tano.

Mpina ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi amewahakikishia wafugaji na wavuvi wote nchini kuwa wako kwenye mikono salama na kwamba Serikali ya Rais Dk. Magufuli iko macho na iko kazini muda wote kushughulikia changamoto zao ili ufugaji na uvuvi uwe na tija na kuleta masilahi makubwa kwa taifa.

Akisoma risala ya wananchi wa Jimbo la Kisesa, Diwani wa Kata ya Tindabuligi, Antony Maghembe alisema wananchi wa jimbo hilo wanamuunga mkono Dk. Magufuli na kumshukuru na kumpongeza kwa kazi kubwa ya kupambania maendeleo ya watanzania, kukomesha dhuluma na kwamba kazi anayoifanya ina Baraka za Mungu na Baraka za wananchi wote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.