Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Akiangalia Meli ya Mafuta ya MT.Ukombozi II Ikipita Bahari ya Kizingo Kuelekea Bandari ya Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein akiwa Ofisini kwake Ikulu Zanzibar akiangalia Meli Mpya ya Mafuta ya MT.Ukombozi II ikiwasili Zanzibar ikitokea Nchini Shanghai China ilikoundwa na Kampuni ya Damen Shipyard ya Uholanzi.
HATIMAE ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyowaahidi wananachi wa Zanzibar kuwa Serikali anayoiongoza itanunua meli mpya ya mafuta MT. UKOMBOZI II leo imetimia baada ya meli hiyo kuwasili katika Bandari ya Zanzibar ikitokea Shanghai nchini China.

Rais Dk. Shein akiwa Ofisini kwake Ikulu mjini Zanzibar alipata fursa ya kuiona meli ya MT UKOMBOZI II ikiwasili kutoka ukingoni mwa pwani ya Zanzibar ikitokea usawa wa kisiwa cha Chumbe na kuelekea katika Bandari ya Malindi Mjini Unguja ilipokwenda kutia nanga.

Akiwa  katika varanda  ya jengo la Ikulu mjini Zanzibar Rais Dk. Shein alionekana akiwa na furaha kubwa wakati akiiangalia meli hiyo ikiwasili ikiwa ni kutokana na ahadi aliyoitoa na azma yake juu ya ujio wa meli hiyo mpya ya mafuta.

Meli hiyo iliyotengenezwa na Kampuni ya Damen Shipyardya nchini Uholanzi iliwasilirasmi katika Bandari ya Malindi Zanzibar majira ya saa saa tano za asubuhi na kupata mapokezi ya aina yake.

Wafanyakazi wa Wizara hiyona viongozi wao pamoja na wafanyakazi wa taasisi nyengine za Serikalina sekta binafsi waliungana pamoja na baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria katika eneo la Bandari ya Malindi mjini Zanzibar kwa ajili ya mapokezi ya meli yao hiyo.

Mapema hapo jana Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, mawasiliano na Usafirishaji Ndg.Mustafa Aboud Jumbe akitoa taarifa kwa wananchi huko ofisi kwake Kisauni, alithibitisha ujio wa meli hiyo na kueleza jinsi hatua mbali mbali zilizochukuliwa katika mchakato wa kununuliwa meli hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi kuwasili kwake hapa nchini hii leo.

Kwa maelezo ya Katibu Mkuu huyo meli mpya MT UKOMBOZI II, ni meli mpya ambapo majadiliano juu ya ujenzi wa meli hiyo yalianza mwaka 2017 na mkukuku wake uliwekwa rasmini mwezi Julai mwaka 2018 na hatimae meli hiyo ujenzi wake ulimalizika mwezi April mwaka huu.2019.

Katibu Jumbe katika taarifa yake alisema kwamba hivi karibuni ujumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ulikwenda kuishuhudia meli hiyo mnamo Julai 8, 2019 ikiwa tayari imeshakamilika na ndipo wakafanya makubaliano na watengenezaji wa meli hiyo ya Kampuni ya DAMEN TANKER SHIP ya Uholanzi iliyoitengeneza meli hiyo.

Ndg.Jumbe alieleza kuwa baada ya makubaliano hayo Meli hiyo iliaza safari ya kusafiri kutoka bandari ya Shanghai nchini China kwa muda wa siku 28 na kuwasili hapo jana katika maji ya pwani ya Zanzibar na leo iliwasili kwa makabidhiano rasmina Serikali na baada ya hapo itazinduliwa kwa ajili ya kuanza shughuli iliyokusudiwa.

Alieleza kuwa meli hiyo ni meli ya mafuta yenye urefu wa mita 86.2 na yenye uwezo wa kupakia tani 3,500 za mafuta kwenye visima 4 vilivyomo katika meli hiyo.

Aidha thamani iliyotumika kuitengeneza meli hiyo ni URO Milioni 14.3 sawa na wastani wa Bilioni 36 za Kitanzania ambapo meli hiyo itaungana na meli ya MT UKOMBOZI I ambayo ipo hapa nchini na yenye uwezo wa kupakia tani 2,400.

Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa madhumuni ya taarifa hiyo aliyoitoa hapo jana jioni ni kuwaarifu wananchi kuwa meli hiyo imeshawasili Zanzibar na maandalizi yanafanywa ili izinduliwe rasmini tayari ameshaombwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa meli hiyo katika siku itakayopangwa.

Aliwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kufuatilia kwa makini juu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kama ilivyo elezwa kwenye ukurasa wa 152 kifungu cha 90 katika kifungu kidogo cha 4 ambacho kimeagiza kwamba Serikali itanunua meli mpya ya mafuta kwa ajili ya matumizi ya Zanzibar.

“Naomba sana kumshukuru Mhe.Rais kwa kutuamini kuisimamia kazi hiyo na hivi sasa tuko ukiongoni katika kuikabidhi meli hiyo”,alisema Ndg.Mustafa Jumbe.

Hizo ni juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein katika kuhakikisha sekta ya usafiri na usafirishaji inaimarika kwa kiasi kikubwa ambapo mnamo mwezi Disemba mwaka 2015 meli mpya ya MV MAPINDUZI IIiliwasili Zanzibar ikitokea nchini Korea Kusini ilikotengenezwa ikiwani agizo la Rais Dk. Shein la kununuliwa meli hiyo.

MV MAPINDUZI II ambayo ilitengenezwa na Kampuni ya Daewoo International ya nchini Korea Kusini ilianza kutengenezwa Julai mwaka 2013 na hadi Disemba 2015 iliwasili Zanzibar ikiwa tayari kuanza kutumika.

Jumla ya Dola za Marekani 30.4 zilitumika kutengenezea meli hiyo ambapo ujenzi wake hadi kukamilika ulichukua miezi 18 ambapo meli hiyo ya MV MAPINDUZI II inauwezo wa kuchukua abiria 1200 pamoja na tani 200 z amizigo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.