Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt.John Pombe Magufuli akihutubia katika ufunguzi wa Maonesho ya Wiki ya
Viwanda ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika(SADC), katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC)
Na.Paschal
Dotto-MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli amefungua maonesho ya wiki ya
viwanda kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC).
Akizungumza katika
hafla hiyo ya Wiki ya Viwanda ya SADC jana, Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli
amesema kuwa ili kufikia uchumi wa kati viwanda ni kichochea muhimu katika
sekta nyingi kwani uwepo wa viwanda utasababisha uhakika wa uzalishaji na
uchakataji wa bidhaa na kufanyabiashara kwa nchi wananchama.
Rais Magufuli amezitaka
nchi wanachama wa SADC kuweka kipaumbele kwenye kuhuisha teknolojia katika
viwanda vilivyoko ndani ya jumuiya ya Maendelea kusini mwa afrika (SADC) pamoja
na kushughulikia kwa haraka zaidi vikwazo vinavyochelewesha ukuaji wa viwanda.
“Viwanda ni Sekta
muhimu katika kukuza uchumi wa nchi yeyote, kuondoa umasikini, kuongeza ajira
na Sekta hii imeziletea Maendeleo makubwa nchi zilizoendelea, kwa hiyo mkutano
huu ni dhahiri kuwa sasa nchi za SADC zimeanza kuchukua hatua madhubuti za
kukuza sekta hii na ikiwa mkakati huu utatekelezwa utasaidia kukuza uchumi wa
nchi zetu”, Rais Magufuli.
Akielezea suala la
teknolojia Rais Magufuli amesema kuwa ukuzaji wa teknolojia na ubunifu kwenye
sekta ya viwanda ni silaha muhimu kwa nchi za SADC kuendelea na kutegemeana
kwani utazalisha ajira, biashara kubwa, na kuepuka kuuza malighafi kwa wingi nje ya Afrika kama ilivyosasa.
Vilevile, mchango wa sekta ya viwanda kwa nchi za SADC
bado ni mdogo kwani Sekta hiyo inachangia wastani wa asilimia 10 ya pato la
taifa na katika Jumuiya ya SADC sekta hiyo muhimu inachangia asilimia 11 tu.
Amesema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli
alizitaka nchi wanachama wa SADC kujikita zaidi katika kukuza ubunifu na
teknolojia rahisi kwenye sekta ya viwanda kwa kuwaendeleza vijana na kuimarisha
viwanda vidogo vidogo vilivyoko kwenye jumuiya, kwa hiyo wiki ya viwanda ni
fursa muhimu kwa nchi zote wananchama.
“Wiki ya Viwanda ya
SADC ni fursa ya kubadilishana uzoefu miongoni mwa wadau kuhusu utekelezaji wa
mikakati ya miaka 49 ya uendelezaji wa viwanda katika jumuiya yetu, bado
tunasafari ndefu kuhakikisha sekta ya viwanda inazidi kukua na kuleta mageuzi
ya kiuchumi katika nchi zetu”, Amesema Rais Magufuli
Rais Magufuli amesisistiza
kwa kusema kuwa katika kuimarisha mashirikiano ndani ya Jumuiya ya Maendeleo (SADC)
ni lazima kuimarisha sekta ya uwekezaji kwani nchi hizo zina fursa nyingi kwenye
uwekezaji ikiwemo viwanda vya madini, kilimo, uvuvi na ufugaji kwa hiyo
wananchi kutoka SADC wanatakiwa kuchangamkia fursa kwenye soko la takribani
watu milioni 344.
Kwa upande wake
Waziri wa Viwanda na Biashara wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Innocent
Bashungwa amesema kuwa uthubutu wa Rais Magufuli kuipeleka Tanzania katika
uchumi wa kati wenye viwanda ni mkubwa na matokea yake
yanaonekana sasa. Hivyo, maonesho haya ni moja ya njia muhimu ya
kuimarisha sekta ya viwanda nchini.
“Maonesho haya ya
wiki ya viwanda yanawawezesha wanachama wa SADC kuona namna nchi wenyeji
inavyotekeleza uwekezaji kwenye sekta ya Viwanda. Aidha, tunaamini wazalishaji, wafanyabiashara, na
wananchi kwa ujumla watachangamkia fursa mbalimbali zitazotokana na mkutano huu
wa SADC.”, Waziri Bashungwa.
Waziri Bashungwa
alisema kuwa Tanzania inafanya vizuri kwenye biashara ndani ya SADC kwani takwimu zinaonyesha kuwa mauzo ya
Tanzania kwenda SADC mwaka 2018 yalikuwa dola za kimarekani milioni 999
ikilinganishwa na dola za kimarekani milioni 875 mwaka 2017 ikiwa na ongezeko
la asilimia 12.16.
Naye Waziri wa
Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Amina Ally amesema
kuwa uthubutu wa Rais Magufuli wa kuendeleza ndoto ya Baba wa Taifa, Mwl .
Julius Nyerere kwa kujenga bwawa Kubwa la kufua na kuzalisha umeme mto Rufiji
ni hatua kubwa kwa maendeleo ya sekta ya viwanda.
Balozi Amina alisema
kuwa katika utekelezaji wa miradi yote inayofanywa na Serikali suala muhimu ni
uwepo wa amani kwa Tanzania na ndiyo maana ikachaguliwa kuwa mwenyeji wa
maonesho ya SADC yakifuatiwa na Mkutano mkuu wa viongozi wakuu wa nchi za wanachama
wa SADC.
“Tanzania itaendelea
kuwa kisiwa cha amani na kwa tukio hili itaendelea kudumisha amani na utilivu
kwani mpaka sasa maonesho na mkutano mkuu unaofanyika hapa unaonesha kuwa
tanzania ni nchi ya amani”, Waziri wa Viwanda Zanzibar, Amesema Balozi Amina
Ally.
Kwa upande wake
Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt.Stagomena Tax, amesema kuwa juhudi za Serikali ya
Tanzania kutekeleza mradi mkubwa wa kufua na kuzalisha umeme mto Rufiji ni moja
ya njia madhubuti katika kuimarisha na kukuza sekta ya viwanda kwa Jumuiya ya
SADC.
“Kutekelezwa kwa
Mradi wa umeme mto rufiji tunaamini kuwa Tanzania itazalisha umeme wa kutosha,
tunaomba ziada iweze kwenda kwenye nchi wanachama wa SADC kwani kumekuwa na
changamoto ya kubwa mgawo wa umeme na uendeshwaji wa viwanda unahitaji mambo
mengi ikiwemo umeme huwezi kuwa na viwanda bila kuwa na umeme unaozalishwa kwa
urahisi, kwa hiyo Tanzania imechukuia maamuzi mazuri kuzalisha umeme mto
Rufiji.”, Stagomena Tax, Katibu Mtendaji, SADC.
Aidha Dkt.Stagomena
aliwaomba watanzania kutumia fursa zilizopo nchi wanachama SADC kwa kuwa ni
soko kubwa ambalo linajumuisha nchi 16, ambazo zinawatu wapatao milioni 344 na
pato la taifa la pamoja la dola za Marekani milioni 2.5 hivyo ni muhimu kwa
watanzania kuzijua fursa hizo na kuzitumia ipasavyo.
Maonesho ya Wiki ya
Viwanda yanayofanyika Tanzania kuanzia tarehe 05 mpaka 9 Agosti 2019 na
kufatiwa na Mkutano wa wakuu wa nchi 16 wanachama utakaofanyika Agosti 17 na
18, 2019, katika Ukumbi wa Julius
Nyerere Dar-es-salaam.
No comments:
Post a Comment